يس
Yaasiyn: 36


بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ


يس ﴿١﴾
1. Yaa Siyn.


وَالْقُرْآنِ الْحَكِيمِ ﴿٢﴾
2. Naapa kwa Qur-aan yenye hikmah.


إِنَّكَ لَمِنَ الْمُرْسَلِينَ ﴿٣﴾
3. Hakika wewe (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) bila shaka ni miongoni mwa Rusuli.


عَلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ ﴿٤﴾
4. Uko juu ya njia iliyonyooka.


تَنزِيلَ الْعَزِيزِ الرَّحِيمِ ﴿٥﴾
5. Ni uteremsho wa Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika, Mwenye kurehemu.


لِتُنذِرَ قَوْمًا مَّا أُنذِرَ آبَاؤُهُمْ فَهُمْ غَافِلُونَ ﴿٦﴾
6. Ili uwaonye watu ambao baba zao hawakuonywa, basi wao ni wenye kughafilika.



لَقَدْ حَقَّ الْقَوْلُ عَلَىٰ أَكْثَرِهِمْ فَهُمْ لَا يُؤْمِنُونَ ﴿٧﴾
7. Kwa yakini imethibiti kauli (ya adhabu) juu ya wengi wao, kwa hiyo hawaamini.



إِنَّا جَعَلْنَا فِي أَعْنَاقِهِمْ أَغْلَالًا فَهِيَ إِلَى الْأَذْقَانِ فَهُم مُّقْمَحُونَ ﴿٨﴾
8. Hakika Sisi Tumeweka kwenye shingo zao minyororo, ikawafika videvuni basi vichwa vyao vinanyanyuka juu na kufumba macho. 



وَجَعَلْنَا مِن بَيْنِ أَيْدِيهِمْ سَدًّا وَمِنْ خَلْفِهِمْ سَدًّا فَأَغْشَيْنَاهُمْ فَهُمْ لَا يُبْصِرُونَ ﴿٩﴾
9. Na Tumeweka mbele yao kizuizi na nyuma yao kizuizi, Tukawafunika, basi wao hawaoni.


وَسَوَاءٌ عَلَيْهِمْ أَأَنذَرْتَهُمْ أَمْ لَمْ تُنذِرْهُمْ لَا يُؤْمِنُونَ ﴿١٠﴾
10. Na ni sawasawa tu juu yao, ukiwaonya au usiwaonye hawaamini.



إِنَّمَا تُنذِرُ مَنِ اتَّبَعَ الذِّكْرَ وَخَشِيَ الرَّحْمَـٰنَ بِالْغَيْبِ ۖ فَبَشِّرْهُ بِمَغْفِرَةٍ وَأَجْرٍ كَرِيمٍ ﴿١١﴾
11. Hakika wewe (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) unamuonya yule anayefuata Ukumbusho na akamkhofu Ar-Rahmaan kwa ghayb, basi mbashirie kwa maghfirah na ujira karimu.


إِنَّا نَحْنُ نُحْيِي الْمَوْتَىٰ وَنَكْتُبُ مَا قَدَّمُوا وَآثَارَهُمْ ۚ وَكُلَّ شَيْءٍ أَحْصَيْنَاهُ فِي إِمَامٍ مُّبِينٍ ﴿١٢﴾
12. Hakika Sisi Tunahuisha wafu, na Tunaandika yale waliyoyakadimisha na athari zao na kila kitu Tumekirekodi barabara katika daftari bayana.


وَاضْرِبْ لَهُم مَّثَلًا أَصْحَابَ الْقَرْيَةِ إِذْ جَاءَهَا الْمُرْسَلُونَ ﴿١٣﴾
13. Na wapigie mfano watu wa mji walipowajia Rusuli.


إِذْ أَرْسَلْنَا إِلَيْهِمُ اثْنَيْنِ فَكَذَّبُوهُمَا فَعَزَّزْنَا بِثَالِثٍ فَقَالُوا إِنَّا إِلَيْكُم مُّرْسَلُونَ ﴿١٤﴾
14. Tulipowapelekea wawili, wakawakadhibisha, Tukawaongezea nguvu kwa wa tatu; wakasema: “Hakika sisi (ni Rusuli) tumetumwa kwenu”.


