بِسْمِ اللّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ


UTANGULIZI

Himdi Anastahiki Allaah (سبحانه وتعالى) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) na Maswahaba wake(رضي الله عنهم)  na wote waliowafuata kwa ihsaan mpaka Siku ya Mwisho.

Qur-aan ni Maneno matukufu ya Allaah Aliyoteremshiwa Nabiy wa mwisho Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) yenye kusadikisha yale yaliyokuja kabla yake katika Vitabu vilivyotangulia na ni Maneno yasiyoweza kufikiwa na upotofu mbele yake wala nyuma yake kama Anavyosema Allaah (سبحانه وتعالى):
لَّا يَأْتِيهِ الْبَاطِلُ مِن بَيْنِ يَدَيْهِ وَلَا مِنْ خَلْفِهِۖ تَنزِيلٌ مِّنْ حَكِيمٍ حَمِيدٍ﴿٤٢﴾
Hakitofikiwa kitabu hicho na ubatilifu mbele yake, wala nyuma yake; ni uteremsho kutoka kwa Allaah Mwenye hikmah wa yote, Mwenye kustahiki kuhimidiwa kwa yote.[1]


Pia Qur-aan ni Kitabu cha mwisho chenye ujumbe kwa viumbe wote kutoka kwa Rabb wa walimwengu, kwa lengo la kuwaongoza viumbe kwenye njia iliyonyooka; na ni mwongozo, rahmah na shifaa kwa Waumini.

Pia Qur-aan ni muujiza wa pekee, na wakati huo huo ni changamoto kwa viumbe wote. Hata kama viumbe vyote hivyo vitashirikiana ili vilete mfano wa Qur-aan basi havitoweza kuleta mfano wake; katika ufasaha wake, hukumu zake, elimu zake, mwongozo wake na yote iliyoyaelezea.[2]

Qur-aan imekusanya yale yote yenye kuhitajiwa na viumbe; yawe ya dunia au Aakhirah yao, zikiwemo khabari za kabla yao na khabari za baada yao, na ni muamuzi na hakimu kwa Waumini wake; na ni Kitabu Alichohitimishia Allaah shariy’ah Zake.

Ni katika desturi Zake Allaah (سبحانه وتعالى) kuwa kila Rasuli akitumwa huwa anapelekwa kwa lugha ya watu wake ili aweze kuwafikishia ujumbe, Allaah (سبحانه وتعالى) Anasema:
وَمَا أَرْسَلْنَا مِن رَّسُولٍ إِلَّا بِلِسَانِ قَوْمِهِ لِيُبَيِّنَ لَهُمْ ۖ
Na Hatukutuma Rasuli yeyote isipokuwa kwa lugha ya kaumu yake ili awabainishie (ujumbe).[3]

Ni jambo lenye kujulikana kuwa lugha ya Ma-Quraysh na ndio lugha ya Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) ilikuwa ya Kiarabu bayana; hivyo ujumbe uliokuja ndani ya Qur-aan ulikuja katika lugha ya Kiarabu, ambayo ndiyo lugha fasaha kuliko lugha zote.[4]

Usomaji wa Qur-aan katika lugha yake, kwa walengwa wake wengi wasiokuwa Waarabu ambao hawakuafikishwa kuisoma lugha ya Kiarabu na kuifahamu vizuri, haswa Qur-aan na elimu zake, haukuweza kuwafikisha kufahamu misingi ya Dini yao, hivyo basi, ndio pakawa na haja na umuhimu mkubwa wa kuweko Tarjama itakayoweza kumsaidia Muislamu kuweza kufikia kufahamu anachosemeshwa na Rabb wake; iwe maamrisho au makatazo apate kutekeleza.

Elimu ya Tarjama ilibuniwa na kupelekea kuweko Tarjama nyingi sana katika kila zama na kila pahala na kwa lugha maarufu za walimwengu, jambo lililopelekea kumfikisha mlengwa kuweza kufahamu mengi katika aliyotakiwa ayafahamu kulikomfikisha kutekeleza na upande mwengine kuitakidi kama alivyofikishiwa na hizo Tarjama.

Tarjama nyingi huenda zikawa zimefanikiwa kumfikisha mlengwa kufahamu maneno ya Allaah (سبحانه وتعالى) kwa kiasi fulani na kufahamu baadhi ya makusudio ya Ayaat katika upande wa shariy’ah. Ama kwenye upande wa itikadi, Tarjama nyingi miongoni mwa hizo, kwa masikitiko makubwa, hazikufanikiwa kumfikisha Muislamu pale alipotakiwa afike kiitikadi kwa sababu moja au nyingine; kwa kuwa kwenye Tarjama hizo kuna mchanganyiko wa itikadi zisizo sahihi na fikra za kifalsafa mbalimbali au fikra za wale wenye upotofu ndani ya nyoyo zao wenye kufuata hawaa za nafsi zao.

Baada ya kuzipitia Tarjama zote za Kiswahili zenye kujulikana kuwa ni za watu wenye kunasibishwa na Ahlus-Sunnah wal-Jamaa’ah tumeweza kugundua kuwa kuna upungufu huo wa kumfikisha Muislamu mwenye kuzungumza Kiswahili pale alipotakiwa kufika kiitikadi; itikadi iliyobalighishwa na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم). Hivyo, hakujapatikana Tarjama inayorandana na itikadi ya Salafus-Swaalih (Wema waliotangulia) miongoni mwa MaswahabaTaabi’iyn na Atbaa'Taabi’iyn na waliowafuata kwa wema.[5]

Kwa minajili hiyo, tukaona kuna umuhimu wa kuweko kwa Tarjama itayokwenda sambamba na Manhaj ya Salaf haswa katika kuibalighisha na kuidhihirisha ile itikadi iliyobalighishwa na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) ambayo iko wazi kwenye Qur-aan kwa atakaye kushikamana nayo.[6]

Ni vyema ifahamike kuwa, Tarjama hii au nyingine yoyote ile, lengo lake kuu ni kuwasaidia walengwa kuweza kufikia kuifahamu Qur-aan, kutakowafikisha kuwaidhika na kuitendea kazi, haswa katika Aayah zenye kuhusiana na ‘Aqiydah yao ili wapate kuitakidi vile wanavyotarajiwa waitakidi kama walivyokuwa wakiitakidi Salaf (Maswahaba na wale waliowafuata kiitikadi na mwenendo).

Tarjama ni jaribio la kuuweka wazi ujumbe na kufikisha makusudio yake kwa walengwa kwa kiasi cha uwezo wa mwana Aadam, na Tarjama ni fani miongoni mwa fani za sayansi ya Qur-aan; sayansi ambayo inazungumzia kila lenye kufungamana na Qur-aan kuanzia kuteremka kwake, Suwrah zake, Aayah zake (za mwanzo na za mwisho kuteremka), sababu za kuteremka kwa Aayah au Suwrah, ukusanyaji wake, mpangilio wa Aayah na Suwrah zake, visa vyake, mifano yake, kujibu tuhuma dhidi yake na kadhalika.

Mkusanyiko wa hayo yote na mengineyo ndani ya sayansi hiyo unadhihirisha kuwa kunahitajika uangalifu mkubwa katika kukata shauri na kutoa hukumu kuhusu maana ya Maneno ya Allaah (سبحانه وتعالى). Ndio ikawa njia pekee sahihi na ya salama ya kufanikisha hilo, ni kwa kushikamana na kutegemea yale yaliyopokelewa na kuthibiti kutoka kwa Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلمna Maswahaba (رضي الله عنهم)na wala si kutokana na rai.

La msingi na lililo muhimu katika kazi ya Tarjama ambalo ni sharti katika masharti ya anayefanya hiyo Tarjama awe mtu mwenye kushikamana na msingi madhubuti wa kufuata manhaj ya Salaf na wala si msingi wa kuzusha au ubunifu na wala asiwe mtu wa hawaa. Atakapokuwa ameshikamana na manhaj sahihi ya Salaf, basi hivyo ndivyo kutampeleka na kumlazimisha kama ni sehemu ya itikadi yake kushikamana na zile Tarjama zenye kwenda sambamba na mafundisho ya Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم), zenye kunukuu kauli za Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم), au kauli za Maswahaba (رضي الله عنهم) au kauli za Taabi’iynna Atbaa’ Taabi’iyn.

