الْمُؤمِنُون
Al-Muuminuwn: 23



بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ



قَدْ أَفْلَحَ الْمُؤْمِنُونَ ﴿١﴾
1. Kwa yakini wamefaulu Waumini.


الَّذِينَ هُمْ فِي صَلَاتِهِمْ خَاشِعُونَ ﴿٢﴾
2. Ambao katika Swalaah zao huwa wananyenyekea.


وَالَّذِينَ هُمْ عَنِ اللَّغْوِ مُعْرِضُونَ ﴿٣﴾
3. Na ambao wanajiepusha na mambo ya upuuzi.


وَالَّذِينَ هُمْ لِلزَّكَاةِ فَاعِلُونَ ﴿٤﴾
4. Na ambao wanatoa Zakaah.


وَالَّذِينَ هُمْ لِفُرُوجِهِمْ حَافِظُونَ ﴿٥﴾
5. Na ambao wanazihifadhi tupu zao.


إِلَّا عَلَىٰ أَزْوَاجِهِمْ أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُمْ فَإِنَّهُمْ غَيْرُ مَلُومِينَ ﴿٦﴾
6. Isipokuwa kwa wake zao, au kwa iliyowamiliki mikono yao ya kuume basi hao hawalaumiwi.


فَمَنِ ابْتَغَىٰ وَرَاءَ ذَٰلِكَ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْعَادُونَ ﴿٧﴾
7. Lakini atakayetaka kinyume ya hayo; basi hao ndio wapindukao mipaka.


وَالَّذِينَ هُمْ لِأَمَانَاتِهِمْ وَعَهْدِهِمْ رَاعُونَ ﴿٨﴾
8. Na ambao amana zao na ahadi zao wanazichunga.


وَالَّذِينَ هُمْ عَلَىٰ صَلَوَاتِهِمْ يُحَافِظُونَ ﴿٩﴾
9. Na ambao wanazihifadhi Swalaah zao.


أُولَـٰئِكَ هُمُ الْوَارِثُونَ ﴿١٠﴾
10. Hao ndio warithi.


الَّذِينَ يَرِثُونَ الْفِرْدَوْسَ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ ﴿١١﴾
11. Ambao watarithi (Jannah) ya Al-Firdaws, wao humo ni wenye kudumu.


وَلَقَدْ خَلَقْنَا الْإِنسَانَ مِن سُلَالَةٍ مِّن طِينٍ ﴿١٢﴾
12. Kwa yakini Tumemuumba insani kutokana na mchujo safi wa udongo.


ثُمَّ جَعَلْنَاهُ نُطْفَةً فِي قَرَارٍ مَّكِينٍ ﴿١٣﴾
13. Kisha Tukamjaalia kuwa tone la manii katika kalio makini.


ثُمَّ خَلَقْنَا النُّطْفَةَ عَلَقَةً فَخَلَقْنَا الْعَلَقَةَ مُضْغَةً فَخَلَقْنَا الْمُضْغَةَ عِظَامًا فَكَسَوْنَا الْعِظَامَ لَحْمًا ثُمَّ أَنشَأْنَاهُ خَلْقًا آخَرَ ۚ فَتَبَارَكَ اللَّـهُ أَحْسَنُ الْخَالِقِينَ ﴿١٤﴾
14. Kisha Tukaumba tone la manii kuwa pande la damu linaloning’inia, Tukaumba pande la damu hilo linaloning’inia kuwa kinofu cha nyama, Tukaumba kinofu cha nyama hiyo kuwa mifupa, Tukavisha mifupa hiyo nyama, kisha Tukamuanzisha kiumbe kingine. Basi Tabaaraka-Allaah, Amebarikika Allaah Mbora wa wenye kuumba.


ثُمَّ إِنَّكُم بَعْدَ ذَٰلِكَ لَمَيِّتُونَ ﴿١٥﴾
15. Kisha nyinyi baada ya hayo, ni wenye kufa.


ثُمَّ إِنَّكُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ تُبْعَثُونَ ﴿١٦﴾
16. Kisha hakika nyinyi Siku ya Qiyaamah mtafufuliwa.


وَلَقَدْ خَلَقْنَا فَوْقَكُمْ سَبْعَ طَرَائِقَ وَمَا كُنَّا عَنِ الْخَلْقِ غَافِلِينَ ﴿١٧﴾
17. Kwa yakini Tumeumba juu yenu tabaka za mbingu saba; na Hatukuwa wenye kughafilika kuhusu viumbe.


وَأَنزَلْنَا مِنَ السَّمَاءِ مَاءً بِقَدَرٍ فَأَسْكَنَّاهُ فِي الْأَرْضِ ۖ وَإِنَّا عَلَىٰ ذَهَابٍ بِهِ لَقَادِرُونَ ﴿١٨﴾
18. Na Tukateremsha kutoka mbinguni maji kwa kiasi, na Tukayawekea maskani ardhini. Nasi kwa kuyaondosha bila shaka ni Wenye uwezo.


فَأَنشَأْنَا لَكُم بِهِ جَنَّاتٍ مِّن نَّخِيلٍ وَأَعْنَابٍ لَّكُمْ فِيهَا فَوَاكِهُ كَثِيرَةٌ وَمِنْهَا تَأْكُلُونَ ﴿١٩﴾
19. Kisha (kwa maji) hayo Tukaanzisha mabustani ya mitende na mizabibu mnapata humo matunda mengi, na katika hayo mnakula.


