الرَّعْد
Ar-Ra’d: 13


بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيمِ


المر ۚ تِلْكَ آيَاتُ الْكِتَابِ ۗ وَالَّذِي أُنزِلَ إِلَيْكَ مِن رَّبِّكَ الْحَقُّ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَ النَّاسِ لَا يُؤْمِنُونَ﴿١﴾
1. Alif Laam Miym Raa. Hizo ni Aayaat za Kitabu. Na yale yaliyoteremshwa kwako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) kutoka kwa Rabb wako ni haki; lakini watu wengi hawaamini.


اللَّـهُ الَّذِي رَفَعَ السَّمَاوَاتِ بِغَيْرِ عَمَدٍ تَرَوْنَهَا ۖ ثُمَّ اسْتَوَىٰ عَلَى الْعَرْشِ ۖ وَسَخَّرَ الشَّمْسَ وَالْقَمَرَ ۖ كُلٌّ يَجْرِي لِأَجَلٍ مُّسَمًّى ۚ يُدَبِّرُ الْأَمْرَ يُفَصِّلُ الْآيَاتِ لَعَلَّكُم بِلِقَاءِ رَبِّكُمْ تُوقِنُونَ ﴿٢﴾
2. Allaah Ambaye Ameinua mbingu bila ya nguzo mnaziona; kisha Istawaa[1] juu ya ‘ArshNa Akavitiisha jua na mwezi, vyote vinakwenda mzunguko kwa muda maalumu uliokadiriwa. Anadabiri mambo, Anazifasili waziwazi Aayaat (na ishara) ili huenda mpate kuwa na yakini (kuhusu) kukutana na Rabb wenu.


وَهُوَ الَّذِي مَدَّ الْأَرْضَ وَجَعَلَ فِيهَا رَوَاسِيَ وَأَنْهَارًا ۖ وَمِن كُلِّ الثَّمَرَاتِ جَعَلَ فِيهَا زَوْجَيْنِ اثْنَيْنِ ۖيُغْشِي اللَّيْلَ النَّهَارَ ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ ﴿٣﴾
3. Na Yeye Ndiye Yule Aliyetandaza ardhi na Akajaalia humo milima thabiti na mito, na kila aina ya mazao Amejaalia humo jozi mbili (dume na jike). Anafunika usiku juu ya mchana. Hakika katika hayo kuna Aayaat (ishara, zingatio) kwa watu wanaotafakari.


وَفِي الْأَرْضِ قِطَعٌ مُّتَجَاوِرَاتٌ وَجَنَّاتٌ مِّنْ أَعْنَابٍ وَزَرْعٌ وَنَخِيلٌ صِنْوَانٌ وَغَيْرُ صِنْوَانٍ يُسْقَىٰ بِمَاءٍ وَاحِدٍ وَنُفَضِّلُ بَعْضَهَا عَلَىٰ بَعْضٍ فِي الْأُكُلِ ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِّقَوْمٍ يَعْقِلُونَ ﴿٤﴾
4. Na katika ardhi kuna majimbo yanayokaribiana na mabustani ya mizabibu na mazao (mingineyo) na mitende inayochipuka katika shina moja na isiyochipuka katika shina moja; vinanyweshezwa kwa maji ya aina moja; na Tunafadhilisha ubora baadhi yake juu ya vinginevyo katika ulaji. Hakika katika hayo kuna Aayaat (ishara, zingatio) kwa watu wanaotia akilini.


وَإِن تَعْجَبْ فَعَجَبٌ قَوْلُهُمْ أَإِذَا كُنَّا تُرَابًا أَإِنَّا لَفِي خَلْقٍ جَدِيدٍ ۗ أُولَـٰئِكَ الَّذِينَ كَفَرُوا بِرَبِّهِمْ ۖ وَأُولَـٰئِكَ الْأَغْلَالُ فِي أَعْنَاقِهِمْ ۖ وَأُولَـٰئِكَ أَصْحَابُ النَّارِ ۖ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ ﴿٥﴾
5. Na ukistaajabu (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم), basi cha ajabu ni kauli yao “Je, tukiwa mchanga, hivi kweli sisi tutakuwa kwa yakini katika umbo jipya?” Hao ni wale waliomkufuru Rabb wao. Hao watafungwa minyororo katika shingo zao. Na hao ndio watu wa motoni, wao humo ni wenye kudumu.