Kutokana na hali hii basi, Mufassiriyna wameweka Manhaj maalumu ya Tafsiyr ya kufuatwa na kushikiliwa na ambayo kwayo kwa kuipitia vizuri, ndipo tutaweza kufikia kupata Tarjama iliyo sahihi.

1.      Tafsiyr ya Qur-aan kwa Qur-aan
Kufasiri Qur-aan kwa Qur-aan ndio njia ya kwanza inayopasa kufuatwa; kwani Qur-aan inajifasiri yenyewe kwa yenyewe. Utakuta pahala inaeleza jambo kwa kifupi na pahala pengine inalieleza jambo hilo hilo kwa ufafanuzi na kwa uchambuzi. Jambo inalolieleza kwa ujumla katika sehemu moja hulieleza kwa kuliwekea ima mipaka au kulihusisha kwa watu makhsusi katika sehemu nyingine. Hivyo, njia iliyo sahihi kabisa katika kufasiri Qur-aan, ni kufasiri Qur-aan kwa Qur-aan.[7]
Ibn Al-Qayyim (رحمه الله) amesema:
“Kufasiri Qur-aan kwa Qur-aan ni njia bora kabisa inayofikisha ujumbe na kuufafanua. Na si ajabu kwani Allaah (سبحانه وتعالىni Mjuzi wa malengo na makusudio Yake. Anafafanua Aayah Zake kwa Aayah nyinginezo. Allaah (سبحانه وتعالى) Anasema:
وَكَذَٰلِكَ نُصَرِّفُ الْآيَاتِ وَلِيَقُولُوا دَرَسْتَ وَلِنُبَيِّنَهُ لِقَوْمٍ يَعْلَمُونَ ﴿١٠٥﴾
Na hivyo ndivyo Tunavyosarifu namna kwa namna Aayaat (ishara, dalili) na wao (makafiri) waseme: “Umedurusu” (kutoka Ahlil-Kitaab) na ili Tuibainishe kwa watu wenye kujua.[8]

Ni jambo lisilopingika kuwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa akifahamu kikamilifu kila kilichoelezwa ndani ya Qur-aan; na ndio akawa wa kwanza kufasiri Qur-aan kwa Qur-aan kama ilivyopokewakuwa alifasiri baadhi ya Aayah kwa Aayah nyinginezo.[9]

Maswahaba (رضي الله عنهم) walishuhudia na kumsikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akifasiri Qur-aan kwa Qur-aan; hivyo nao kama ilivyo desturi yao walimuiga katika hilo pia kama walivyokuwa wakimuiga katika mengineyo; na kwa kufahamu kuwa ni jukumu lao kufikisha kila walichochukua kutoka kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) na kuwafikishia wataokuja baada yao. Maswahaba (رضي الله عنهم) waliwafunza wanafunzi wao Taabi’iyn kila walichopokea kutoka kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) tena kwa muradi wake Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم). Taabi’iyn nao waliwafunza wanafunzi wao Atbaa’ Taabi’iyn kila walichopokea na kuchukua kutoka kwa waalimu wao ambao ni Maswahaba (رضي الله عنهم)nao kwa upande wao walinukuu na kufikisha kwa waliokuja baada yao tena kwa muradi ule ule walioupokea na kuuchukua kutoka kwa Maswahaba wa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) na katika waliyoyapokea ni aina hii ya kufasiri Qur-aan kwa Qur-aan.

Hivyo, haijuzu wala si sahihi kuiacha aina hii ya Tafsiyr na kuiendea nyingine ikiwa Aayah husika ina Aayah nyingine iliyoifasiri kama ilivyo katika mifano ifuatayo:
Kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى):
Na Kwake (Allaah) zipo funguo za ghayb; hakuna azijuaye ila Yeye tu. Na Anajua yale yote yaliyomo barani na baharini. Na halianguki jani lolote ila Hulijua, na wala punje katika viza vya ardhi, na wala kilichorutubika na wala kikavu isipokuwa kimo katika Kitabu kinachobainisha wazi.[10]

Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) aliwabainishia na kuwawekea wazi kuwa funguo za ghayb ni tano; kwa kuwasomea kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى) ifuatayo:
 إِنَّ اللَّـهَ عِندَهُ عِلْمُ السَّاعَةِ وَيُنَزِّلُ الْغَيْثَ وَيَعْلَمُ مَا فِي الْأَرْحَامِ ۖ وَمَا تَدْرِي نَفْسٌ مَّاذَا تَكْسِبُ غَدًا ۖ وَمَا تَدْرِي نَفْسٌ بِأَيِّ أَرْضٍ تَمُوتُ ۚ إِنَّ اللَّـهَ عَلِيمٌ خَبِيرٌ ﴿٣٤﴾
Hakika Allaah Ana elimu ya Saa, na Anateremsha mvua na Anajua yale yaliyomo katika tumbo la uzazi na nafsi yoyote haijui nini itachuma kesho, na nafsi yoyote haijui itafia katika ardhi gani, hakika Allaah ni Mjuzi wa yote, Mwenye upeo wa khabari za dhahiri na za kufichika.[11]

Mfano mwengine ni pale Allaah (سبحانه وتعالى) Anaposema:
الَّذِينَ آمَنُوا وَلَمْ يَلْبِسُوا إِيمَانَهُم بِظُلْمٍ أُولَـٰئِكَ لَهُمُ الْأَمْنُ وَهُم مُّهْتَدُونَ ﴿٨٢﴾
Wale walioamini na hawakuchanganya iymaan zao na dhulma; hao ndio watakaopata amani nao ndio walioongoka.[12]

Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم) aliwabainishia na kuwawekea wazi kuwa dhulma ni shirki; kwa kuwasomea Aayah ifuatayo:
وَإِذْ قَالَ لُقْمَانُ لِابْنِهِ وَهُوَ يَعِظُهُ يَا بُنَيَّ لَا تُشْرِكْ بِاللَّـهِ ۖ إِنَّ الشِّرْكَ لَظُلْمٌ عَظِيمٌ ﴿١٣﴾
Na Luqmaan alipomwambia mwanawe huku akimuwaidhi: “Ee mwanangu! Usimshirikishe Allaah, hakika shirki ni dhulma kubwa mno!”[13]


2.      Kufasiri Qur-aan kwa Sunnah za Nabiy Muhammad (صلى الله عليه وآله وسلم)[14]
Sunnah ni tafsiyr, kishereheshaji na kibainifu cha Qur-aan kwa kudhihirisha yasiyokuwa dhahiri. Sunnah inaisherehesha Qur-aan kwa kuyachambua, kuyapambanua na kwa kuyaainisha yale ambayo Qur-aan imeyaelezea kwa ujumla. Sunnah inaweka mipaka kwa yale yasiyokuwa yamewekewa mipaka na Qur-aan. Sunnah inayachambua yaliyotolewa hukumu kwa pamoja, ikifafanua yaliyoachwa wazi hukumu zake; yote kwa kuwa katika Qur-aan kuna yasiyoweza kufahamika isipokuwa kwa kupata ufafanuzi na kuwekwa wazi na Sunnah za Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم); kama vile uchambuzi wake (صلى الله عليه وآله وسلم) katika namna za amri na makatazo, idadi za Rakaa za Swalaah, viwango vya yale Aliyofaradhisha Allaah (سبحانه وتعالى) katika hukumu.[15]


Ufafanuzi wa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) ni kitu kisichoweza kuepukika; na ndio akaweka wazi kwa kusema kuwa hakupewa Qur-aan pekee, bali alipewa pamoja na Qur-aan kinachofanana nayo.[16]

Umahiri katika lugha ya Kiarabu pekee haukuwa wenye kutosheleza wala hautatosheleza katika kufahamu kusudio la Maneno ya Allaah (سبحانه وتعالى) bila ya kutafuta msaada kutoka kwenye Sunnah. Kama ilivyokuwa hali kwa Maswahaba (رضي الله عنهم) japokuwa walikuwa wenye ufasaha na umiliki kamili wa lugha ya Kiarabulakini walikuwa wakitatanishwa au wakati mwengine wakifahamu baadhi za Aayah kinyume na inavyotakiwa ifahamike, jambo lililowapelekea kurejea kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) kwa kutafuta ufafanuzi.