وَشَجَرَةً تَخْرُجُ مِن طُورِ سَيْنَاءَ تَنبُتُ بِالدُّهْنِ وَصِبْغٍ لِّلْآكِلِينَ ﴿٢٠﴾
20. Na mti (wa zaituni) unaotoka katika mlima wa Sinai, unaomea kwa (kutoa) mafuta na kuwa kitoweo kwa walaji.


وَإِنَّ لَكُمْ فِي الْأَنْعَامِ لَعِبْرَةً ۖ نُّسْقِيكُم مِّمَّا فِي بُطُونِهَا وَلَكُمْ فِيهَا مَنَافِعُ كَثِيرَةٌ وَمِنْهَا تَأْكُلُونَ ﴿٢١﴾
21. Na hakika katika wanyama wa mifugo mnapata zingatio. Tunakunywisheni (maziwa) kutoka matumboni mwao, na mnapata humo manufaa mengi, na kati yao mnawala.


وَعَلَيْهَا وَعَلَى الْفُلْكِ تُحْمَلُونَ ﴿٢٢﴾
22. Na juu yao (hao wanyama), na juu ya merikebu mnabebwa.


وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا نُوحًا إِلَىٰ قَوْمِهِ فَقَالَ يَا قَوْمِ اعْبُدُوا اللَّـهَ مَا لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرُهُ ۖ أَفَلَا تَتَّقُونَ ﴿٢٣﴾
23. Kwa yakini Tulimpeleka Nuwh kwa kaumu yake, akasema: “Enyi kaumu yangu! Mwabuduni Allaah, hamna Muabudiwa wa haki ghairi Yake. Je, basi hamtokuwa na taqwa?” 


فَقَالَ الْمَلَأُ الَّذِينَ كَفَرُوا مِن قَوْمِهِ مَا هَـٰذَا إِلَّا بَشَرٌ مِّثْلُكُمْ يُرِيدُ أَن يَتَفَضَّلَ عَلَيْكُمْ وَلَوْ شَاءَ اللَّـهُ لَأَنزَلَ مَلَائِكَةً مَّا سَمِعْنَا بِهَـٰذَا فِي آبَائِنَا الْأَوَّلِينَ ﴿٢٤﴾
24. Wakasema wakuu waliokufuru miongoni mwa kaumu yake: “Huyu si chochote ila ni binaadamu kama nyinyi; anataka ajifadhilishe juu yenu. Na lau Allaah Angelitaka (kutuma Rasuli), bila shaka Angeliteremsha Malaika. Hatukusikia haya kwa baba zetu wa awali.”


إِنْ هُوَ إِلَّا رَجُلٌ بِهِ جِنَّةٌ فَتَرَبَّصُوا بِهِ حَتَّىٰ حِينٍ ﴿٢٥﴾
25. “Yeye si lolote ila ni mtu ana wazimu; basi mngojeeni na mwangalieni tu kwa muda.”


قَالَ رَبِّ انصُرْنِي بِمَا كَذَّبُونِ ﴿٢٦﴾
26. (Nuwh) Akasema: “Rabb wangu! Ninusuru kutokana na yale waliyonikadhibisha.”


فَأَوْحَيْنَا إِلَيْهِ أَنِ اصْنَعِ الْفُلْكَ بِأَعْيُنِنَا وَوَحْيِنَا فَإِذَا جَاءَ أَمْرُنَا وَفَارَ التَّنُّورُ ۙ فَاسْلُكْ فِيهَا مِن كُلٍّ زَوْجَيْنِ اثْنَيْنِ وَأَهْلَكَ إِلَّا مَن سَبَقَ عَلَيْهِ الْقَوْلُ مِنْهُمْ ۖ وَلَا تُخَاطِبْنِي فِي الَّذِينَ ظَلَمُوا ۖ إِنَّهُم مُّغْرَقُونَ﴿٢٧﴾
27. Basi Tukamfunulia Wahy kwamba: Unda jahazi mbele ya Macho Yetu na Wahy Wetu. Itakapokuja amri Yetu, na tanuri likafoka, basi waingize humo kila namna dume na jike na ahli zako isipokuwa yule miongoni mwao iliyekwishmtangulia kauli, na wala usinisemeshe kuhusu hao waliodhulumu; hakika wao wenye kugharikishwa.


فَإِذَا اسْتَوَيْتَ أَنتَ وَمَن مَّعَكَ عَلَى الْفُلْكِ فَقُلِ الْحَمْدُ لِلَّـهِ الَّذِي نَجَّانَا مِنَ الْقَوْمِ الظَّالِمِينَ ﴿٢٨﴾
28. Basi utakaposawazika wewe na wale walio pamoja nawe jahazini, sema: “AlhamduliLLaah, Himidi Anastahiki Allaah Ambaye Ametuokoa kutokana na watu madhalimu.”


وَقُل رَّبِّ أَنزِلْنِي مُنزَلًا مُّبَارَكًا وَأَنتَ خَيْرُ الْمُنزِلِينَ ﴿٢٩﴾
29. Na sema: “Rabb wangu! Niteremshe mteremko wa baraka, Nawe ni Mbora wa wenye kuteremsha.”

إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ وَإِن كُنَّا لَمُبْتَلِينَ ﴿٣٠﴾
30. Hakika katika hayo bila shaka ni Aayaat (ishara, zingatio, mawaidha n.k), na hakika Tumekuwa Wenye kuwafanyia mitihani.


ثُمَّ أَنشَأْنَا مِن بَعْدِهِمْ قَرْنًا آخَرِينَ ﴿٣١﴾
31. Kisha Tukaanzisha baada yao karne nyingine.


فَأَرْسَلْنَا فِيهِمْ رَسُولًا مِّنْهُمْ أَنِ اعْبُدُوا اللَّـهَ مَا لَكُم مِّنْ إِلَـٰهٍ غَيْرُهُ ۖ أَفَلَا تَتَّقُونَ ﴿٣٢﴾
32. Tukawapelekea Rasuli miongoni mwao (awalinganie) kwamba: “Mwabuduni Allaah, hamna Muabudiwa wa haki ghairi Yake. Je, basi hamtokuwa na taqwa?” 


وَقَالَ الْمَلَأُ مِن قَوْمِهِ الَّذِينَ كَفَرُوا وَكَذَّبُوا بِلِقَاءِ الْآخِرَةِ وَأَتْرَفْنَاهُمْ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا مَا هَـٰذَا إِلَّا بَشَرٌ مِّثْلُكُمْ يَأْكُلُ مِمَّا تَأْكُلُونَ مِنْهُ وَيَشْرَبُ مِمَّا تَشْرَبُونَ ﴿٣٣﴾
33. Na wakasema wakuu miongoni mwa kaumu yake waliokufuru na wakakadhibisha mkutano wa Aakhirah, na Tukawapa utajri kwa anasa na starehe katika uhai wa dunia: “Huyu si lolote ila ni binaadamu kama nyinyi; anakula katika yale mnayokula nyinyi, na anakunywa katika yale mnayokunywa.”


وَلَئِنْ أَطَعْتُم بَشَرًا مِّثْلَكُمْ إِنَّكُمْ إِذًا لَّخَاسِرُونَ ﴿٣٤﴾
34. “Na mkimtii binaadamu kama nyinyi; basi hapo hakika nyinyi mtakuwa wenye kukhasirika.


أَيَعِدُكُمْ أَنَّكُمْ إِذَا مِتُّمْ وَكُنتُمْ تُرَابًا وَعِظَامًا أَنَّكُم مُّخْرَجُونَ ﴿٣٥﴾
35. “Je, anakuahidini kwamba nyinyi mtakapokufa, mkawa mchanga na mifupa kuwa hakika mtatolewa (kuwa hai)?

هَيْهَاتَ هَيْهَاتَ لِمَا تُوعَدُونَ ﴿٣٦﴾
36. “Mbali kabisa, mbali kabisa! Hayo mnayoahidiwa.


إِنْ هِيَ إِلَّا حَيَاتُنَا الدُّنْيَا نَمُوتُ وَنَحْيَا وَمَا نَحْنُ بِمَبْعُوثِينَ ﴿٣٧﴾
37. “Hakuna lolote isipokuwa tu uhai wetu wa duniani; tunakufa na tunahuika, na wala sisi hatutofufuliwa.


إِنْ هُوَ إِلَّا رَجُلٌ افْتَرَىٰ عَلَى اللَّـهِ كَذِبًا وَمَا نَحْنُ لَهُ بِمُؤْمِنِينَ ﴿٣٨﴾
38. “Yeye si lolote isipokuwa mtu aliyemtungia Allaah uongo, nasi hatutomwamini.” 


قَالَ رَبِّ انصُرْنِي بِمَا كَذَّبُونِ ﴿٣٩﴾
39. (Rasuli huyo) Akasema: “Rabb wangu! Ninusuru kutokana na yale waliyonikadhibisha.”


قَالَ عَمَّا قَلِيلٍ لَّيُصْبِحُنَّ نَادِمِينَ ﴿٤٠﴾
40. (Allaah) Akasema: “Muda mchache tu, bila shaka watapambazukiwa wawe wenye kujuta.”


فَأَخَذَتْهُمُ الصَّيْحَةُ بِالْحَقِّ فَجَعَلْنَاهُمْ غُثَاءً ۚ فَبُعْدًا لِّلْقَوْمِ الظَّالِمِينَ ﴿٤١﴾
41. Basi ikawachukua ukelele angamizi kwa haki; Tukawafanya kama takataka za majani zinazoelea juu ya maji; basi wametokomelea mbali watu madhalimu.


ثُمَّ أَنشَأْنَا مِن بَعْدِهِمْ قُرُونًا آخَرِينَ ﴿٤٢﴾
42. Kisha Tukaanzisha baada yao karne nyingi nyinginezo. 


مَا تَسْبِقُ مِنْ أُمَّةٍ أَجَلَهَا وَمَا يَسْتَأْخِرُونَ ﴿٤٣﴾
43. Hapana ummah uwezao kutanguliza ajali yake, na wala hawawezi kuakhirisha.