قَالُوا مَا أَنتُمْ إِلَّا بَشَرٌ مِّثْلُنَا وَمَا أَنزَلَ الرَّحْمَـٰنُ مِن شَيْءٍ إِنْ أَنتُمْ إِلَّا تَكْذِبُونَ ﴿١٥﴾
15. (Watu wa mji) Wakasema: “Nyinyi si chochote isipokuwa ni watu kama sisi, na wala Ar-Rahmaan Hakuteremsha chochote; hamkuwa nyinyi isipokuwa mnaongopa tu.”


قَالُوا رَبُّنَا يَعْلَمُ إِنَّا إِلَيْكُمْ لَمُرْسَلُونَ ﴿١٦﴾
16. (Rusuli) Wakasema: “Rabb wetu Anajua kwamba sisi bila shaka tumetumwa kwenu.”


وَمَا عَلَيْنَا إِلَّا الْبَلَاغُ الْمُبِينُ ﴿١٧﴾
17. “Na si juu yetu lolote isipokuwa ubalighisho wa bayana.”


قَالُوا إِنَّا تَطَيَّرْنَا بِكُمْ ۖ لَئِن لَّمْ تَنتَهُوا لَنَرْجُمَنَّكُمْ وَلَيَمَسَّنَّكُم مِّنَّا عَذَابٌ أَلِيمٌ ﴿١٨﴾
18. (Watu wa mji) Wakasema: “Hakika sisi tumepata nuksi kwenu; msipokoma hakika tutakurajimuni, na bila shaka itakuguseni kutoka kwetu adhabu iumizayo.”



قَالُوا طَائِرُكُم مَّعَكُمْ ۚ أَئِن ذُكِّرْتُم ۚ بَلْ أَنتُمْ قَوْمٌ مُّسْرِفُونَ ﴿١٩﴾
19. (Rusuli) Wakasema: “Nuksi yenu mnayo wenyewe. Je, kwa vile mnakumbushwa? Bali nyinyi ni watu wapindukao mipaka.”


وَجَاءَ مِنْ أَقْصَى الْمَدِينَةِ رَجُلٌ يَسْعَىٰ قَالَ يَا قَوْمِ اتَّبِعُوا الْمُرْسَلِينَ ﴿٢٠﴾
20. Akaja mtu kutoka upande wa mbali wa ule mji akiwa anakimbia; akasema: “Enyi watu wangu! Wafuateni Rusuli.”


اتَّبِعُوا مَن لَّا يَسْأَلُكُمْ أَجْرًا وَهُم مُّهْتَدُونَ ﴿٢١﴾
21. “Fuateni wale wasiokuombeni ujira, nao ni wenye kuongoka.”


وَمَا لِيَ لَا أَعْبُدُ الَّذِي فَطَرَنِي وَإِلَيْهِ تُرْجَعُونَ ﴿٢٢﴾
22. “Na kwa nini mimi nisimwabudu Ambaye Ameniumba na Kwake mtarejeshwa?”



أَأَتَّخِذُ مِن دُونِهِ آلِهَةً إِن يُرِدْنِ الرَّحْمَـٰنُ بِضُرٍّ لَّا تُغْنِ عَنِّي شَفَاعَتُهُمْ شَيْئًا وَلَا يُنقِذُونِ ﴿٢٣﴾
23. “Je, nijichukulie badala Yake waabudiwa, na hali Akinitakia Ar-Rahmaan dhara yoyote haitonifaa chochote uombezi wao na wala hawatoniokoa.”


إِنِّي إِذًا لَّفِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ ﴿٢٤﴾
24. “Hakika hapo nitakuwa katika upotofu bayana.”


إِنِّي آمَنتُ بِرَبِّكُمْ فَاسْمَعُونِ ﴿٢٥﴾
25. “Hakika mimi nimemwamini Rabb wenu, basi nisikilizeni!”