وَيَسْتَعْجِلُونَكَ بِالسَّيِّئَةِ قَبْلَ الْحَسَنَةِ وَقَدْ خَلَتْ مِن قَبْلِهِمُ الْمَثُلَاتُ ۗ وَإِنَّ رَبَّكَ لَذُو مَغْفِرَةٍ لِّلنَّاسِ عَلَىٰ ظُلْمِهِمْ ۖ وَإِنَّ رَبَّكَ لَشَدِيدُ الْعِقَابِ ﴿٦﴾
6. Na wanakuhimiza kwa maovu kabla ya mazuri, na hali imekwishapita kabla yao mifano ya adhabu. Na hakika Rabb wako ni Mwenye maghfirah kwa watu juu ya dhulma zao, na hakika Rabb wako ni Mkali wa kuakibu.

وَيَقُولُ الَّذِينَ كَفَرُوا لَوْلَا أُنزِلَ عَلَيْهِ آيَةٌ مِّن رَّبِّهِ ۗ إِنَّمَا أَنتَ مُنذِرٌ ۖ وَلِكُلِّ قَوْمٍ هَادٍ ﴿٧﴾
7. Na wanasema wale waliokufuru: “Kwa nini hakuteremshiwa Aayah (muujiza, ishara) kutoka kwa Rabbwake?” Hakika wewe ni mwonyaji tu na kwa kila kaumu ina mwenye kuongoza.


اللَّـهُ يَعْلَمُ مَا تَحْمِلُ كُلُّ أُنثَىٰ وَمَا تَغِيضُ الْأَرْحَامُ وَمَا تَزْدَادُ ۖ وَكُلُّ شَيْءٍ عِندَهُ بِمِقْدَارٍ ﴿٨﴾
8. Allaah Anajua abebacho mimba kila mwanamke na kinachopunguza matumbo ya uzazi na kinachozidisha (muda au umbile). Na kila kitu Kwake ni kwa kipimo.


عَالِمُ الْغَيْبِ وَالشَّهَادَةِ الْكَبِيرُ الْمُتَعَالِ ﴿٩﴾
9. Mjuzi wa ghayb na dhahiri, Mkubwa wa dhati vitendo na sifa, Mwenye Uluwa Aliyejitukuza kabisa.


سَوَاءٌ مِّنكُم مَّنْ أَسَرَّ الْقَوْلَ وَمَن جَهَرَ بِهِ وَمَنْ هُوَ مُسْتَخْفٍ بِاللَّيْلِ وَسَارِبٌ بِالنَّهَارِ ﴿١٠﴾
10. Ni sawasawa kwenu anayefanya siri kauli (yake), au anayeisema kwa jahara, na anayenyemelea usiku na anayatembea huru mchana.


لَهُ مُعَقِّبَاتٌ مِّن بَيْنِ يَدَيْهِ وَمِنْ خَلْفِهِ يَحْفَظُونَهُ مِنْ أَمْرِ اللَّـهِ ۗ إِنَّ اللَّـهَ لَا يُغَيِّرُ مَا بِقَوْمٍ حَتَّىٰ يُغَيِّرُوا مَا بِأَنفُسِهِمْ ۗ وَإِذَا أَرَادَ اللَّـهُ بِقَوْمٍ سُوءًا فَلَا مَرَدَّ لَهُ ۚ وَمَا لَهُم مِّن دُونِهِ مِن وَالٍ ﴿١١﴾
11. Ana Malaika wanaofuatana kwa zamu mbele yake na nyuma yake wanamhifadhi kwa amri ya Allaah. Hakika Allaah Habadilishi yale yaliyoko kwa watu mpaka wao wenyewe wabadilishe yale yaliyomo katika nafsi zao. Na Allaah Akiwakusudia watu uovu, basi hakuna wa kuurudisha. Na hawana wao pasi Naye mlinzi yeyote.