Kuna mifano mingi tu ya Aayah za Qur-aan ambapo Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amezifasiri na kuzifafanua. Tafsiyr au ufafanuzi wake (صلى الله عليه وآله وسلم) uko wa namna mbili; hufasiri Aayah au neno ambalo Maswahaba (رضي الله عنهم) hawakuweza kuifahamu tafsiyr yake au walipofahamu kinyume na inavyotakiwa ifahamike.

Mfano neno قُوَّةٍ (nguvu):
Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alifasiri neno قُوَّةٍ katika Aayah ya Al-Anfaal kuwa ni Ar-Ramyu:
 وَأَعِدُّوا لَهُم مَّا اسْتَطَعْتُم مِّن قُوَّةٍ
“Na waandalieni nguvu zozote mziwezazo.”[17]
Tafsiyr ya nenقُوَّةٍ kuwa ni Ar-Ramyu limepatikana katika usimulizi ufuatao:
عَنْ عُقْبَةَ بْن عَامِر يَقُولُ: سَمِعْتُ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ وَهُوَ عَلَى الْمِنْبَرِ يَقُولُ: ((وَأَعِدُّوا لَهُمْ مَا اسْتَطَعْتُمْ مِنْ قُوَّةٍ... أَلَا إِنَّ الْقُوَّةَ الرَّمْيُ، أَلَا إِنَّ الْقُوَّةَ الرَّمْيُ، أَلَا إِنَّ الْقُوَّةَ الرَّمْيُ))
‘Uqbah bin ‘Aamir (رضي الله عنه) amehadithia kwamba: “Nimemsikia Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) hali akiwa yu juu ya minbar akisema: “Na waandalieni nguvu kama muwezavyo…” Tanabahi! Hakika Al-Quwwah ni Ar-Ramyu (kutupa mshale, kulenga kwa kutumia silaha)hakika Al-Quwwah ni Ar-Ramyu, hakika Al-Quwwah ni Ar-Ramyu.”[18]

Mfano mwengine ni neno الْكَوْثَرَ
Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alilifasiri nenoالْكَوْثَرَ katika Suwrah Al-Kawthar:
إِنَّا أَعْطَيْنَاكَ الْكَوْثَرَ ﴿١﴾
Hakika Sisi Tumekupa (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلمAl-Kawthar (Mto katika Jannah)[19]

kuwa ni Mto katika Jannnah, maana ambayo haikufahamika isipokuwa kwa njia ya kufafanuliwa na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلمkatika Hadiyth ifuatayo:
عَنْ أَنَسٍ (رضي الله عنه) ((إِنَّا أَعْطَيْنَاكَ الْكَوْثَرَ)) أَنّ النَّبِيَّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ، قَالَ: ((هُوَ نَهْرٌ فِي الْجَنَّةِ))
Anas (رضي الله عنه) amehadithia (kuhusu kauli yake Allaah): Hakika Sisi Tumekupa Al-Kawthar”kuwa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Huo ni Mto katika Jannah.”[20]

Mfano mwengine ni neno زِيَادَةٌ
Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alifasiri kwa kubainisha kuwa neno زِيَادَةٌ katikaAayah ya Suwrah Yuwnus,
لِّلَّذِينَ أَحْسَنُوا الْحُسْنَىٰ وَزِيَادَةٌ ۖ
Kwa wale waliofanya ihsaan watapata (jazaa) nzuri kabisa na ziada (kumuona Allaah Jannah).[21]


Kuwa ni kumuona Allaah Ta’aalaa; maana ambayo haikufahamika isipokuwa kwa njia ya ufafanuzi wa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلمkatika Hadiyth ifuatayo:

عَنْ صُهَيْبٍ (رضي الله عنه) قَالَ: قَالَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((إِذَا دَخَلَ أَهْلُ الْجَنَّةِ الْجَنَّةَ نُودُوا: يَا أَهْلَ الْجَنَّةِ، إِنَّ لَكُمْ عِنْدَ اللَّهِ مَوْعِدًا لَمْ تَرَوْهُ، فَقَالُوا: وَمَا هُوَ؟ أَلَمْ تُبَيِّضْ وُجُوهَنَا وَتُزَحْزِحْنَا عَنِ النَّارِ، وَتُدْخِلْنَا الْجَنَّةَ؟)) قَالَ: ((فَيُكْشَفُ الْحِجَابُ، فَيَنْظُرُونَ إِلَيْهِ، فَوَاللَّهِ مَا أَعْطَاهُمْ اللَّهُ شَيْئًا أَحَبَّ إِلَيْهِمْ مِنْهُ)) ثُمَّ تَلاَ رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ: ((لِلَّذِينَ أَحْسَنُوا الْحُسْنَى وَزِيَادَةٌ))
Swuhayb (رضي الله عنه) amehadithia kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema: “Watakapoingia Ahlul-Jannah katika Jannah; wataitwa: Ee Ahlal-Jannah! Hakika nyinyi mna ahadi kwa Rabb wenu bado hamjaiona; watauliza: ‘Ni (ahadi) ipi hiyo? Kwani Hukuzing’arisha nyuso zetu, na Hukutuokoa na moto, na Hukutuingiza Jannah?’” Akasema: “Litaondoshwa pazia, na watamtazama Allaah; Naapa kwa Jina la Allaah Hakuwahi Allaah kuwapa kitu wanachokipenda zaidi kuliko huko (kumuona Allaah).” Kisha Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) akasoma Aayah hii: Kwa wale waliofanya ihsaan watapata (jazaa) nzuri kabisa na ziada (kumuona Allaah Jannah).[22]

Hii inathibitisha kuwa ufafanuzi wa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) ni wenye umuhimu mkubwa katika kufasiri Qur-aan kwani ni ufafanuzi wa aina yake pekee na wenye thamani isiyoweza kununulika wala kukadirika ndio ikawa Qur-aan inaihitaji Sunnah (Hadiyth); na ndio ikawa hakuna kitabu katika vitabu vya Hadiyth isipokuwa kutakuwepo mlango wa Tafsiyr Maathuwr.[23]

  
3.      Kufasiri Qur-aan kwa kauli za Maswahaba (رضي الله عنهم) 
Kauli (tafsiyr) za Maswahaba  (رضي الله عنهم)ni chanzo cha tatu cha kutafuta ufafanuzi pale inapokuwa haujapatikana ufafanuzi kutoka vyanzo viwili vilivyotangulia, kama alivyosema Al-Haafidhw Ibn Kathiyr katika utangulizi wa Tafsiyr yake kuwa: “Tutakapokuwa hatukufanikiwa kupata Tafsiyr katika Qur-aan au Sunnah, tutarejea katika kauli za Maswahaba (رضي الله عنهم) kwani wao waliifahamu Qur-aan vilivyo kwa ufasaha na sarufi zake, na kwa kuwa walishuhudia matukio yaliyosababisha kuteremshwa kwa Aayah au Suwrah husika, hakuna aliyeyashuhudia isipokuwa wao, na pia kutokana na kuwa na na elimu sahihi na ‘amali njema haswa haswa Wanachuoni miongoni mwao.”[24]

Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alibainisha na kufafanua kwa kufasiri maana za Aayah za Qur-aan kwa Maswahaba zake (رضي الله عنهم) kama inavyoashiria kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى):
لِتُبَيِّنَ لِلنَّاسِ مَا نُزِّلَ إِلَيْهِمْ
“…ili uwabainishie watu yaliyoteremshwa kwao...”[25]

Maswahaba (رضي الله عنهم) walijifunza Qur-aan na elimu yake kwa kina kutoka kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم).[26]

Hata hivyo, ufahamu wa Maswahaba (رضي الله عنهم) wa Qur-aan na ufahamu wao haukuwa wa daraja moja; kwani miongoni mwao (رضي الله عنهم) wako waliojulikana kuwa ni wafasiri wa Qur-aan; kama vile Makhalifa wanne (رضي الله عنهم), Ibn Mas’uwd[27] ambaye alikuwa akijulikana miongoni mwa Maswahaba kuwa ni mjuzi wao wa Qur-aan (kuisoma na kuifasiri). Ibn ‘Abbaas (رضي الله عنهما),[28] pia Mama wa Waumini ‘Aaishah (رضي الله عنها) na wengineo ambao walikuwa na ufahamu uliokamilika kwa vile ulijengeka juu ya elimu iliyo sahihi iliyopambika kwa ‘amali swaalih. Hivyo, tafsiyr zao zina thamani, uzito na umuhimu mkubwa mpaka ikawa tafsiyr ya Maswahaba inachukua hukumu ya Al-Marfuw’[29] haswa inapojulikana kuwa Swahaba huyo hakuwahi kupokea Israaiyliyyaat katika hilo.