قِيلَ ادْخُلِ الْجَنَّةَ ۖ قَالَ يَا لَيْتَ قَوْمِي يَعْلَمُونَ ﴿٢٦﴾
26.  Ikasemwa (alipouliwa): “Ingia Jannah.” Akasema: “Laiti watu wangu wangelijua.


بِمَا غَفَرَ لِي رَبِّي وَجَعَلَنِي مِنَ الْمُكْرَمِينَ ﴿٢٧﴾
27. “Kwa yale Aliyonighufuria Rabb wangu, na Akanijaalia kuwa miongoni mwa waliokirimiwa.”


وَمَا أَنزَلْنَا عَلَىٰ قَوْمِهِ مِن بَعْدِهِ مِن جُندٍ مِّنَ السَّمَاءِ وَمَا كُنَّا مُنزِلِينَ ﴿٢٨﴾
28. Na Hatukuwateremshia watu wake baada yake jeshi lolote kutoka mbinguni na wala Hatukuwa wateremshao.


إِن كَانَتْ إِلَّا صَيْحَةً وَاحِدَةً فَإِذَا هُمْ خَامِدُونَ ﴿٢٩﴾
29. Haikuwa isipokuwa ukelele angamizi mmoja tu, basi mara hao wenye kuzimika.


يَا حَسْرَةً عَلَى الْعِبَادِ ۚ مَا يَأْتِيهِم مِّن رَّسُولٍ إِلَّا كَانُوا بِهِ يَسْتَهْزِئُونَ ﴿٣٠﴾
30. Ee! Ole na majuto juu ya waja!  Hawafikiwi na Rasuli yeyote isipokuwa walikuwa wakimfanyia istihzai.


أَلَمْ يَرَوْا كَمْ أَهْلَكْنَا قَبْلَهُم مِّنَ الْقُرُونِ أَنَّهُمْ إِلَيْهِمْ لَا يَرْجِعُونَ ﴿٣١﴾
31. Je, hawajaona karne ngapi Tumeangamiza kabla yao na kwamba wao hawatorejea kwao?


وَإِن كُلٌّ لَّمَّا جَمِيعٌ لَّدَيْنَا مُحْضَرُونَ ﴿٣٢﴾
32. Na hapana yeyote ila wote watahudhurishwa Kwetu. 



وَآيَةٌ لَّهُمُ الْأَرْضُ الْمَيْتَةُ أَحْيَيْنَاهَا وَأَخْرَجْنَا مِنْهَا حَبًّا فَمِنْهُ يَأْكُلُونَ ﴿٣٣﴾
33. Na Aayah (ishara, dalili) kwao ni ardhi iliyokufa, Tukaihuisha, na Tukatoa humo nafaka, basi kutoka kwayo wanakula.


وَجَعَلْنَا فِيهَا جَنَّاتٍ مِّن نَّخِيلٍ وَأَعْنَابٍ وَفَجَّرْنَا فِيهَا مِنَ الْعُيُونِ ﴿٣٤﴾
34. Na Tukafanya humo mabustani ya mitende, na mizabibu, na Tukabubujua humo chemchemu.


لِيَأْكُلُوا مِن ثَمَرِهِ وَمَا عَمِلَتْهُ أَيْدِيهِمْ ۖ أَفَلَا يَشْكُرُونَ ﴿٣٥﴾
35. Ili wale katika matunda yake, na haikuyafanya hayo mikono yao, je basi hawashukuru?



سُبْحَانَ الَّذِي خَلَقَ الْأَزْوَاجَ كُلَّهَا مِمَّا تُنبِتُ الْأَرْضُ وَمِنْ أَنفُسِهِمْ وَمِمَّا لَا يَعْلَمُونَ ﴿٣٦﴾
36. Subhaanah! Utakasifu ni wa Ambaye Ameumba dume na jike vyote katika ambavyo inaotesha ardhi na katika nafsi zao na katika vile wasivyovijua.


وَآيَةٌ لَّهُمُ اللَّيْلُ نَسْلَخُ مِنْهُ النَّهَارَ فَإِذَا هُم مُّظْلِمُونَ ﴿٣٧﴾
37. Na Aayah (ishara, dalili) kwao ni usiku, Tunauvua humo mchana, basi tahamaki wao ni wenye kuwa kizani.