هُوَ الَّذِي يُرِيكُمُ الْبَرْقَ خَوْفًا وَطَمَعًا وَيُنشِئُ السَّحَابَ الثِّقَالَ ﴿١٢﴾
12.  Yeye Ndiye Anayekuonyesheni umeme kwa khofu na matumaini na Anaanzisha mawingu mazito.


وَيُسَبِّحُ الرَّعْدُ بِحَمْدِهِ وَالْمَلَائِكَةُ مِنْ خِيفَتِهِ وَيُرْسِلُ الصَّوَاعِقَ فَيُصِيبُ بِهَا مَن يَشَاءُ وَهُمْ يُجَادِلُونَ فِي اللَّـهِ وَهُوَ شَدِيدُ الْمِحَالِ ﴿١٣﴾
13. Na radi inamsabbih (Allaah) kwa Himidi Zake na Malaika pia kwa kumkhofu, na Anatuma mingurumo ya radi, humsibu kwayo Amtakaye nao huku (makafiri) wakiwa wanabishana kuhusu Allaah Naye ni Mkali na Mwenye nguvu za kuhujumu. 


لَهُ دَعْوَةُ الْحَقِّ ۖ وَالَّذِينَ يَدْعُونَ مِن دُونِهِ لَا يَسْتَجِيبُونَ لَهُم بِشَيْءٍ إِلَّا كَبَاسِطِ كَفَّيْهِ إِلَى الْمَاءِ لِيَبْلُغَ فَاهُ وَمَا هُوَ بِبَالِغِهِ ۚ وَمَا دُعَاءُ الْكَافِرِينَ إِلَّا فِي ضَلَالٍ ﴿١٤﴾
14.  Ni Kwake wito wa haki. Na wale wanaowaomba badala Yake, hawawaitikii kwa chochote isipokuwa kama anayenyosha viganja vyake viwili vya mikono kwenye maji ili yafikie kinywani mwake, na wala si yenye kuyafikia hata kidogo.  Na du’aa za makafiri hazipo ila katika upotofu. 


وَلِلَّـهِ يَسْجُدُ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ طَوْعًا وَكَرْهًا وَظِلَالُهُم بِالْغُدُوِّ وَالْآصَالِ ۩﴿١٥﴾
15. Na kwa Allaah Pekee Humsujudia vilivyomo katika mbingu na ardhi kwa khiyari na kuchukia na vivuli vyao pia (vinamsujudia) asubuhi na jioni. 


قُلْ مَن رَّبُّ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ قُلِ اللَّـهُ ۚ قُلْ أَفَاتَّخَذْتُم مِّن دُونِهِ أَوْلِيَاءَ لَا يَمْلِكُونَ لِأَنفُسِهِمْ نَفْعًا وَلَا ضَرًّا ۚ قُلْ هَلْ يَسْتَوِي الْأَعْمَىٰ وَالْبَصِيرُ أَمْ هَلْ تَسْتَوِي الظُّلُمَاتُ وَالنُّورُ ۗ أَمْ جَعَلُوا لِلَّـهِ شُرَكَاءَ خَلَقُوا كَخَلْقِهِ فَتَشَابَهَ الْخَلْقُ عَلَيْهِمْ ۚ قُلِ اللَّـهُ خَالِقُ كُلِّ شَيْءٍ وَهُوَ الْوَاحِدُ الْقَهَّارُ ﴿١٦﴾
16.  Sema: “Ni nani Rabb wa mbingu na ardhi?” Sema: “Ni Allaah.” Sema: “Je, mnawafanya wengineo badala Yake kuwa walinzi na hali hawamiliki kwa ajili ya nafsi zao manufaa wala dhara?”  Sema: “Je,   kipofu analingana sawa na mwenye kuona, au je, viza vinalingana sawa na nuru?” Au wamemfanyia Allaah washirika wameumba kama kwamba uumbaji Wake, kisha yakafanana maumbile kwao?  Sema: “Allaah  ni Muumbaji wa kila kitu, Naye ni Mmoja Pekee, Mwenye kudhibiti na kudhalilisha, Mshindi, Asiyepingika.”