ثُمَّ أَرْسَلْنَا رُسُلَنَا تَتْرَىٰ ۖ كُلَّ مَا جَاءَ أُمَّةً رَّسُولُهَا كَذَّبُوهُ ۚ فَأَتْبَعْنَا بَعْضَهُم بَعْضًا وَجَعَلْنَاهُمْ أَحَادِيثَ ۚفَبُعْدًا لِّقَوْمٍ لَّا يُؤْمِنُونَ ﴿٤٤﴾
44. Kisha Tukatuma Rusuli Wetu waliofuatana mfululizo. Kila ummah alipowajia Rasuli wao, walimkadhibisha. Basi Tukawafuatanisha baadhi yao kwa wao (kwa maangamizi). Na Tukawafanya ni hadithi za kusimuliwa. Basi wametokomelea mbali watu wasioamini.


ثُمَّ أَرْسَلْنَا مُوسَىٰ وَأَخَاهُ هَارُونَ بِآيَاتِنَا وَسُلْطَانٍ مُّبِينٍ ﴿٤٥﴾
45. Kisha Tukamtuma Muwsaa na kaka yake Haaruwn kwa Aayaat (ishara na dalili) Zetu na mamlaka bayana.


إِلَىٰ فِرْعَوْنَ وَمَلَئِهِ فَاسْتَكْبَرُوا وَكَانُوا قَوْمًا عَالِينَ ﴿٤٦﴾
46. Kwa Fir’awn, na wakuu wake; lakini walitakabari, na wakawa watu waliotakabari.


فَقَالُوا أَنُؤْمِنُ لِبَشَرَيْنِ مِثْلِنَا وَقَوْمُهُمَا لَنَا عَابِدُونَ ﴿٤٧﴾
47. Wakasema: “Je, tuwaamini binaadamu wawili kama sisi, na hali watu wao kwetu ni watumwa?”


فَكَذَّبُوهُمَا فَكَانُوا مِنَ الْمُهْلَكِينَ ﴿٤٨﴾
48. Wakawakadhibisha; basi wakawa miongoni mwa walioangamizwa.


وَلَقَدْ آتَيْنَا مُوسَى الْكِتَابَ لَعَلَّهُمْ يَهْتَدُونَ ﴿٤٩﴾
49. Na kwa yakini Tulimpa Muwsaa Kitabu (Tawraat) ili waongoke.


وَجَعَلْنَا ابْنَ مَرْيَمَ وَأُمَّهُ آيَةً وَآوَيْنَاهُمَا إِلَىٰ رَبْوَةٍ ذَاتِ قَرَارٍ وَمَعِينٍ ﴿٥٠﴾
50. Na Tukamjaalia mwana wa Maryam na mama yake kuwa ni Aayah (ishara, dalili) na Tukawapa kimbilio katika sehemu iliyoinuka na penye utulivu na chemchemu.


يَا أَيُّهَا الرُّسُلُ كُلُوا مِنَ الطَّيِّبَاتِ وَاعْمَلُوا صَالِحًا ۖ إِنِّي بِمَا تَعْمَلُونَ عَلِيمٌ ﴿٥١﴾
51. (Allaah Akasema): “Enyi Rusuli! Kuleni katika vizuri na tendeni mema, hakika Mimi kwa yale myatendayo ni Mjuzi.”


وَإِنَّ هَـٰذِهِ أُمَّتُكُمْ أُمَّةً وَاحِدَةً وَأَنَا رَبُّكُمْ فَاتَّقُونِ ﴿٥٢﴾
52. “Na kwamba hakika huu ummah wenu, ni ummah mmoja Nami ni Rabb   wenu, basi Nicheni.”


فَتَقَطَّعُوا أَمْرَهُم بَيْنَهُمْ زُبُرًا ۖ كُلُّ حِزْبٍ بِمَا لَدَيْهِمْ فَرِحُونَ ﴿٥٣﴾
53. Wakakatakata makundi na kufarikiana kuhusu Dini yao, kila kundi kwa waliyokuwa nayo linafurahia.


فَذَرْهُمْ فِي غَمْرَتِهِمْ حَتَّىٰ حِينٍ ﴿٥٤﴾
54. Basi waachilie mbali katika mkanganyiko wao kwa muda.


أَيَحْسَبُونَ أَنَّمَا نُمِدُّهُم بِهِ مِن مَّالٍ وَبَنِينَ ﴿٥٥﴾
55. Je, wanadhani kwamba kwa vile Tunavyowakunjulia kwa mali na watoto.


نُسَارِعُ لَهُمْ فِي الْخَيْرَاتِ ۚ بَل لَّا يَشْعُرُونَ ﴿٥٦﴾
56. Tunawaharakishia katika ya kheri?  Bali hawahisi.


إِنَّ الَّذِينَ هُم مِّنْ خَشْيَةِ رَبِّهِم مُّشْفِقُونَ ﴿٥٧﴾
57. Hakika wale ambao kwa kumuogopa Rabb wao ni wenye kukhofu huku wakinyenyekea.


وَالَّذِينَ هُم بِآيَاتِ رَبِّهِمْ يُؤْمِنُونَ ﴿٥٨﴾
58. Na wale ambao Aayaat za Rabb wao wanaziamini.