Kilichojitokeza ni kuwa hakuna tafsiyr iliyoandikwa katika wakati wao, kwani ilikuwa ni sehemu katika Hadiyth.
Mfano wa Tafsiyr ya neno  لَامَسْتُمُ (mmewagusa) kuwa ni kujimai katika kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى):
 أَوْ لَامَسْتُمُ النِّسَاءَ
“au mmewagusa wanawake.”[30]
Ibn ‘Abbaas alilitafsiri kwa kusema kuwa: “Ni kujimai.”[31]

Mfano mwengine ni kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى):
وَمِنَ النَّاسِ مَن يَشْتَرِي لَهْوَ الْحَدِيثِ لِيُضِلَّ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ بِغَيْرِ عِلْمٍ وَيَتَّخِذَهَا هُزُوًا ۚ
Na miongoni mwa watu yuko ambaye hununua maneno ya upuuzi ili apoteze (watu) njia ya Allaah bila elimu, na huichukulia mzaha. Hao watapata adhabu ya kudhalilisha.[32]

Ibn Mas'uwd (رضي الله عنه) amesema kuhusu Aayah hii: “Naapa kwa Jina la Allaah hii inamaanisha ni muziki.”[33]

Mfano mwengine ni kuhusu kufanya sa’y baina ya majabali mawili ya Swafaa na Marwah kulikotajwa kwenye kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى):
إِنَّ الصَّفَا وَالْمَرْوَةَ مِن شَعَائِرِ اللَّـهِ ۖ فَمَنْ حَجَّ الْبَيْتَ أَوِ اعْتَمَرَ فَلَا جُنَاحَ عَلَيْهِ أَن يَطَّوَّفَ بِهِمَا ۚ
Hakika Asw-Swafaa na Al-Marwah ni katika alama za Allaah. Basi yeyote anayehiji kwenye Nyumba hiyo au akatekeleza ‘Umrah basi hakuna lawama kwake kutufu (vilima) viwili hivyo[34] 
Baadhi ya Maswahaba (رضي الله عنهم) walifahamu kinyume na vile inavyotakiwa ifahamike Aayah hiyo. Mmojawao ni baba wa Hishaam bin ‘Urwah Akamuuliza Mama wa Waumini ‘Aaishah (رضي الله عنها) ambaye alimfahamisha kwa kutumia ‘sabab an-nuzuwl’ (sababu iliyopelekea kuteremka Aayah) ili aweze kufahamu usahihi wa maana ya Aayah kama ilivyothibiti katika kauli ya Mama wa Waumini ‘Aaishah (رضي الله عنها)katika usimulizi ufuatao:
عَنْ هِشَامِ بْنِ عُرْوَةَ، عَنْ أَبِيهِ، أَنَّهُ قَالَ: قُلْتُ لِعَائِشَةَ زَوْجِ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ، وَأَنَا يَوْمَئِذٍ حَدِيثُ السِّنِّ: "أَرَأَيْتِ قَوْلَ اللَّهِ تَبَارَكَ وَتَعَالَى: ((إِنَّ الصَّفَا وَالْمَرْوَةَ مِنْ شَعَائِرِ اللَّهِ فَمَنْ حَجَّ الْبَيْتَ أَوِ اعْتَمَرَ فَلا جُنَاحَ عَلَيْهِ أَنْ يَطَّوَّفَ بِهِمَا))  فَمَا أُرَى عَلَى أَحَدٍ شَيْئًا أَنْ لَا يَطَّوَّفَ بِهِمَا، فَقَالَتْ عَائِشَةُ: "كَلَّا، لَوْ كَانَتْ كَمَا تَقُولُ، كَانَتْ فَلَا جُنَاحَ عَلَيْهِ أَنْ لَا يَطَّوَّفَ بِهِمَا، إِنَّمَا أُنْزِلَتْ هَذِهِ الْآيَةُ فِي الْأَنْصَارِ كَانُوا يُهِلُّونَ لِمَنَاةَ، وَكَانَتْ مَنَاةُ حَذْوَ قُدَيْدٍ، وَكَانُوا يَتَحَرَّجُونَ أَنْ يَطُوفُوا بَيْنَ الصَّفَا وَالْمَرْوَةِ، فَلَمَّا جَاءَ الْإِسْلَامُ سَأَلُوا رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ عَنْ ذَلِكَ، فَأَنْزَلَ اللَّهُ: ((إِنَّ الصَّفَا وَالْمَرْوَةَ مِنْ شَعَائِرِ اللَّهِ فَمَنْ حَجَّ الْبَيْتَ أَوِ اعْتَمَرَ فَلا جُنَاحَ عَلَيْهِ أَنْ يَطَّوَّفَ بِهِمَا))
Kutoka kwa Hishaam bin ‘Urwah kutoka kwa baba yake kwamba alisema: Nilimwambia ‘Aaishah (رضي الله عنها) mke wa Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم), na mimi wakati huo ni kijana mdogo: “Unaionaje kauli ya Allaah Tabaaraka wa Ta’aalaa: Hakika Asw-Swafaa na Al-Marwah ni katika alama za Allaah. Basi yeyote anayehiji kwenye Nyumba hiyo au akatekeleza ‘Umrah basi hakuna lawama kwake kutufu (vilima) viwili hivyo”[35]Sioni kama kutakuwa na kitu (dhambi) juu ya yeyote ikiwa hatofanya sa’y baina ya majabali mawili haya.” Mama wa Waumini ‘Aaishah (رضي الله عنها) alisema: “Si hivyo; lau ingelikuwa kama unavyosema basi ingekuwa (hivi): “Hakutokuwa na dhambi juu yake kama hatotufu baina ya (vilima) viwili hivyo.” Kwa hakika Aayah hii imeteremshwa kuhusiana na Answaar walikuwa wakihiji kwa Manaat (wakiliabudu sanamu hilo na wakilifanyia Hijjah na wakilitufu), lakini walikuwa hawatufu (sa’y baina ya Swafaa na Marwah) na lilikuwa hilo sanamu la Manaat likielekea (kijiji cha) Qadiyd, hivyo walikuwa wakiona tabu kulitufu. Ulipokuja Uislamu walimuuliza Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) kuhusu hivyo (kwenda sa’y baina ya Swafaa na Marwah), ndio Allaah Akateremsha: Hakika Asw-Swafaa na Al-Marwah ni katika alama za Allaah. Basi yeyote anayehiji kwenye Nyumba hiyo au akatekeleza ‘Umrah basi hakuna lawama kwake kutufu (vilima) viwili hivyo.”[36]


4.      Kufasiri Qur-aan kwa kauli za Taabi’iyn
Kutakaposhindwa kupatikana Tafsiyr ya Aayah husika kwenye Qur-aan, au kwenye Sunnah, au kwenye kauli za Maswahaba (رضي الله عنهم); ‘Ulamaa hurejea kwenye kauli za Taabi’iyn;[37] kwani kama walivyotajika baadhi ya Maswahaba (رضي الله عنهم) kwa Tafsiyr, wametajika pia baadhi ya Taabi’iyn kwa Tafsiyr.[38]