أَنزَلَ مِنَ السَّمَاءِ مَاءً فَسَالَتْ أَوْدِيَةٌ بِقَدَرِهَا فَاحْتَمَلَ السَّيْلُ زَبَدًا رَّابِيًا ۚ وَمِمَّا يُوقِدُونَ عَلَيْهِ فِي النَّارِ ابْتِغَاءَ حِلْيَةٍ أَوْ مَتَاعٍ زَبَدٌ مِّثْلُهُ ۚ كَذَٰلِكَ يَضْرِبُ اللَّـهُ الْحَقَّ وَالْبَاطِلَ ۚ فَأَمَّا الزَّبَدُ فَيَذْهَبُ جُفَاءً ۖ وَأَمَّا مَا يَنفَعُ النَّاسَ فَيَمْكُثُ فِي الْأَرْضِ ۚ كَذَٰلِكَ يَضْرِبُ اللَّـهُ الْأَمْثَالَ ﴿١٧﴾
17. (Allaah) Ameteremsha kutoka mbinguni maji na mabonde yakatiririka kwa kadiri yake, kisha mbubujiko ukabeba mapovu ya takataka yanayopanda juu yake. Na katika vile wanavyoviwashia moto ili kutaka mapambo au vyombo hutokea povu vile vile. Hivyo ndivyo Anavyotoa Allaah haki na batili. Basi povu la takataka linapita bure bila ya kufaa. Lakini vile vinavyowafaa watu hubakia ardhini. Hivyo ndivyo Allaah Anavyopiga mifano.


لِلَّذِينَ اسْتَجَابُوا لِرَبِّهِمُ الْحُسْنَىٰ ۚ وَالَّذِينَ لَمْ يَسْتَجِيبُوا لَهُ لَوْ أَنَّ لَهُم مَّا فِي الْأَرْضِ جَمِيعًا وَمِثْلَهُ مَعَهُ لَافْتَدَوْا بِهِ ۚ أُولَـٰئِكَ لَهُمْ سُوءُ الْحِسَابِ وَمَأْوَاهُمْ جَهَنَّمُ ۖ وَبِئْسَ الْمِهَادُ﴿١٨﴾
18. Kwa wale wanaomuitikia Rabb wao watapata Al-Husnaa (Jannah). Na wale wasiomuitikia hata kama wangelikuwa wana vyote viliomo ardhini na mfano wa kama hivyo pamoja, bila shaka wangelivitoa kujikombolea navyo. Hao watapa hesabu mbaya, na makazi yao ni Jahannam. Na mahali pabaya mno pa kupumzikia.


أَفَمَن يَعْلَمُ أَنَّمَا أُنزِلَ إِلَيْكَ مِن رَّبِّكَ الْحَقُّ كَمَنْ هُوَ أَعْمَىٰ ۚ إِنَّمَا يَتَذَكَّرُ أُولُو الْأَلْبَابِ ﴿١٩﴾
19. Je, anayejua kwamba yaliyoteremshwa kwako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) kutoka kwa Rabb wako ni haki ni sawas na ambaye yeye ni kipofu? Hakika wanazingatia wenye akili tu.


الَّذِينَ يُوفُونَ بِعَهْدِ اللَّـهِ وَلَا يَنقُضُونَ الْمِيثَاقَ ﴿٢٠﴾
20.  Ambao wanatimiza ahadi ya Allaah, na wala hawavunji fungamano.


وَالَّذِينَ يَصِلُونَ مَا أَمَرَ اللَّـهُ بِهِ أَن يُوصَلَ وَيَخْشَوْنَ رَبَّهُمْ وَيَخَافُونَ سُوءَ الْحِسَابِ ﴿٢١﴾
21. Na ambao wanaunga yale Aliyoamrisha Allaah kuungwa na wanamkhofu Rabb wao, na wanakhofu hesabu mbaya.