وَالشَّمْسُ تَجْرِي لِمُسْتَقَرٍّ لَّهَا ۚ ذَٰلِكَ تَقْدِيرُ الْعَزِيزِ الْعَلِيمِ ﴿٣٨﴾
38. Na jua linatembea hadi matulio yake. Hiyo ni takdiri ya Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika, Mjuzi wa yote.

وَالْقَمَرَ قَدَّرْنَاهُ مَنَازِلَ حَتَّىٰ عَادَ كَالْعُرْجُونِ الْقَدِيمِ ﴿٣٩﴾
39. Na mwezi Tumeukadiria vituo mpaka ukarudi (mwembamba) kama kwamba karara la shina la mtende lililopinda la zamani.


لَا الشَّمْسُ يَنبَغِي لَهَا أَن تُدْرِكَ الْقَمَرَ وَلَا اللَّيْلُ سَابِقُ النَّهَارِ ۚ وَكُلٌّ فِي فَلَكٍ يَسْبَحُونَ ﴿٤٠﴾
40. Halipasi jua kuudiriki mwezi, na wala usiku kuutangulia mchana; na kila kimoja viko katika falaki vinaogelea.


وَآيَةٌ لَّهُمْ أَنَّا حَمَلْنَا ذُرِّيَّتَهُمْ فِي الْفُلْكِ الْمَشْحُونِ ﴿٤١﴾
41. Na Aayah (ishara, dalili) kwao, kwamba Sisi Tumebeba vizazi vyao katika merikebu iliyosheheni.


وَخَلَقْنَا لَهُم مِّن مِّثْلِهِ مَا يَرْكَبُونَ ﴿٤٢﴾
42. Na Tukawaumbia kutoka mfano wake wa vile wanavyovipanda.


وَإِن نَّشَأْ نُغْرِقْهُمْ فَلَا صَرِيخَ لَهُمْ وَلَا هُمْ يُنقَذُونَ ﴿٤٣﴾
43. Na kama Tungetaka, Tungeliwagharikisha, basi hakuna wa kupiga kelele kuwasaidia na wala hawatookolewa.


إِلَّا رَحْمَةً مِّنَّا وَمَتَاعًا إِلَىٰ حِينٍ ﴿٤٤﴾
44. Isipokuwa rahmah kutoka Kwetu, na starehe kwa muda tu.



وَإِذَا قِيلَ لَهُمُ اتَّقُوا مَا بَيْنَ أَيْدِيكُمْ وَمَا خَلْفَكُمْ لَعَلَّكُمْ تُرْحَمُونَ ﴿٤٥﴾
45. Na wanapoambiwa: “Ogopeni yale yaliyo mbele yenu na yale yaliyo nyuma yenu ili mpate kurehemewa.”


وَمَا تَأْتِيهِم مِّنْ آيَةٍ مِّنْ آيَاتِ رَبِّهِمْ إِلَّا كَانُوا عَنْهَا مُعْرِضِينَ ﴿٤٦﴾
46. Na haiwafikii Aayah (na ishara) yoyote katika Aayaat za Rabb wao, isipokuwa walikuwa ni wenye kuzikengeuka.



وَإِذَا قِيلَ لَهُمْ أَنفِقُوا مِمَّا رَزَقَكُمُ اللَّـهُ قَالَ الَّذِينَ كَفَرُوا لِلَّذِينَ آمَنُوا أَنُطْعِمُ مَن لَّوْ يَشَاءُ اللَّـهُ أَطْعَمَهُ إِنْ أَنتُمْ إِلَّا فِي ضَلَالٍ مُّبِينٍ ﴿٤٧﴾
47. Na wanapoambiwa: “Toeni kutokana na vile Alivyokuruzukuni Allaah.” Husema wale waliokufuru kuwaambia wale walioamni: “Je, tumlishe ambaye (Allaah) Angelitaka Angelimlisha? Nyinyi hamumo isipokuwa katika upotofu bayana.”