Taabi’iyn walitegemea katika Tafsiyr zao, ufahamu wao wa Qur-aan kutokana na yaliyokuja ndani ya Qur-aan yenyewe, na yale waliyoyapokea kutokana na Maswahaba (رضي الله عنهم), kutoka kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم), na yale Aliyowafungulia Allaah kupitia njia ya ijtihaad na utafiti wao katika Qur-aan na wala hawakuwa tayari kutumia rai zao.[39]

Kinachofahamika ni kuwa Tafsiyr zilizopokelewa kutokana na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلمna pia kutokana na Maswahaba (رضي الله عنهم) hazikuwa za Qur-aan yote, bali zilikuwa ni zenye kuhusiana na baadhi ya Aayah za Qur-aan au baadhi ya maneno ya Aayah ambayo yaliyoonekana kuwa ni miongoni mwa yale yenye kuhitaji ufafanuzi kwa wale waliokuwa katika zama hizo.  Kutofahamika huku, huwa kunazidi kila pale wanapobaidika watu na zama za Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) na Maswahaba (رضي الله عنهم); hivyo wale wenye kujishughulisha na fani ya Tafsiyr miongoni mwa Taabi’iyn, wakaongeza katika Tafsiyr kadiri ya kule kuongezeka kutofahamika; kisha baada yao wakaja wale waliokamilisha Tafsiyr ya Qur-aan huku wakitegemea juu ya yale waliyoyafahamu katika lugha na lahaja za Waarabu, na juu ya yale yaliyothibiti kuwa ni sahihi kwao katika matukio yaliyotokea wakati wa kushuka kwa Qur-aan na mengineo.

Taabi’iyn wametunukiwa daraja ya kuwa miongoni mwa watu bora kabisa[40]kwa kuwa walichukua na kuchota elimu zao kutoka vyanzo sahihi na vilivyoasisiwa kwa misingi sahihi.

Mfano wa Tafsiyr ya neno قَانِتُونَ katika Kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى):
 كُلٌّ لَّهُ قَانِتُونَ ﴿١١٦﴾
...vyote vinamtii.[41]
Kuhusiana na neno قَانِتُونَMujaahid alilifasiri kwa kusema kuwa: “Ni kutii: na kuwa utiifu wa kafiri hupatikana pale kivuli chake kinaposujudu, wakati ambapo yeye mwenyewe (kafiri) ni mwenye kuchukia hilo.”[42]

Mfano mwengine ni kuhusiana na Kauli ya Allaah (سبحانه وتعالى):
قَالَ أَنَا أُحْيِي وَأُمِيتُ ﴿٢٥٨﴾
“... akasema: “Mimi (pia) nahuisha na nafisha...[43]
Kuhusiana na ibara hii: ‘Mimi (pia) nahuisha na nafisha,’ Qataadah amesema kuwa yule mfalme aliyemuhoji Nabiy Ibraahiym (عليه السلامalimaanisha kuwa: Watu wawili waliostahiki kuuawa, wangeletwa mbele yake, na angeliamrisha mmoja wao auawe na angeliuawa; na angeliamrisha kuwa mtu wa pili asamehewe na angesamehewa; hivi ndivyo ninavyoleta uhai na kifo.”[44]
Hivyo Tafsiyr ya Taabi’iyn ni chanzo chengine cha kutafuta ufafanuzi pale inapokuwa haujapatikana ufafanuzi kutoka kwenye vyanzo vilivyotangulia.  Hata hivyo baadhi ya Wanachuoni wanaonelea kuwa Tafsiyr za Taabi’iyn na wanafunzi wao hazitoki moja kwa moja kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلمna wala si kama Tafsiyr za Maswahaba (رضي الله عنهم), yote kwa kuwa Taabi’iyn na wanafunzi wao hawajamuona Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) na wala hawakushuhudia Wahy pale zinapoteremshwa Aayah; na vilevile si wote wanakubalika uaminifu wao, kwa kuwa wao si kama Maswahaba (رضي الله عنهم) ambao uaminifu na uadilifu wao umeshuhudiwa na kuthibitishwa na Qur-aan. Ama wao Taabi’iyn na wanafunzi wao wamesifiwa kama ni ‘kizazi’ na si mmoja mmoja.


Hata hivyo, maelezo mazuri na ya salama ni yale ya Shu’bah bin Al-Hajjaaj na wengineo ambayo ameyanukuu Shaykh Al-Islaam Ibn Taymiyyah: “Kauli za Taabi’iyn katika furuw’ (matawi ya Shariy’ah) si hoja, basi vipi zitakuwa hoja katika Tafsiyr. Kwa maana kuwa haziwi hoja juu ya wengineo wasiokuwa wao miongoni mwa wale waliowakhalifu; na hii ndio sahihi. Ama pale watakapokubaliana juu ya kitu, basi bila shaka yoyote ile ni hoja, na endapo watakhitalifiana basi haitokuwa kauli ya baadhi yao hoja juu ya wengine, na wala juu ya watakaokuja baada yao, bali kutafuatwa na kutazamwa lugha ya Qur-aan, au Sunnah, au kauli za Maswahaba (رضي الله عنهم).“[45]

Hakuna shaka yoyote ile kwamba ujuzi wa lugha ya Kiarabu, na matawi yake una mchango mkubwa na ni ufunguo katika kuifahamu Qur-aan na kuweza kupata Tafsiyr yenye kukubalika. Hivyo basi, ufahamu sahihi wa Tafsiyr ya Qur-aan, makusudio yake na yote yenye kufungamana nayo, unafungamana pia na ufahamu sahihi wa lugha ya Kiarabu na matawi yake.

Kadhaalika, kuna elimu na fani nyingi ambazo zimefungamana na kushikamana na Qur-aan zenye kuweza kusaidia katika kufikia kufahamu Tafsiyr ya Aayah; kama vile elimu ya Uswuwl ya Tafsiyr pamoja na kutabahari (kubobea) katika fani zote zile ambazo hakuna njia ya kufahamika Tafsiyr wala kuwa sahihi isipokuwa kwayo, kama vile kufahamu sababu za kuteremka kwa Aayah (Asbaab An-Nuzuwl), Naasikh wa Mansuwkh (kinachofuta na kilichofutwa), na kadhalika. Hivyo, Tafsiyr inayokubalika ni ile yenye kufuata Manhaj iliyoelezwa juu inayotegemea zaidi nukuu badala ya mawazo au rai ya Mfasiri.

Tarjama hii kwa lugha ya Kiswahili si Tarjama mpya, bali ni katika yale yanayohitajika kufanywa kwa Tarjama zilizopo kama ni huduma muhimu ya kujaribu kuzifikisha daraja ya kukubalika kiitikadi kutakozipelekea kuwa sahihi kiitikadi kwa kuthibitisha yale yote yaliyothibiti tena bila ya kuleta Ta'twiyl[46]wala kuleta Tamthiyl[47] wala kuleta Takyiyf[48] na wala kuleta Tahriyf[49], kisha kushikamana na hiyo itikadi kama vile walivyokuwa wameshikamana nayo Salaf.

Haitarajiwi Tarjama hii kuja na kipya kisichowahi kuthibiti au kusikiwa au kuandikwa, bali ni Tarjama inayotarajiwa kujaribu kuhuisha kwa kuyathibitisha yale yote yaliyothibiti kwa kusahihisha na kurekebisha pale palipokwenda kombo katika Tarjama za Kiswahili haswa haswa katika uwanja wa ‘Aqiydah na zaidi kumpwekesha Allaah (سبحانه وتعالى) katika Majina Yake na Sifa Zake na kumsifia kama Alivyojisifu Yeye Mwenyewe (سبحانه وتعالى) au alivyomsifu Rasuli Wake (صلى الله عليه وآله وسلم) bila ya kuzibadilisha sifa hizo, wala kuzigeuza wala kuzifananisha wala kuzipindua maana yake. Hivyo tumemthibitishia Allaah (سبحانه وتعالى) yale yote Aliyojithibitishia Mwenyewe (سبحانه وتعالى) kuanzia neno ‘mkono’, ‘uso’, ‘kuja’, ‘kuteremka’, na kadhalika.  Na jambo hili huenda likaonekana kuwa ni jipya na si la kawaida kwa baadhi yetu, na hali ni kuithibitisha itikadi ya Ahlus-Sunnah wal-Jamaa’ah (Salaf), itikadi ambayo imepokelewa kutoka kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) na ni itikadi ya Maswahaba zake (رضي الله عنهم) na ni itikadi ya kila aliyewafuata kwa ihsaan mpaka Siku ya Qiyaamah.

