Wanajeshi wa Israel washambulia waumini wa Kiislamu karibu na Msikiti wa Al-Aqsa

Mji wa Al-Quds (Jerusalem) unaokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel Ijumaa ulishuhudia vikosi vya Israel vikitumia gesi ya kutoa machozi na nguvu ziada kwa ajili ya kuwatawanya waumini karibu na eneo la Msikiti wa Al-Aqsa huku watu wengi wakiugua kwa kuvuta gesi hiyo ya machozi.



Mapigano hayo yalizuka katika mtaa wa Wadi al-Joz, karibu na eneo hilo takatifu, ambapo waumini walikuwa wamekusanyika kwa ajili ya Swala ya Ijumaa. Walizuiwa kuingia Msikiti wa Al-Aqsa kwa wiki ya 11 mfululizo kutokana na vikwazo vya utawala dhalimu wa Israel.


Vikosi vya utawala katili wa Israel pia viliwalenga waandishi wa habari waliokuwa wakiripoti tukio hilo, kuwashambulia na kuwaondoa katika eneo hilo. Video zinazosambaa mtandaoni zinaonyesha wanajeshi wa Israel wakiwarushia mabomu ya machozi waumini waliokuwa wakielekea msikitini.


Ni waumini 12,000 pekee ndio waliweza kuingia katika Msikiti wa Al-Aqsa, kutokana na vizuizi vilivyowekwa na utawala haramu wa Israel.


Vikosi vya utawala vamizi wa Israel pia vilifunga milango ya msikiti na kutowaruhusu kuingia humo wale wanaoishi nje ya Mji Mkongwe wa al-Quds.



Wanaharakati wameendelea kutoa wito kwa watu kukusanyika na kuswali huko Al-Aqsa, licha ya juhudi za Israel za kutaka kukoloni na kubadilisha hadhi ya kihistoria na kidini ya eneo hilo takatifu. Katika miezi ya hivi karibuni, walowezi wa Kizayuni wenye misimamo mikali wameingia mara kwa mara katika eneo hilo takatifu chini ya ulinzi wa majeshi ya Israel.


Msikiti wa Al-Aqsa ni eneo la tatu kwa utakatifu katika Uislamu baada ya Masjid al-Haram huko Makka na Masjid al-Nabawi huko Madina. Utawala wa Kizayuni unatekeleza njama ya muda mrefu ya kupora eneo hilo takatifu la Waislamu na kujenga mahala pake hekalu la Kizayuni.