وَالَّذِينَ هُم بِرَبِّهِمْ لَا يُشْرِكُونَ ﴿٥٩﴾
59. Na wale ambao Rabb wao hawamshirikishi.


وَالَّذِينَ يُؤْتُونَ مَا آتَوا وَّقُلُوبُهُمْ وَجِلَةٌ أَنَّهُمْ إِلَىٰ رَبِّهِمْ رَاجِعُونَ ﴿٦٠﴾
60. Na ambao wanatoa vile walivyopewa na huku nyoyo zao zinakhofu kwamba hakika watarejea kwa Rabb wao.

أُولَـٰئِكَ يُسَارِعُونَ فِي الْخَيْرَاتِ وَهُمْ لَهَا سَابِقُونَ ﴿٦١﴾
61. Hao wanakimbilia katika mambo ya kheri; na wao ndio wenye kuyatanguliza.   


وَلَا نُكَلِّفُ نَفْسًا إِلَّا وُسْعَهَا ۖ وَلَدَيْنَا كِتَابٌ يَنطِقُ بِالْحَقِّ ۚ وَهُمْ لَا يُظْلَمُونَ ﴿٦٢﴾
62. Na wala Hatuikalifishi nafsi yoyote isipokuwa kwa kadiri ya uwezo wake. Na Kwetu kuna Kitabu kisemacho haki; nao hawatodhulumiwa.


بَلْ قُلُوبُهُمْ فِي غَمْرَةٍ مِّنْ هَـٰذَا وَلَهُمْ أَعْمَالٌ مِّن دُونِ ذَٰلِكَ هُمْ لَهَا عَامِلُونَ ﴿٦٣﴾
63. Bali nyoyo zao zimo katika mkanganyiko kutokana na haya; na wanazo ‘amali (ovu) pasi na hizo; wao wanazitenda.


حَتَّىٰ إِذَا أَخَذْنَا مُتْرَفِيهِم بِالْعَذَابِ إِذَا هُمْ يَجْأَرُونَ ﴿٦٤﴾
64. Mpaka Tutakapowachukua kwa adhabu wastareheshwa wao wa anasa za dunia, basi mara wao wanaomba du’aa kwa udhalili na kupiga mayowe.    

لَا تَجْأَرُوا الْيَوْمَ ۖ إِنَّكُم مِّنَّا لَا تُنصَرُونَ ﴿٦٥﴾
65. Msiombe du’aa kwa udhalili na kupiga mayowe leo; hakika nyinyi Kwetu hamtonusuriwa.


قَدْ كَانَتْ آيَاتِي تُتْلَىٰ عَلَيْكُمْ فَكُنتُمْ عَلَىٰ أَعْقَابِكُمْ تَنكِصُونَ ﴿٦٦﴾
66. Kwa yakini zilikuwa Aayaat Zangu zikisomwa kwenu, lakini mlikuwa mnarudi nyuma juu ya visigino vyenu (kukanusha). 

مُسْتَكْبِرِينَ بِهِ سَامِرًا تَهْجُرُونَ ﴿٦٧﴾
67. Mkitakabari kwayo, mkikaa usiku kuisimulia (Qur-aan) kwa kubwabwaja maovu ya batili.


أَفَلَمْ يَدَّبَّرُوا الْقَوْلَ أَمْ جَاءَهُم مَّا لَمْ يَأْتِ آبَاءَهُمُ الْأَوَّلِينَ ﴿٦٨﴾
68. Je, hawakuzingatia kauli (ya Allaah; Qur-aan) au yamewajia yasiyowafikia baba zao wa awali?


أَمْ لَمْ يَعْرِفُوا رَسُولَهُمْ فَهُمْ لَهُ مُنكِرُونَ ﴿٦٩﴾
69. Au hawamtambui Rasuli wao (Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم); basi wao ndio wanamkanusha?


أَمْ يَقُولُونَ بِهِ جِنَّةٌ ۚ بَلْ جَاءَهُم بِالْحَقِّ وَأَكْثَرُهُمْ لِلْحَقِّ كَارِهُونَ ﴿٧٠﴾
70. Au wanasema ana wazimu? Bali amewajia kwa haki; na wengi wao hiyo haki wanaichukia.


وَلَوِ اتَّبَعَ الْحَقُّ أَهْوَاءَهُمْ لَفَسَدَتِ السَّمَاوَاتُ وَالْأَرْضُ وَمَن فِيهِنَّ ۚ بَلْ أَتَيْنَاهُم بِذِكْرِهِمْ فَهُمْ عَن ذِكْرِهِم مُّعْرِضُونَ ﴿٧١﴾
71. Na lau kama haki ingelifuata hawaa zao; basi zingelifisidika mbingu na ardhi na waliokuwemo humo. Bali Tumewaletea ukumbusho wao lakini wao ni wenye kupuuza ukumbusho wao.


أَمْ تَسْأَلُهُمْ خَرْجًا فَخَرَاجُ رَبِّكَ خَيْرٌ ۖ وَهُوَ خَيْرُ الرَّازِقِينَ ﴿٧٢﴾
72. Au unawoamba ujira? Basi ujira wa Rabb wako ni bora. Naye ni Mbora wa wenye kuruzuku.


وَإِنَّكَ لَتَدْعُوهُمْ إِلَىٰ صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ ﴿٧٣﴾
73. Na bila shaka wewe (Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) unawaita kuelekea njia iliyonyooka.