Tarjama itathibitisha maneno hayo na mengine kama hayo kama yalivyothibitishwa na Qur-aan na Sunnah sahihi za Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلمbila ya kumithilisha au kukanusha na kukataa, kwa visingizio kuwa yakithibitishwa kama yalivyothibitibasi kuna khofu kuwa atashabihishwa Muumba na viumbe Vyake! Hiyo si hoja muwafaka, kwani iymaan thabiti ya Muislamu kuhusiana na Allaah (سبحانه وتعالى) ni kuwa: Hapana anayefanana Naye (Muumba) hata mmoja wala hakuna kitu chochote mfano Wake kama inavyothibitishwa na Allaah (سبحانه وتعالى) Mwenyewe.[50]

Kwa hiyo, lengo kubwa la kuifanya kazi hii, ni kujaribu kuifanya iwe karibu kabisa na Tafsiyr za Salaf kwa kuchunga mas-alah yote ya ‘AQIYDAH na mengine muhimu kwa kuleta maana za karibu na sahihi zilizopokelewa na kuthibiti.

Tumeona ni vyema na ndio sahihi ndani ya kazi hii pia, kulithibitisha Jina ‘Allaah’ badala ya kulifasiri kwa kuligeuza na kutumia neno ‘Mwenyezi Mungu’, kama linavyotumika katika karibu Tarjama zote za lugha ya Kiswahili. Ni iymaan yetu kuwa kulithibitisha jina Lake ‘Allaah’, kama lilivyothibiti, ni kumuadhimisha Yeye Allaah (سبحانه وتعالى) na kulipa haki Jina Lake Tukufu; na kubwa na la muhimu zaidi ni kuwa kuna thawabu kwa kuwa ndivyo lilivyothibiti. Hivyo, tutalitumia na kulithibitisha Jina la ‘Allaah’ pote katika Tarjama hii kama lilivyothibitishwa na Qur-aan na Sunnah za Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلمkwa lengo la kuwarejesha Waumini katika kutumia Majina ya Allaah kama yalivyothibiti.

Hali kadhaalika, tumethibitisha Sifa ya Allaah (سبحانه وتعالى) ya “Rabb” kwa kuibakisha kama ilivyo katika asli yake bila kuipa maana; kwa sababu neno “Rabb” linatumika Kiswahili kama “Rabi” na linafahamika, vilevile kulipa maana ya “Mola” tumeona ni maana finyu isiyokidhi taarifu kamili ya “Rabb”. “Ar-Rabb” Ina maana nyingi na pana. Inaweza kumaanisha; Mfalme, Bwana, Mlezi, Mwendeshaji na Mpangaji, Mola, Msimamiaji, Mwenye Kuneemesha n.k. Hivyo, tumeonelea litumike kwenye Tarjama hii hivyo hivyo lilivyo.

Na katika Tarjama hii tumeona muhimu kutaja Asbaab An-Nuzuwl zilizo sahihi ili msomaji afahamu sababu ya kuteremshwa Aayah na apate ladha ya kufahamu sababu mbalimbali zilizosababisha kuteremshwa Aayah au Suwrah fulani, na hivyo kuongeza faida ya elimu yake ya Qur-aan.

Vilevile, tumeongezea baadhi ya faida za ziada ili nazo zimpanulie ufahamu msomaji na kumuongezea elimu na ufahamu wa Qur-aan kwa kina.


Tumetegemea zaidi katika kuikamilisha kazi hii Tafsiyr zifuatazo:

·       تفسير القرآن العظيم للإمام الحافظ ابن كثير
Tafsiyr Al-Qur-aan Al-‘Adhwiym ya Al-Haafidhw ‘Imaad Ad-Diyn Abi Al-Fidaa Ismaa’iyl bin Kathiyr.

au maarufu kama ‘Tafsiyr Ibn Kathiyr
·       تفسير ابن كثير

·       تيسير الكريم الرحمن في تفسير كلام المنان
Taysiyr Al-Kariym Ar-Rahmaan Fiy Tafsiyr Kalaam Al-Manaan ya Al-‘Allaamah Ash-Shaykh ‘Abdur-Rahmaan bin Naaswir As-Sa’diy.
au maarufu kama ‘Tafsiyr As-Sa’diy.
تفسير السعدي

·       التفسير الميسر - نخبة من العلماء
At-Tafsiyr Al-Muyassar – Nukhbat Minal ‘Ulamaa

Na Tarjama (Tarjama) ifuatayo ya Kiingereza:
·        Interpretation of The Meanings of THE NOBLE QUR’AN IN THE ENGLISH LANGUAGE (a Summarized Version of At-Tabari, Al-Qurtubi and Ibn Kathir with Comments from Sahih Al-Bukhari – Dr. Muhammad Taqi-ud-Diyn Al-Hilaaliy, Dr Muhammad Muhsin Khan.

Mwisho tunamshukuru Allaah (سبحانه وتعالى) kwa kutuwafikisha kuweza kuikamilisha kazi hii tukufu, kazi ambayo ni jukumu kubwa mbele ya Allaah (سبحانه وتعالى) na wala hatusemi kuwa Tarjama hii itakuwa haina kasoro, kwani hakuna mkamilifu isipokuwa Allaah (سبحانه وتعالى).

Tunawaomba ndugu zetu watuarifu kwa kosa lolote lile watakaloligundua au kasoro yoyote ile watakayoiona.

Tunamuomba Allaah (سبحانه وتعالى) Atughufurie kwa makosa yetu na Aijaalie kazi hii iwe ni kwa ajili ya kuzipata radhi Zake Pekee na Atutakabalie.
Na Allaah Anajua zaidi

الحمد لله رب العالمين وصلى الله على محمد وعلى آله واصحابه وسلم



Imeandaliwa Na:  Alhidaaya.com 
Imechapishwa Na:  Muislamu.com 




[1]Fusw-swilat (41: 42).
[2]Allaah (سبحانه وتعالى) Anasema:
قُل لَّئِنِ اجْتَمَعَتِ الْإِنسُ وَالْجِنُّ عَلَىٰ أَن يَأْتُوا بِمِثْلِ هَـٰذَا الْقُرْآنِ لَا يَأْتُونَ بِمِثْلِهِ وَلَوْ كَانَ بَعْضُهُمْ لِبَعْضٍ ظَهِيرًا ﴿٨٨
Sema: “Ikiwa watajumuika wana Aadam na majini ili walete mfano wa hii Qur-aan; hawatoweza kuleta mfano wake, japokuwa watasaidiana wao kwa wao.” [Al-Israa 17:88].
[3]Ibraahiym (14: 4).
[4]Allaah (سبحانه وتعالى) Anasema:
وَلَقَدْ نَعْلَمُ أَنَّهُمْ يَقُولُونَ إِنَّمَا يُعَلِّمُهُ بَشَرٌ ۗ لِّسَانُ الَّذِي يُلْحِدُونَ إِلَيْهِ أَعْجَمِيٌّ وَهَـٰذَا لِسَانٌ عَرَبِيٌّ مُّبِينٌ ﴿١٠٣﴾
Na kwa yakini Tunajua kwamba wao wanasema: “Hakika hapana isipokuwa mtu anamfundisha (Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم Qur-aan).” Lisani wanayomnasibishia nao ni ya kigeni, na hii ni lisani ya Kiarabu bayana. [An-Nahl 16:103].