وَالَّذِينَ صَبَرُوا ابْتِغَاءَ وَجْهِ رَبِّهِمْ وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ وَأَنفَقُوا مِمَّا رَزَقْنَاهُمْ سِرًّا وَعَلَانِيَةً وَيَدْرَءُونَ بِالْحَسَنَةِ السَّيِّئَةَ أُولَـٰئِكَ لَهُمْ عُقْبَى الدَّارِ ﴿٢٢﴾
22. Na ambao wamesubiri kutaka Wajihi wa Rabb wao, na wakasimamisha Swalaah, na wakatoa katika yale Tuliyowaruzuku kwa siri na dhahiri, na wanaepusha ovu kwa zuri, hao watapata hatima njema ya makazi ya Aakhirah.


جَنَّاتُ عَدْنٍ يَدْخُلُونَهَا وَمَن صَلَحَ مِنْ آبَائِهِمْ وَأَزْوَاجِهِمْ وَذُرِّيَّاتِهِمْ ۖ وَالْمَلَائِكَةُ يَدْخُلُونَ عَلَيْهِم مِّن كُلِّ بَابٍ﴿٢٣﴾
23. Jannaat  za milele wataingia pamoja na waliotengenea miongoni mwa baba zao na wake zao na dhuria zao. Na Malaika wanawaingilia katika kila milango.


سَلَامٌ عَلَيْكُم بِمَا صَبَرْتُمْ ۚ فَنِعْمَ عُقْبَى الدَّارِ ﴿٢٤﴾
24. “Salaamun ‘Alaykum!" Amani iwe juu yenu kwa yale mliyosubiri. Basi uzuri ulioje hatima njema ya makazi ya Aakhirah.


وَالَّذِينَ يَنقُضُونَ عَهْدَ اللَّـهِ مِن بَعْدِ مِيثَاقِهِ وَيَقْطَعُونَ مَا أَمَرَ اللَّـهُ بِهِ أَن يُوصَلَ وَيُفْسِدُونَ فِي الْأَرْضِ ۙ أُولَـٰئِكَ لَهُمُ اللَّعْنَةُ وَلَهُمْ سُوءُ الدَّارِ ﴿٢٥﴾
25.  Na wale wanaovunja ahadi ya Allaah baada ya kufungamana kwake na wanakata yale Aliyoyaamrisha Allaah kuwa yaungwe na wanafanya ufisadi katika ardhi, hao watapata laana na watapata maskani mabaya (motoni).


اللَّـهُ يَبْسُطُ الرِّزْقَ لِمَن يَشَاءُ وَيَقْدِرُ ۚ وَفَرِحُوا بِالْحَيَاةِ الدُّنْيَا وَمَا الْحَيَاةُ الدُّنْيَا فِي الْآخِرَةِ إِلَّا مَتَاعٌ﴿٢٦﴾
26. Allaah Hukunjua riziki kwa Amtakaye, na Hubana (kwa Amtakaye). Na wamefurahia uhai wa dunia na hali uhai wa dunia si chochote kulingana na Aakhirah ila ni starehe ya muda tu.


وَيَقُولُ الَّذِينَ كَفَرُوا لَوْلَا أُنزِلَ عَلَيْهِ آيَةٌ مِّن رَّبِّهِ ۗ قُلْ إِنَّ اللَّـهَ يُضِلُّ مَن يَشَاءُ وَيَهْدِي إِلَيْهِ مَنْ أَنَابَ﴿٢٧﴾
27. Na wanasema wale waliokufuru: “Kwanini hakuteremshiwa Aayah (muujiza, ishara) kutoka kwa Rabb wake?” Sema: (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) Hakika Allaah Anampotoa Amtakaye na Anamuongoza kuelekea Kwake anayerudi kutubuia


الَّذِينَ آمَنُوا وَتَطْمَئِنُّ قُلُوبُهُم بِذِكْرِ اللَّـهِ ۗ أَلَا بِذِكْرِ اللَّـهِ تَطْمَئِنُّ الْقُلُوبُ ﴿٢٨﴾
28. Wale walioamini na zikatua nyoyo zao kwa kumdhukuru Allaah. Tanabahi!  Kwa kumdhukuru Allaah nyoyo hutulia!

الَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ طُوبَىٰ لَهُمْ وَحُسْنُ مَآبٍ ﴿٢٩﴾
29. Wale walioamini na wakatenda mema watapata ‘twuwbaa’ (hali nzuri) na marejeo mazuri (Jannah).


كَذَٰلِكَ أَرْسَلْنَاكَ فِي أُمَّةٍ قَدْ خَلَتْ مِن قَبْلِهَا أُمَمٌ لِّتَتْلُوَ عَلَيْهِمُ الَّذِي أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ وَهُمْ يَكْفُرُونَ بِالرَّحْمَـٰنِ ۚ قُلْ هُوَ رَبِّي لَا إِلَـٰهَ إِلَّا هُوَ عَلَيْهِ تَوَكَّلْتُ وَإِلَيْهِ مَتَابِ ﴿٣٠﴾
30.  Hivyo ndivyo Tumekutuma katika Ummah uliokwishapita kabla yake umati nyingine ili uwasomee yale Tuliyokufunulia Wahy; nao wanamkufuru Ar-Rahmaan. Sema: “Yeye Ndiye Rabb wangu, hapana Muabudiwa wa haki ila Yeye, Kwake natawakali na Kwake ni mahali pangu pa kurejea kutubu.”


وَلَوْ أَنَّ قُرْآنًا سُيِّرَتْ بِهِ الْجِبَالُ أَوْ قُطِّعَتْ بِهِ الْأَرْضُ أَوْ كُلِّمَ بِهِ الْمَوْتَىٰ ۗ بَل لِّلَّـهِ الْأَمْرُ جَمِيعًا ۗ أَفَلَمْ يَيْأَسِ الَّذِينَ آمَنُوا أَن لَّوْ يَشَاءُ اللَّـهُ لَهَدَى النَّاسَ جَمِيعًا ۗ وَلَا يَزَالُ الَّذِينَ كَفَرُوا تُصِيبُهُم بِمَا صَنَعُوا قَارِعَةٌ أَوْ تَحُلُّ قَرِيبًا مِّن دَارِهِمْ حَتَّىٰ يَأْتِيَ وَعْدُ اللَّـهِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ لَا يُخْلِفُ الْمِيعَادَ ﴿٣١﴾
31. Na kama ingelikuweko Qur-aan ambayo kwayo majabali yangeliondoshwa au kwayo ardhi ingelipasuliwa au kwayo wafu wangelisemeshwa (basi ni Qur-aan hii hii), bali ni ya Allaah Pekee amri ya mambo yote. Je, hawakukata tamaa  wale walioamini kwamba kama Angetaka Allaah bila shaka Angeliwaongoa watu wote. Na hayatoacha kuwasibu wale waliokufuru maafa ya kuteketeza kwa sababu ya yale waliyoyatenda, au yakawateremkia karibu na nyumba zao, mpaka ifike ahadi ya Allaah. Hakika Allaah Hakhalifu miadi (Yake).


وَلَقَدِ اسْتُهْزِئَ بِرُسُلٍ مِّن قَبْلِكَ فَأَمْلَيْتُ لِلَّذِينَ كَفَرُوا ثُمَّ أَخَذْتُهُمْ ۖ فَكَيْفَ كَانَ عِقَابِ ﴿٣٢﴾
32. Na kwa yakini walifanyiwa istihzai Rusuli kabla yako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) Nikawapa muhula wale waliokufuru, kisha Nikawachukua kuwaadhibu. Basi vipi ilikuwa (kali) kulipiza ikabu Yangu.