وَيَقُولُونَ مَتَىٰ هَـٰذَا الْوَعْدُ إِن كُنتُمْ صَادِقِينَ ﴿٤٨﴾
48. Na wanasema: “Ni lini hiyo ahadi (ya kufufuliwa) mkiwa ni wasemao kweli?”


مَا يَنظُرُونَ إِلَّا صَيْحَةً وَاحِدَةً تَأْخُذُهُمْ وَهُمْ يَخِصِّمُونَ ﴿٤٩﴾
49. Hawangojei isipokuwa ukelele mmoja tu, uwachukue hali wao wanakhasimiana.


فَلَا يَسْتَطِيعُونَ تَوْصِيَةً وَلَا إِلَىٰ أَهْلِهِمْ يَرْجِعُونَ ﴿٥٠﴾
50. Basi hawatoweza kuusia, na wala kurejea kwa ahli zao.


وَنُفِخَ فِي الصُّورِ فَإِذَا هُم مِّنَ الْأَجْدَاثِ إِلَىٰ رَبِّهِمْ يَنسِلُونَ ﴿٥١﴾
51. Na litapulizwa baragumu basi tahamaki wanatoka makaburini mwao wakienda mbio mbio kwa Rabb wao.


قَالُوا يَا وَيْلَنَا مَن بَعَثَنَا مِن مَّرْقَدِنَا ۜ ۗ هَـٰذَا مَا وَعَدَ الرَّحْمَـٰنُ وَصَدَقَ الْمُرْسَلُونَ ﴿٥٢﴾
52. Waseme: “Ole wetu! Nani ametufufua katika malazo yetu?” (Wataambiwa): “Haya ndio Aliyoahidi Ar-Rahmaan na Rusuli walisema kweli.”


إِن كَانَتْ إِلَّا صَيْحَةً وَاحِدَةً فَإِذَا هُمْ جَمِيعٌ لَّدَيْنَا مُحْضَرُونَ ﴿٥٣﴾
53. Haitokuwa isipokuwa ukelele mmoja tu, tahamaki wote watahudhurishwa mbele Yetu.


فَالْيَوْمَ لَا تُظْلَمُ نَفْسٌ شَيْئًا وَلَا تُجْزَوْنَ إِلَّا مَا كُنتُمْ تَعْمَلُونَ ﴿٥٤﴾
54. Basi leo nafsi yoyote haitodhulumiwa kitu chochote, na wala hamtalipwa isipokuwa yale mliyokuwa mkiyatenda.


إِنَّ أَصْحَابَ الْجَنَّةِ الْيَوْمَ فِي شُغُلٍ فَاكِهُونَ ﴿٥٥﴾
55. Hakika watu wa Jannah leo wamo katika kushughulika wakifurahi.


هُمْ وَأَزْوَاجُهُمْ فِي ظِلَالٍ عَلَى الْأَرَائِكِ مُتَّكِئُونَ ﴿٥٦﴾
56. Wao na wake zao, wakiwa katika vivuli, juu ya makochi ya fakhari wakiegemea.


لَهُمْ فِيهَا فَاكِهَةٌ وَلَهُم مَّا يَدَّعُونَ ﴿٥٧﴾
57. Watapata humo kila aina ya matunda, na watapata wanavyoomba.


سَلَامٌ قَوْلًا مِّن رَّبٍّ رَّحِيمٍ ﴿٥٨﴾
58. “Salaamun!” Kauli kutoka kwa Rabb Mwenye kurehemu.


وَامْتَازُوا الْيَوْمَ أَيُّهَا الْمُجْرِمُونَ ﴿٥٩﴾
59. (Itasemwa): “Na jitengeni enyi wahalifu.”


أَلَمْ أَعْهَدْ إِلَيْكُمْ يَا بَنِي آدَمَ أَن لَّا تَعْبُدُوا الشَّيْطَانَ ۖ إِنَّهُ لَكُمْ عَدُوٌّ مُّبِينٌ ﴿٦٠﴾
60. “Je, Sijakukuahidini enyi wana wa Aadam kwamba: “Msimwabudu shaytwaan, hakika yeye kweni ni adui bayana!”