[5]Mfano wa haraka ni kama neno ‘Istawaa’ katika Aayah ya 5 ya Suwrah ya 20 (Twaahaa), Tarjuma za Kiswahili zilizoko hivi sasa, karibu zote zinaeleza ‘istiwaa’ (kulingana, kuwa juu) kuwa maana yake ‘istawlaa’ ni ‘kutawala’, kinyume na ufahamu na tafsiyr ya Salaf ya neno hilo. Msimamo wa Salaf katika tafsiyr ya Aayah hiyo ni kama huu uliopokelewa kuwa, Ja’far bin ‘Abdillaah na wengine miongoni mwao walisema: “Tulikuwa kwa Imaam Maalik bin Anas basi akatokea mtu akamuuliza? Ee Abaa ‘Abdillaah! Allaah (سبحانه وتعالى) Anasema:
الرَّحْمَـٰنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَىٰ ﴿٥
“Ar-Rahmaan; juu ya Arshi Istawaa (Yuko juu kwa namna inayolingana na Utukufu Wake Yeye Mwenyewe Allaah).” [Twaahaa 20: 5]. 
Je, vipi Istawaa? Basi Imaam Maalik hakuwahi kughadhibika kutokana na kitu chochote kile kama alivyoghadhibika kutokana na swali la mtu huyo, kisha (Imaam Maalik) akatazama chini na huku akikwaruza kwaruza kwa kijiti kilichokuwa kwenye mkono wake mpaka akarowa jasho, kisha akanyanyua kichwa chake na kukirembea kile kijiti kisha akasema: ‘Vipi’ ni ghayr-ma’quwl(hakutambuliki), na al-Istiwaa ghayr-maj-huwl (si jambo lisilojulikana), na kuamini hilo ni waajib (lazima), na kuuliza (au kuhoji hilo) ni bid’ah (uzushi); na nina khofu kuwa wewe ni mzushi.” Akaamrisha mtu huyo atolewe; basi akatolewa.” 
Imesimuliwa kwenye Al-Hilyah (6/325-326) na pia imesimuliwa na Abu ‘Uthmaan Asw-Swaabuniy katika ‘Aqiydatus Salaf Asw-haab Al-Hadiyth (uk. 17-18), kutoka kwa Ja’far bin ‘Abdillaah kutoka kwa Maalik na Ibn ‘Abdil-Barr katika At-Tamhiyd (7/151) kutoka kwa ‘Abdullaah bin Naafi’ kutoka kwa Maalik na Al-Bayhaqiyy katika Al-Asmaa wasw-Swifaat (uk. 408) kutoka kwa ‘Abdullaah bin Wahb kutoka kwa Maalik; Ibn Hajr amesema katika Al-Fat-h (13/406-407) mlolongo wake ni mzuri na imesahihishwa na Adh-Dhahabiy katika Al-‘Uluww (uk. 103). Shaykh Al-Albaaniy amesema Hadiyth hii ni SwahiyhMukhthaswar Al-‘Uluww - Imaam Adh-Dhahabiy iliyopitiwa na Shaykh Muhammad Naaswirud-Diyn Al-Albaaniy (uk. 131).
[6]Salaf ni Maswahaba (رضي الله عنهم) na wanafunzi wao -Taabi’iyn- na wanafunzi wa wanafunzi wao -Atbaa’ Taabi’iyn-. Hawa ni wale aliowataja Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) kuwa ni watu bora kabisa wa karne zote.

[7]Tazama Sharh Kitaab Muqaddimah fiy Uswuwl At-Tafsiyr - Ibn Taymiyyah.
[8]Al-An’aam (6: 105).
[9]Allaah (سبحانه وتعالى) Anasema:
إِنَّ عَلَيْنَا جَمْعَهُ وَقُرْآنَهُ ﴿١٧﴾ فَإِذَا قَرَأْنَاهُ فَاتَّبِعْ قُرْآنَهُ ﴿١٨﴾ ثُمَّ إِنَّ عَلَيْنَا بَيَانَهُ ﴿١٩﴾
Hakika ni juu Yetu kuikusanya na kukuwezesha kuisoma kwake. Basi Tunapoisoma (kupitia Jibriyl), fuata kusomwa kwake. Kisha ni juu Yetu kuibainisha (kwako).” [Al-Qiyaamah 75: 17-19].

[10]Al-An’aam (6: 59).
[11]Luqmaan (31: 13).
[12]Al-An‘aam (6:  82).
[13]Luqmaan (31: 13).
[14]Sunnah (Hadiyth) ni kila kilichonasibishwa kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) katika kauli au kitendo au yale aliyoyakubali au sifa za kimaumbile au tabia au mwenendo.
[15]Hakika kila kile alichohukumu kwacho Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) ni katika yale aliyoyaelewa (صلى الله عليه وآله وسلمkutokana na Qur-aan; kama alivyosema Imaam Ash-Shaafi’y; taz. Sharh Kitaab Muqaddimah fiy Uswuwl At-Tafsiyr. Allaah (سبحانه وتعالى)Anasema:
إِنَّا أَنزَلْنَا إِلَيْكَ الْكِتَابَ بِالْحَقِّ لِتَحْكُمَ بَيْنَ النَّاسِ بِمَا أَرَاكَ اللَّـهُ ۚ وَلَا تَكُن لِّلْخَائِنِينَ خَصِيمًا ﴿١٠٥﴾
Hakika Sisi Tumekuteremshia (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) Kitabu kwa haki ili uhukumu baina ya watu kwa Aliyokuonyesha Allaah. Wala usiwe mtetezi kwa makhaini. [An Nisaa 4: 105]; pia Allaah (سبحانه وتعالى) Anasema:
وَمَا أَنزَلْنَا عَلَيْكَ الْكِتَابَ إِلَّا لِتُبَيِّنَ لَهُمُ الَّذِي اخْتَلَفُوا فِيهِ ۙ وَهُدًى وَرَحْمَةً لِّقَوْمٍ يُؤْمِنُونَ ﴿٦٤﴾
Na Hatukukuteremshia Kitabu isipokuwa uwabainishie yale waliyokhitilafiana kwayo, na ni mwongozo na rahmah kwa watu wanaoamini.” [An Nahl 16: 64].
[16]Kama ilivyothibiti kuwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema
((أَلَا إِنِّي أُوتِيتُ الْقُرْآنَ وَمِثْلَهُ، أَلَا يُوشِكُ رَجُلٌ يَنْثَنِي شَبْعَانًا عَلَى أَرِيكَتِهِ يَقُولُ: "عَلَيْكُمْ بِالْقُرْآنِ فَمَا وَجَدْتُمْ فِيهِ مِنْ حَلَال فَأَحِلُّوهُ وَمَا وَجَدْتُمْ فِيهِمِنْ حَرَامٍ فَحَرِّمُوهُ... ((رواه أبو داود والترمذي والحاكم وصححه وأحمد بسند صحيح
“Tanabahi! Hakika nimepewa Qur-aan na inayofanana nayo (Sunnah) Tanabahi! Utafika wakati mtu aliyeshiba mno ataegemea kwenye kochi na kusema: “Shikamaneni na Qur-aan, mtakayokuta humo ya halali halalisheni, na mtakayokuta ya haramu haramisheni.” [Imepokewa na Abu Daawuwd, na At-Tirmidhiy, na Al-Haakim na ameisahihisha Ahmad kwa isnaad Swahiyh].