أَفَمَنْ هُوَ قَائِمٌ عَلَىٰ كُلِّ نَفْسٍ بِمَا كَسَبَتْ ۗ وَجَعَلُوا لِلَّـهِ شُرَكَاءَ قُلْ سَمُّوهُمْ ۚ أَمْ تُنَبِّئُونَهُ بِمَا لَا يَعْلَمُ فِي الْأَرْضِ أَم بِظَاهِرٍ مِّنَ الْقَوْلِ ۗ بَلْ زُيِّنَ لِلَّذِينَ كَفَرُوا مَكْرُهُمْ وَصُدُّوا عَنِ السَّبِيلِ ۗ وَمَن يُضْلِلِ اللَّـهُ فَمَا لَهُ مِنْ هَادٍ ﴿٣٣﴾
33. Je, basi Anayeisimamia kila nafsi kwa yale iliyoyachuma, (ni sawa na miungu ya uongo?). Hata hivyo wanamfanyia Allaah washirika. Sema: “Watajeni!” Au, mnampa habari kwa yale Asiyoyajua katika ardhi, au ni kudhihirisha maneno ya uongo tu?” Bali waliokufuru wamepambiwa mbinu zao na wamezuiliwa na njia (ya haki). Na ambaye Allaah Amempotoa, basi hana wa kumuongoa.

لَّهُمْ عَذَابٌ فِي الْحَيَاةِ الدُّنْيَا ۖ وَلَعَذَابُ الْآخِرَةِ أَشَقُّ ۖ وَمَا لَهُم مِّنَ اللَّـهِ مِن وَاقٍ ﴿٣٤﴾
34. Watapata adhabu katika uhai wa dunia, na bila shaka adhabu ya Aakhirah ni ya mashaka zaidi. Na hawatopata mbele ya Allaah wa kuwahami.


مَّثَلُ الْجَنَّةِ الَّتِي وُعِدَ الْمُتَّقُونَ ۖ تَجْرِي مِن تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ ۖ أُكُلُهَا دَائِمٌ وَظِلُّهَا ۚ تِلْكَ عُقْبَى الَّذِينَ اتَّقَوا ۖوَّعُقْبَى الْكَافِرِينَ النَّارُ ﴿٣٥﴾
35. Mfano wa Jannah ambayo wameahidiwa wenye taqwa, inapita chini yake mito. Makulaji yake ya kudumu, na pia kivuli chake. Hiyo ndiyo hatima ya Aakhirah ya wale waliokuwa na taqwa. Na hatima ya makafiri ni moto.


وَالَّذِينَ آتَيْنَاهُمُ الْكِتَابَ يَفْرَحُونَ بِمَا أُنزِلَ إِلَيْكَ ۖ وَمِنَ الْأَحْزَابِ مَن يُنكِرُ بَعْضَهُ ۚ قُلْ إِنَّمَا أُمِرْتُ أَنْ أَعْبُدَ اللَّـهَ وَلَا أُشْرِكَ بِهِ ۚ إِلَيْهِ أَدْعُو وَإِلَيْهِ مَآبِ ﴿٣٦﴾
36. Na wale Tuliowapa Kitabu (wakaamini) wanafurahia kwa yale yaliyoteremshwa kwako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم). Na miongoni mwa makundi wako wanaoyakanusha baadhi yake. Sema: “Hakika mimi nimeamrishwa nimwabudu Allaah, na nisimshirikishe. Kwake nalingania na Kwake ni marejeo yangu.”


وَكَذَٰلِكَ أَنزَلْنَاهُ حُكْمًا عَرَبِيًّا ۚ وَلَئِنِ اتَّبَعْتَ أَهْوَاءَهُم بَعْدَ مَا جَاءَكَ مِنَ الْعِلْمِ مَا لَكَ مِنَ اللَّـهِ مِن وَلِيٍّ وَلَا وَاقٍ ﴿٣٧﴾
37.  Na hivyo ndivyo Tumeiteremsha (Qur-aan) kuwa ni hukman (shariy’ah) kwa Kiarabu. Na kama utafuata hawaa zao baada ya kukujia elimu, basi hutokuwa na mlinzi, msimamizi yeyote wala mwenye kukuhami mbele ya Allaah. 