وَإِنَّ الَّذِينَ لَا يُؤْمِنُونَ بِالْآخِرَةِ عَنِ الصِّرَاطِ لَنَاكِبُونَ ﴿٧٤﴾
74. Na hakika wale wasioiamini Aakhirah wanajitenga na njia hiyo.


وَلَوْ رَحِمْنَاهُمْ وَكَشَفْنَا مَا بِهِم مِّن ضُرٍّ لَّلَجُّوا فِي طُغْيَانِهِمْ يَعْمَهُونَ ﴿٧٥﴾
75. Na lau kama Tungeliwarehemu, na Tukawaondoshea dhara waliyokuwa nayo; bila shaka wangeng’ang’ania ukaidi katika upindukaji mipaka wa kuasi kwao, wakitangatanga kwa upofu.


وَلَقَدْ أَخَذْنَاهُم بِالْعَذَابِ فَمَا اسْتَكَانُوا لِرَبِّهِمْ وَمَا يَتَضَرَّعُونَ ﴿٧٦﴾
76. Kwa yakini Tuliwachukua kwa adhabu, basi hawakunyenyekea kujisalimisha kwa Rabb wao, na wala hawakuomba du’aa kwa raghba na khofu.


حَتَّىٰ إِذَا فَتَحْنَا عَلَيْهِم بَابًا ذَا عَذَابٍ شَدِيدٍ إِذَا هُمْ فِيهِ مُبْلِسُونَ ﴿٧٧﴾
77. Mpaka Tulipowafungulia mlango wenye adhabu kali, tahamaki wao humo wenye kujuta, huzuni na kukata tamaa.


وَهُوَ الَّذِي أَنشَأَ لَكُمُ السَّمْعَ وَالْأَبْصَارَ وَالْأَفْئِدَةَ ۚ قَلِيلًا مَّا تَشْكُرُونَ ﴿٧٨﴾
78. Naye (Allaah) Ndiye Ambaye Aliyekuumbieni  kusikia na kuona na nyoyo. Ni machache mnayoshukuru.

وَهُوَ الَّذِي ذَرَأَكُمْ فِي الْأَرْضِ وَإِلَيْهِ تُحْشَرُونَ ﴿٧٩﴾
79. Naye Ndiye Ambaye Amekutawanyeni katika ardhi; na Kwake mtakusanywa.


وَهُوَ الَّذِي يُحْيِي وَيُمِيتُ وَلَهُ اخْتِلَافُ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ ۚ أَفَلَا تَعْقِلُونَ ﴿٨٠﴾
80. Naye Ndiye Ambaye Anayehuisha na kufisha; na ni Yake Pekee mabadiliko ya mfuatano wa usiku na mchana. Je, basi hamtii akilini?


بَلْ قَالُوا مِثْلَ مَا قَالَ الْأَوَّلُونَ ﴿٨١﴾
81. Bali walisema kama walivyosema watu wa awali.


قَالُوا أَإِذَا مِتْنَا وَكُنَّا تُرَابًا وَعِظَامًا أَإِنَّا لَمَبْعُوثُونَ ﴿٨٢﴾
82. Wamesema: “Je, tutakapokufa na tukawa mchanga na mifupa; je, hivi sisi tutafufuliwa?”


لَقَدْ وُعِدْنَا نَحْنُ وَآبَاؤُنَا هَـٰذَا مِن قَبْلُ إِنْ هَـٰذَا إِلَّا أَسَاطِيرُ الْأَوَّلِينَ ﴿٨٣﴾
83. “Kwa yakini tumeahidiwa haya sisi na baba zetu kabla. Haya si chochote isipokuwa hekaya za watu wa kale.”


قُل لِّمَنِ الْأَرْضُ وَمَن فِيهَا إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ ﴿٨٤﴾
84. Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): “Ni ya nani ardhi na wale waliokuwemo humo mkiwa mnajua?”

سَيَقُولُونَ لِلَّـهِ ۚ قُلْ أَفَلَا تَذَكَّرُونَ ﴿٨٥﴾
85. Watasema: “Ni ya Allaah Pekee” Sema: “Je, basi hamkumbuki”?


قُلْ مَن رَّبُّ السَّمَاوَاتِ السَّبْعِ وَرَبُّ الْعَرْشِ الْعَظِيمِ ﴿٨٦﴾
86. Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): “Nani Rabb wa mbingu saba, na Rabb wa ‘Arsh adhimu?”


سَيَقُولُونَ لِلَّـهِ ۚ قُلْ أَفَلَا تَتَّقُونَ ﴿٨٧﴾
87. Watesema: “Ni ya Allaah Pekee” Sema: “Je, basi hamtokuwa na taqwa?


قُلْ مَن بِيَدِهِ مَلَكُوتُ كُلِّ شَيْءٍ وَهُوَ يُجِيرُ وَلَا يُجَارُ عَلَيْهِ إِن كُنتُمْ تَعْلَمُونَ ﴿٨٨﴾
88. Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): “Nani katika mikono Yake uko ufalme wa kila kitu, Naye Ndiye Alindae, na wala hakilindwi chochote kinyume Naye, ikiwa mnajua?”


