Fataawaa Mas-ala 60 Kuhusu Hedhi Na Nifaas
31-Akipata Hedhi Baada Ya Kuingia Wakati Wa Swalaah
Au Akitoharika Kabla Ya Kutoka Wakati
Imaam Ibn 'Uthaymiyn (Rahimahu-Allaah)
SWALI:
Muulizaji anauliza: Ni nini hukumu ya mwanamke akiingia kwenye hedhi baada ya kuingia wakati wa Swalaah? Je yampasa ailipe akitoharika? Na vile vile akitoharika kabla ya kutoka wakati wa Swalaah?
JIBU:
Kwanza: Mwanamke akiingia katika hedhi baada ya kuingia wakati yaani baada ya kuingia wakati wa Swalaah inampasa kwake akitoharika kuilipa Swalaah ile kama hakuiswali kabla ya kumjia hedhi kwa kauli ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
من أدرك ركعة من الصلاة فقد أدرك الصلاة
“Atakayediriki rakaa katika Swalaah basi ameidiriki Swalaah yenyewe.”
Hivyo kama mwanamke ameidiriki Swalaah kiasi cha rakaa kisha ikamjia hedhi kabla ya kuswali basi akitoharika itamlazimu kuilipa.
Pili: Akitoharika na hedhi kabla ya kuondoka kwa wakati wa Swalaah itampasa ailipe Swalaah ile. Na akitoharika kabla ya kuchomoza kwa jua kwa kiasi cha rakaa basi inampasa kuilipa Swalaah ya Alfajiri. Na akitoharika kabla ya kuzama kwa jua kwa kiasi cha rakaa basi ni juu yake kulipa Swalaah ya Alasiri. Na akitoharika kabla ya kufikia nusu ya usiku kwa kadiri ya rakaa, basi inamwajibikia alipe Swalaah ya ‘Ishaa. Akitoharika baada ya kufikia nusu ya usiku, haimwajibikii kulipa Swalaah ya ‘Ishaa, bali aswali Alfajiri itakapofika wakati wake. Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:
فَإِذَا اطْمَأْنَنتُمْ فَأَقِيمُوا الصَّلَاةَ ۚ إِنَّ الصَّلَاةَ كَانَتْ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ كِتَابًا مَّوْقُوتًا
Mtakapopata utulivu, simamisheni Swalaah (kama desturi), hakika Swalaah kwa Waumini ni fardhi iliyowekwa nyakati maalumu)). [An-Nisaa (4:103)]
Yaani faradhi yenye wakati maalum haimpasi mtu kuiacha Swalaah kutoka katika wakati wake hajaswali au kuianza kabla ya kuingia wakati wake.
0 Comments