[17]Al-Anfaal (8: 60).
[18]Muslim, katika Kitabu cha Al-Imaarah, mlango wa fadhila za Ar-Ramyu na ushajiishaji wake; na At-Tirmidhiy, katika Kitabu cha Tafsiyr ya Qur-aan, mlango na katika Suwrah Al-Anfaal.
[19]Al-Kawthar (108: 1).
[20]Al-Bukhaariy, katika Kitabu cha Tafsiyr ya Qur-aan, Tafsiyr Suwrat Al-Kawthar, At-Tirmidhiy, katika Kitabu cha Tafsiyr ya Qur-aan, mlango na katika Suwrah Al-Kawthar.
[21]Yuwnus (10: 26).
[22]Ahmad, katika Musnad Kumi waliobashiriwa Jannah, Ukamilisho wa Musnad ya Kuufiyyiyn; na At-Tirmidhiy, katika Kitabu cha Tafsiyr ya Qur-aan, mlango na katika Suwrah Yuwnus.
[23]Ni Tafsiyr yenye kutegemea yaliyo sahihi katika yaliyopokelewa kulingana na mpangilio huu; Tafsiyr ya Qur-aan kwa Qur-aan; Tafsiyr ya Qur-aan kwa Sunnah, Tafsiyr ya Qur-aan kwa kauli za Maswahaba (رضي الله عنهم), Tafsiyr ya Qur-aan kwa kauli za Taabi’iyn kwa kuwa wao walichukua tafsiyr zao kutokana na Maswahaba (رضي الله عنهم). Vitabu vinavyotajika katika fani hii ya Tafsiyr ni kama:
i. Jaami’ul Bayaan Fiy Tafsiyril Qur-aan ya Ibn Jariyr Atw-Twabariy.
ii. Tafsiyrul Qur-aanil ‘Adhwiym ya Ibn Kathiyr.
iii. Fat-hul Qadiyr ya Ash-Shawkaaniy.
[24]Utangulizi wa Tafsiyr Ibn Kathiyr; vyanzo vya Tafsiyr.
[25][An-Nahl 16: 44]. Kadhalika Kauli Yake Allaah (سبحانه وتعالى):
ثُمَّ إِنَّ عَلَيْنَا بَيَانَهُ ﴿١٩
“Kisha ni juu Yetu kuibainisha (kwako).” [Al-Qiyaamah 75:19] inawarudi kwa uwazi kabisa wale wenye kudai kuwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلمhakubainisha maana ya Majina na Sifa za Allaah, na kwa kauli yao hii; ima wanakusudia kuwa: Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alikuwa hajui maana ya Majina na Sifa za Allaah; au ima Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) alificha kile alichokifahamu. Taz. Sharh Kitaab Muqaddimah fiy Uswuwl At-Tafsiyr.
[26]Amesema Abuu ‘Abdir-Rahmaan As-Sulamy: “Wametuhadithia wale waliokuwa wakitusomesha Qur-aan kama ‘Uthmaan bin ‘Affaan (رضي الله عنه) na ‘Abdullaah bin Mas’uwd (رضي الله عنه) na wengineo kuwa wao walikuwa pale wanapojifunza kutoka kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلمAayah kumi huwa hawaongezi nyingine mpaka pale watakapojifunza (na kutekeleza) yale yaliyomo ya elimu na ‘amali katika hizo Aayah kumi walizojifunza, basi wakasema: Tulijifunza Qur-aan na elimu na ‘amali kwa pamoja, na kwa sababu hiyo ndio walikuwa wakichukua muda kati kuhifadhi Suwrah.” Taz. Sharh Kitaab Muqaddimah fiy Uswuwl At-Tafsiyr.
[27]Aliyepokelewa akisema: “Naapa kwa Yule Ambaye hakuna Muabudiwa wa haki isipokuwa Yeye, hakuna katika Kitabu cha Allaah Suwrah isipokuwa mimi najua ilivyoteremka, na hakuna Aayah isipokuwa najua imeteremshwa kwa ajili gani (sababu) na lau ningelimjua yeyote kuwa yeye ni mjuzi zaidi yangu kwa Kitabu cha Allaah, na ngamia anaweza kufika, basi ningepanda kwenda kwake.” [Imepokelewa na Muslim, katika Kitabu cha Fadhila za Maswahaba, mlango wa fadhila za ‘Abdullaah bin Mas’uwd na mama yake (رضي الله عنهما)].
[28]Ibn ‘Abbaas aliyetambulikana kama ni ‘Tur-jumanil Qur-aan’ na aliyeombewa na Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) kama ilivyothibiti kwa kusema:
((اللَّهُمَّ عَلِّمْهُ الْحِكْمَةَ وَتَأْوِيلَ الْكِتَابِ))
“Ee Allaah, Mfunze Hikmah na Ta-awiyl (ufasiri, utambuzi) wa Kitabu (Qur-aan).” [Imepokelewa na At-Tirmidhiyy, katika Kitabu cha Ad-Da’waat, milango ya Manaaqiyb; na Sunan Ibn Maajah, katika Kitabu cha Ibn Maajah, milango ya fadhila za Maswahaba wa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم)].
[29]Ni kila kilichotegemezwa kwa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلمkatika kauli au kitendo au kuthibitisha jambo au sifa katika tabia zake au umbo lake.
[30]An-Nisaa (4: 43).
[31]Tafsiyr Ibn Kathiyr.
[32]Luqmaan (31: 6).
[33]Atw-Twabariy (20: 127).
[34]Al-Baqarah (2: 158).
[35]Al-Baqarah (2: 158).
[36]Al-Bukhaariy, katika Kitabu cha Tafsiyr ya Qur-aan, Suwrat Al-Baqarah, mlango wa aliyekuwa adui wa Jibriyl.
[37]Tazama Ibn Taymiyyah, Sharh Kitaab Muqaddimah fiy Uswuwl at-Tafsiyr.
[38]Kama vile Mujaahid, Sa’iyd bin Jubayr, ‘Ikrimah, Twaawuws, ‘Atwaa, Zayd bin Aslam, Abul ‘Aaliyah na Muhammad bin Ka’b, ‘Alqamah bin Qays, Masruwq, ‘Aamir Ash-Sha’biy na Hasan Al-Baswriy na Qataadah.
[39]Imaam At-Tirmidhiy amesema: “Ama yale yaliyopokelewa kutokana na Mujaahid na Qataadah na wengineo miongoni mwa Ahlul-‘Ilmi kwamba walifasiri Qur-aan,  basi hakuna haja ya kuwadhania kuwa walifasiri Qur-aan bila ya elimu –kwa rai zao- au kutokana na nafsi zao, na kumekwishapokewa kutokana na wao yale tuliyoyasema yenye kuthibitisha kwamba wao hawakuifasiri Qur-aan kutokana na nafsi zao bila ya elimu; kama ilivyothibiti kutokana na Al-Hassan bin Al-Mahdiy Al-Baswriyy amesema: Ametupa habari ‘Abdur-Razzaaq kutokana na Ma’mar kutoka kwa Qataadah kuwa amesema: “Katika Qur-aan hakuna Aayah yoyote ile isipokuwa nimesikia kitu kuhusiana nayo.” [At-Tirmidhiyy katika Kitabu cha Tafsiyr ya Qur-aan, mlango wa katika yale yaliyokuja kwa yule anayefasiri Qur-aan kwa rai yake]
[40]Kutoka kwa Ibn Mas’uwd(رضي الله عنه)  amesema kwamba Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم) amesema:
((خَيْرُ النَّاسِ قَرْنِي، ثُمَّ الَّذِينَ يَلُونَهُمْ، ثُمَّ الَّذِينَ يَلُونَهُمْ)) صحيح البخاري ومسلم
“Watu bora kabisa ni karne yangu, kisha wanaowafuatia, kisha wanaowafuatia.” [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, katika Kitabu Al-Manaaqib, mlango wa Fadhila za Maswahaba wa Rasuli wa Allaah (صلى الله عليه وآله وسلم); na Muslim Kitabu cha Fadhila za Maswahaba, mlango wa Fadhila za Maswahaba (رضي الله عنهم)].
[41]Al-Baqarah (2: 116).
[42]Tafsiyr Ibn Kathiyr.
[43]Al-Baqarah (2: 258).
[44]Tafsiyr Ibn Kathiyr.
[45]Tazama Ibn Taymiyyah, Sharh Kitaab Muqaddimah fiy Uswuwl At-Tafsiyr.
[46]Kukanusha maana.
[47]Mithilisha; linganisha, kufananisha.
[48]Kuainisha maana na kuziulizia namna yake au kuuliza ni vipi Sifa hiyo ipo kuchunguza ni kwa namna “gani” zimefungamana au kuambatana na Allaah.
[49]Kubadilisha maana, kupotosha Sifa ya Allaah kwa kutoa maana isiyo sahihi.
[50]Allaah (سبحانه وتعالى) Anasema:
لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ ﴿١١﴾
“Hakuna chochote kinachofanana Naye, Naye Ndiye Mwenye kusikia yote daima, Mwenye kuona yote daima.“ [Ash-Shuwraa 42: 11].