سَيَقُولُونَ لِلَّـهِ ۚ قُلْ فَأَنَّىٰ تُسْحَرُونَ ﴿٨٩﴾
89. Watasema: “Ni Allaah Pekee” Sema: “Basi vipi mnazugwa?”


بَلْ أَتَيْنَاهُم بِالْحَقِّ وَإِنَّهُمْ لَكَاذِبُونَ ﴿٩٠﴾
90. Bali Tuliwajia kwa haki, na kwa hakika wao ni wenye kukadhibisha.


مَا اتَّخَذَ اللَّـهُ مِن وَلَدٍ وَمَا كَانَ مَعَهُ مِنْ إِلَـٰهٍ ۚ إِذًا لَّذَهَبَ كُلُّ إِلَـٰهٍ بِمَا خَلَقَ وَلَعَلَا بَعْضُهُمْ عَلَىٰ بَعْضٍۚ سُبْحَانَ اللَّـهِ عَمَّا يَصِفُونَ ﴿٩١﴾
91. Allaah Hakujifanyia mwana yeyote, na wala hakukuwa pamoja Naye mwabudiwa yeyote, hapo bila shaka kila mwabudiwa angelichukua vile alivyoviumba, na bila shaka baadhi yao wangeliwashinda wengineo. Subhaana Allaah! Utakasifu ni wa Allaah kutokana na ambayo wanayavumisha.


عَالِمِ الْغَيْبِ وَالشَّهَادَةِ فَتَعَالَىٰ عَمَّا يُشْرِكُونَ ﴿٩٢﴾
92. Mjuzi wa ghayb na dhahiri, basi Ametukuka kwa ‘Uluwa kutokana na yale wanayomshirikisha.


قُل رَّبِّ إِمَّا تُرِيَنِّي مَا يُوعَدُونَ ﴿٩٣﴾
93. Sema: “Rabb wangu! Ukinionyesha yale wanayotishiwa.”


رَبِّ فَلَا تَجْعَلْنِي فِي الْقَوْمِ الظَّالِمِينَ ﴿٩٤﴾
94. “Rabb wangu! Basi usinijaalie katika watu madhalimu.”


وَإِنَّا عَلَىٰ أَن نُّرِيَكَ مَا نَعِدُهُمْ لَقَادِرُونَ ﴿٩٥﴾
95. Na hakika Sisi kukuonyesha yale Tunayowatishia bila shaka ni Wenye kuweza.



ادْفَعْ بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ السَّيِّئَةَ ۚ نَحْنُ أَعْلَمُ بِمَا يَصِفُونَ ﴿٩٦﴾
96.  Zuia maovu kwa (kutenda) yale ambayo ni mema zaidi. Sisi Tunajua zaidi yale wanayoyavumisha. 


وَقُل رَّبِّ أَعُوذُ بِكَ مِنْ هَمَزَاتِ الشَّيَاطِينِ ﴿٩٧﴾
97. Na sema: “Rabb wangu! Najikinga Kwako kutokana na udokezi wa mashaytwaan,”


وَأَعُوذُ بِكَ رَبِّ أَن يَحْضُرُونِ ﴿٩٨﴾
98. “Na najikinga Kwako Rabb wasinihudhurie.”


حَتَّىٰ إِذَا جَاءَ أَحَدَهُمُ الْمَوْتُ قَالَ رَبِّ ارْجِعُونِ ﴿٩٩﴾
99. Mpaka itakapomfikia mmoja wao mauti, atasema: “Rabb wangu! Nirejeshe (duniani).”


لَعَلِّي أَعْمَلُ صَالِحًا فِيمَا تَرَكْتُ ۚ كَلَّا ۚ إِنَّهَا كَلِمَةٌ هُوَ قَائِلُهَا ۖ وَمِن وَرَائِهِم بَرْزَخٌ إِلَىٰ يَوْمِ يُبْعَثُونَ﴿١٠٠﴾
100. “Ili nikatende mema katika yale niliyoyaacha.” (Ataambiwa) “Laa hasha!” Hakika hilo ni neno alisemaye yeye tu.  Na nyuma yao kuna barzakh mpaka Siku watakayofufuliwa.


فَإِذَا نُفِخَ فِي الصُّورِ فَلَا أَنسَابَ بَيْنَهُمْ يَوْمَئِذٍ وَلَا يَتَسَاءَلُونَ ﴿١٠١﴾
101. Basi itakapopulizwa baragumu, hakutokuwa na unasaba baina yao Siku hiyo, na wala hawatoulizana.

فَمَن ثَقُلَتْ مَوَازِينُهُ فَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ ﴿١٠٢﴾
102. Basi yule ambaye mizani yake itakuwa nzito, hao ndio wenye kufaulu.


وَمَنْ خَفَّتْ مَوَازِينُهُ فَأُولَـٰئِكَ الَّذِينَ خَسِرُوا أَنفُسَهُمْ فِي جَهَنَّمَ خَالِدُونَ ﴿١٠٣﴾
103. Na yule ambaye mizani yake itakuwa khafifu, basi hao ni ambao wamekhasirika nafsi zao; katika Jahannam ni wenye kudumu.