وَأَنِ اعْبُدُونِي ۚ هَـٰذَا صِرَاطٌ مُّسْتَقِيمٌ ﴿٦١﴾
61. “Na kwamba Niabuduni Mimi? Hii ndio njia iliyonyooka.”


وَلَقَدْ أَضَلَّ مِنكُمْ جِبِلًّا كَثِيرًا ۖ أَفَلَمْ تَكُونُوا تَعْقِلُونَ ﴿٦٢﴾
62. “Na kwa yakini (shaytwaan) amekwishawapotoa viumbe wengi miongoni mwenu; je basi hamtokuwa wenye kutia akilini?”


هَـٰذِهِ جَهَنَّمُ الَّتِي كُنتُمْ تُوعَدُونَ ﴿٦٣﴾
63. “Huu hii ni Jahannam ambayo mlikuwa mkiahidiwa.”


اصْلَوْهَا الْيَوْمَ بِمَا كُنتُمْ تَكْفُرُونَ ﴿٦٤﴾
64. “Ingieni muungue leo kwa sababu ya yale mliyokuwa mkiyakufuru.”


الْيَوْمَ نَخْتِمُ عَلَىٰ أَفْوَاهِهِمْ وَتُكَلِّمُنَا أَيْدِيهِمْ وَتَشْهَدُ أَرْجُلُهُم بِمَا كَانُوا يَكْسِبُونَ ﴿٦٥﴾
65. Leo Tunatia vizibo juu ya vinywa vyao, na itatusemesha mikono yao, na itashuhudia miguu yao kwa yale waliyokuwa wakiyachuma.


وَلَوْ نَشَاءُ لَطَمَسْنَا عَلَىٰ أَعْيُنِهِمْ فَاسْتَبَقُوا الصِّرَاطَ فَأَنَّىٰ يُبْصِرُونَ ﴿٦٦﴾
66. Na lau Tungelitaka, Tungelipofoa macho yao, wakashindana mbio kuitafuta njia, lakini kutoka wapi wataona?


وَلَوْ نَشَاءُ لَمَسَخْنَاهُمْ عَلَىٰ مَكَانَتِهِمْ فَمَا اسْتَطَاعُوا مُضِيًّا وَلَا يَرْجِعُونَ ﴿٦٧﴾
67. Na lau Tungelitaka, Tungeliwaumbua tukawalemaza hapo mahali walipo, basi wasingeliweza kwenda mbele wala wasingerudi. 


وَمَن نُّعَمِّرْهُ نُنَكِّسْهُ فِي الْخَلْقِ ۖ أَفَلَا يَعْقِلُونَ ﴿٦٨﴾
68. Na yule Tunayempa umri, Tunamrejesha nyuma katika umbo (kumdhoofisha), je, basi hamtii akilini?


وَمَا عَلَّمْنَاهُ الشِّعْرَ وَمَا يَنبَغِي لَهُ ۚ إِنْ هُوَ إِلَّا ذِكْرٌ وَقُرْآنٌ مُّبِينٌ ﴿٦٩﴾
69. Na hatukumfunza (Nabiy Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) mashairi, na wala haipasi kwake, hii si chochote isipokuwa ni ukumbusho na Qur-aan bayana.


لِّيُنذِرَ مَن كَانَ حَيًّا وَيَحِقَّ الْقَوْلُ عَلَى الْكَافِرِينَ ﴿٧٠﴾
70. Ili imuonye yule aliyekuwa hai na neno lihakikike juu ya makafiri.


أَوَلَمْ يَرَوْا أَنَّا خَلَقْنَا لَهُم مِّمَّا عَمِلَتْ أَيْدِينَا أَنْعَامًا فَهُمْ لَهَا مَالِكُونَ ﴿٧١﴾
71. Je, hawaoni kwamba Sisi Tumewaumbia kutokana na yale iliyofanya Mikono Yetu; wanyama wa mifugo basi wao wanawamiliki?


وَذَلَّلْنَاهَا لَهُمْ فَمِنْهَا رَكُوبُهُمْ وَمِنْهَا يَأْكُلُونَ ﴿٧٢﴾
72. Na Tumewadhalilisha kwao, basi miongoni mwao ni vipando vyao na miongoni mwao wanawala?