وَلَقَدْ أَرْسَلْنَا رُسُلًا مِّن قَبْلِكَ وَجَعَلْنَا لَهُمْ أَزْوَاجًا وَذُرِّيَّةً ۚ وَمَا كَانَ لِرَسُولٍ أَن يَأْتِيَ بِآيَةٍ إِلَّا بِإِذْنِ اللَّـهِ ۗ لِكُلِّ أَجَلٍ كِتَابٌ﴿٣٨﴾
38. Na kwa yakini Tulituma Rusuli kabla yako, na Tukawajaalia wawe na wake na dhuria. Na haiwi kwa Rasuli yeyote kuleta Aayah (muujiza) isipokuwa kwa idhini ya Allaah. Kwa kila kipindi kina hukmu iliyoandikwa.


يَمْحُو اللَّـهُ مَا يَشَاءُ وَيُثْبِتُ ۖ وَعِندَهُ أُمُّ الْكِتَابِ﴿٣٩﴾
39. Allaah Anafuta yale Ayatakayo na Anathibitisha (Ayatakayo), na Kwake kiko Mama wa Kitabu.


وَإِن مَّا نُرِيَنَّكَ بَعْضَ الَّذِي نَعِدُهُمْ أَوْ نَتَوَفَّيَنَّكَ فَإِنَّمَا عَلَيْكَ الْبَلَاغُ وَعَلَيْنَا الْحِسَابُ ﴿٤٠﴾
40. Na kama Tutakuonyesha (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) baadhi ya yale Tunayowaahidi (ya adhabu), au Tukikufisha; basi hakika juu yako ni kubalighisha tu (ujumbe), na juu Yetu ni hesabu.


أَوَلَمْ يَرَوْا أَنَّا نَأْتِي الْأَرْضَ نَنقُصُهَا مِنْ أَطْرَافِهَا ۚ وَاللَّـهُ يَحْكُمُ لَا مُعَقِّبَ لِحُكْمِهِ ۚ وَهُوَ سَرِيعُ الْحِسَابِ﴿٤١﴾
41. Je, hawaoni kwamba Tunaifikia ardhi, Tunaipunguza katika mipaka yake? Na Allaah Anahukumu na hakuna wa kupinga hukumu Yake. Naye ni Mwepesi wa kuhesabu.


وَقَدْ مَكَرَ الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ فَلِلَّـهِ الْمَكْرُ جَمِيعًا ۖ يَعْلَمُ مَا تَكْسِبُ كُلُّ نَفْسٍ ۗ وَسَيَعْلَمُ الْكُفَّارُ لِمَنْ عُقْبَى الدَّارِ ﴿٤٢﴾
42. Na kwa yakini walifanya njama wale wa kabla yao, basi ni ya Allaah mipango yote (ya kulipiza njama). Allaah Anajua yale yote yanayochumwa na kila nafsi. Na makafiri watajua ni ya nani itakuwa hatima njema ya makazi ya Aakhirah.


وَيَقُولُ الَّذِينَ كَفَرُوا لَسْتَ مُرْسَلًا ۚ قُلْ كَفَىٰ بِاللَّـهِ شَهِيدًا بَيْنِي وَبَيْنَكُمْ وَمَنْ عِندَهُ عِلْمُ الْكِتَابِ﴿٤٣﴾
43.  Na wanasema waliokufuru: “Wewe si Rasuli uliyetumwa.” Sema (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم): “Anatosheleza Allaah kuwa ni Shahidi baina yangu na baina yenu, na pia (shahidi) yule mwenye elimu ya Kitabu.” 


 
[1] Maana ya Istawaa: Yuko juu kwa namna inayolingana na Utukufu Wake Yeye Mwenyewe Allaah. Na rejea tanbih kwa faida bayana: (2: 29).