تَلْفَحُ وُجُوهَهُمُ النَّارُ وَهُمْ فِيهَا كَالِحُونَ ﴿١٠٤﴾
104. Moto utababua nyuso zao; nao humo watakuwa ni wenye midomo iliyosinyaa na kuvutika mbali na meno.


أَلَمْ تَكُنْ آيَاتِي تُتْلَىٰ عَلَيْكُمْ فَكُنتُم بِهَا تُكَذِّبُونَ ﴿١٠٥﴾
105. (Wataambiwa): “Je, hazikuwa Aayaat Zangu zinasomwa kwenu na nyinyi mkawa mnazikadhibisha?”


قَالُوا رَبَّنَا غَلَبَتْ عَلَيْنَا شِقْوَتُنَا وَكُنَّا قَوْمًا ضَالِّينَ ﴿١٠٦﴾
106. Watasema: “Rabb wetu!  Imetughilibu ufedhuli wetu, na tulikuwa watu waliopotea.”


رَبَّنَا أَخْرِجْنَا مِنْهَا فَإِنْ عُدْنَا فَإِنَّا ظَالِمُونَ ﴿١٠٧﴾
107. “Rabb wetu!  Tutoe humo (motoni); na tukirudia tena, basi hakika sisi ni madhalimu.”


قَالَ اخْسَئُوا فِيهَا وَلَا تُكَلِّمُونِ ﴿١٠٨﴾
108. Wataambiwa: “Hizikeni humo! Na wala msinisemeshe!”


إِنَّهُ كَانَ فَرِيقٌ مِّنْ عِبَادِي يَقُولُونَ رَبَّنَا آمَنَّا فَاغْفِرْ لَنَا وَارْحَمْنَا وَأَنتَ خَيْرُ الرَّاحِمِينَ ﴿١٠٩﴾
109. Hakika lilikuwa kundi miongoni mwa waja Wangu, wakisema: “Rabb wetu! Tumeamini, basi Tughufurie na Uturehemu, Nawe ni Mbora wa wenye kurehemu.”


فَاتَّخَذْتُمُوهُمْ سِخْرِيًّا حَتَّىٰ أَنسَوْكُمْ ذِكْرِي وَكُنتُم مِّنْهُمْ تَضْحَكُونَ ﴿١١٠﴾
110. Mkawafanyia dhihaka, hadi wakakusahaulisheni na kunidhukuru na mlikuwa ni wenye kuwacheka.


إِنِّي جَزَيْتُهُمُ الْيَوْمَ بِمَا صَبَرُوا أَنَّهُمْ هُمُ الْفَائِزُونَ ﴿١١١﴾
111. Hakika Mimi Nimewalipa leo (Jannah) kwa yale waliyokuwa wakisubiri; hakika wao ndio wenye kufuzu.

قَالَ كَمْ لَبِثْتُمْ فِي الْأَرْضِ عَدَدَ سِنِينَ ﴿١١٢﴾
112. (Allaah) Atasema: “Muda gani mlikaa katika ardhi kwa idadi ya miaka?


قَالُوا لَبِثْنَا يَوْمًا أَوْ بَعْضَ يَوْمٍ فَاسْأَلِ الْعَادِّينَ ﴿١١٣﴾
113. Watasema: “Tumekaa siku au sehemu tu ya siku. Basi waulize wanaohesabu.”


قَالَ إِن لَّبِثْتُمْ إِلَّا قَلِيلًا ۖ لَّوْ أَنَّكُمْ كُنتُمْ تَعْلَمُونَ ﴿١١٤﴾
114. (Allaah) Atasema: “Hamkukaa (huko duniani) isipokuwa kidogo tu, lau mngelikuwa mnajua.”



أَفَحَسِبْتُمْ أَنَّمَا خَلَقْنَاكُمْ عَبَثًا وَأَنَّكُمْ إِلَيْنَا لَا تُرْجَعُونَ ﴿١١٥﴾
115. “Je, mlidhania kwamba Sisi Tulikuumbeni bila kusudio mcheze tu na kwamba nyinyi Kwetu hamtorejeshwa?”


فَتَعَالَى اللَّـهُ الْمَلِكُ الْحَقُّ ۖ لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ رَبُّ الْعَرْشِ الْكَرِيمِ ﴿١١٦﴾
116. Basi Ametukuka Allaah Mfalme wa hak). Hapana Muabudiwa wa haki ila Yeye. Rabb wa ‘Arsh tukufu.


وَمَن يَدْعُ مَعَ اللَّـهِ إِلَـٰهًا آخَرَ لَا بُرْهَانَ لَهُ بِهِ فَإِنَّمَا حِسَابُهُ عِندَ رَبِّهِ ۚ إِنَّهُ لَا يُفْلِحُ الْكَافِرُونَ ﴿١١٧﴾
117. Na yeyote yule anayeomba du’aa (au kuabudu) pamoja na Allaah muabudiwa mwengine hana ushahidi wa wazi wa hilo; basi hakika hesabu yake iko kwa Rabb wake. Hakika hawafaulu makafiri.


وَقُل رَّبِّ اغْفِرْ وَارْحَمْ وَأَنتَ خَيْرُ الرَّاحِمِينَ ﴿١١٨﴾
118. Na sema: “Rabb wangu! Ghufuria na Rehemu, Nawe ni Mbora wa wenye kurehemu.