وَلَهُمْ فِيهَا مَنَافِعُ وَمَشَارِبُ ۖ أَفَلَا يَشْكُرُونَ ﴿٧٣﴾
73. Na wanapata humo manufaa na vinywaji je, basi hawashukuru?


وَاتَّخَذُوا مِن دُونِ اللَّـهِ آلِهَةً لَّعَلَّهُمْ يُنصَرُونَ ﴿٧٤﴾
74. Na wamejichukulia badala ya Allaah waabudiwa ili wakitumaini kuwa watawanusuru!


لَا يَسْتَطِيعُونَ نَصْرَهُمْ وَهُمْ لَهُمْ جُندٌ مُّحْضَرُونَ ﴿٧٥﴾
75. Hawawezi kuwanusuru, na watahudhurishwa (adhabuni) kama askari dhidi ya hao (waliowaabudu).


فَلَا يَحْزُنكَ قَوْلُهُمْ ۘ إِنَّا نَعْلَمُ مَا يُسِرُّونَ وَمَا يُعْلِنُونَ ﴿٧٦﴾
76. Basi isikuhuzunishe kauli yao (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم), hakika Sisi Tunajua yale wanayoyaficha na yale wanayoyatangaza.


أَوَلَمْ يَرَ الْإِنسَانُ أَنَّا خَلَقْنَاهُ مِن نُّطْفَةٍ فَإِذَا هُوَ خَصِيمٌ مُّبِينٌ ﴿٧٧﴾
77. Je, insani haoni kwamba Sisi Tumemuumba kutokana na tone la manii, mara yeye ni hasimu wa bayana?


وَضَرَبَ لَنَا مَثَلًا وَنَسِيَ خَلْقَهُ ۖ قَالَ مَن يُحْيِي الْعِظَامَ وَهِيَ رَمِيمٌ ﴿٧٨﴾
78. Na akatupigia mfano, akasahau kuumbwa kwake; akasema: “Ni nani atakayehuisha mifupa hii na hali imeshaoza na kusagika na kuwa kama vumbi.”


قُلْ يُحْيِيهَا الَّذِي أَنشَأَهَا أَوَّلَ مَرَّةٍ ۖ وَهُوَ بِكُلِّ خَلْقٍ عَلِيمٌ ﴿٧٩﴾
79. Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): “Ataihuisha Yule Aliyeianzisha mara ya kwanza; Naye ni Mjuzi wa kila kiumbe.


الَّذِي جَعَلَ لَكُم مِّنَ الشَّجَرِ الْأَخْضَرِ نَارًا فَإِذَا أَنتُم مِّنْهُ تُوقِدُونَ ﴿٨٠﴾
80. Ambaye Amekujaalieni moto kutokana na miti ya kijani, kisha nyinyi mnauwasha.



أَوَلَيْسَ الَّذِي خَلَقَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ بِقَادِرٍ عَلَىٰ أَن يَخْلُقَ مِثْلَهُم ۚ بَلَىٰ وَهُوَ الْخَلَّاقُ الْعَلِيمُ ﴿٨١﴾
81. Je, kwani Yule Aliyeumba mbingu na ardhi (mnadhani) Hana uwezo wa kuumba mfano wao? Naam bila shaka (Anaweza)! Naye ni Mwingi wa kuumba Atakavyo, Mjuzi wa yote.


إِنَّمَا أَمْرُهُ إِذَا أَرَادَ شَيْئًا أَن يَقُولَ لَهُ كُن فَيَكُونُ ﴿٨٢﴾
82. Hakika amri Yake Anapotaka chochote hukiambia: “Kun! (Kuwa), nacho huwa.”


فَسُبْحَانَ الَّذِي بِيَدِهِ مَلَكُوتُ كُلِّ شَيْءٍ وَإِلَيْهِ تُرْجَعُونَ ﴿٨٣﴾
83. Basi Subhaanah! Utakasifu ni wa Ambaye Mkononi Mwake kuna ufalme wa kila kitu, na Kwake mtarejeshwa.