الأَنْفَال
Al-Anfaal: 8



بِسْمِ اللَّـهِ الرَّحْمَـٰنِ الرَّحِيم



يَسْأَلُونَكَ عَنِ الْأَنفَالِ ۖ قُلِ الْأَنفَالُ لِلَّـهِ وَالرَّسُولِ ۖ فَاتَّقُوا اللَّـهَ وَأَصْلِحُوا ذَاتَ بَيْنِكُمْ ۖ وَأَطِيعُوا اللَّـهَ وَرَسُولَهُ إِن كُنتُم مُّؤْمِنِينَ﴿١﴾
1. Wanakuuliza (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) kuhusu ngawira; sema: ngawira ni ya Allaah na Rasuli. Basi mcheni Allaah na tengenezeni yaliyo baina yenu. Na mtiini Allaah na Rasuli Wake mkiwa ni Waumini.


إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ الَّذِينَ إِذَا ذُكِرَ اللَّـهُ وَجِلَتْ قُلُوبُهُمْ وَإِذَا تُلِيَتْ عَلَيْهِمْ آيَاتُهُ زَادَتْهُمْ إِيمَانًا وَعَلَىٰ رَبِّهِمْ يَتَوَكَّلُونَ﴿٢﴾
2. Hakika Waumini ni wale ambao Anapokumbukwa na kutajwa Allaah, nyoyo zao zinajaa khofu na wanaposomewa Aayaat Zake huwazidishia iymaan, na kwa Rabb wao wanatawakali.


الَّذِينَ يُقِيمُونَ الصَّلَاةَ وَمِمَّا رَزَقْنَاهُمْ يُنفِقُونَ﴿٣﴾
3. Ambao wanasimamisha Swalaah na katika yale Tuliyowaruzuku hutoa.


أُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُؤْمِنُونَ حَقًّا ۚ لَّهُمْ دَرَجَاتٌ عِندَ رَبِّهِمْ وَمَغْفِرَةٌ وَرِزْقٌ كَرِيمٌ﴿٤﴾
4. Hao ndio Waumini wa kweli!  Wana daraja (za Jannah) kwa Rabb wao na maghfirah na riziki karimu.


كَمَا أَخْرَجَكَ رَبُّكَ مِن بَيْتِكَ بِالْحَقِّ وَإِنَّ فَرِيقًا مِّنَ الْمُؤْمِنِينَ لَكَارِهُونَ﴿٥﴾
5. Kama Alivyokutoa Rabb wako (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) kutoka nyumbani kwako kwa haki, na hakika kundi miongoni mwa Waumini bila shaka ni wenye kuchukia.


يُجَادِلُونَكَ فِي الْحَقِّ بَعْدَ مَا تَبَيَّنَ كَأَنَّمَا يُسَاقُونَ إِلَى الْمَوْتِ وَهُمْ يَنظُرُونَ﴿٦﴾
6. Wanabishana nawe katika haki baada ya kubainika, kama kwamba wanasukumwa katika mauti nao huku wanatazama.


وَإِذْ يَعِدُكُمُ اللَّـهُ إِحْدَى الطَّائِفَتَيْنِ أَنَّهَا لَكُمْ وَتَوَدُّونَ أَنَّ غَيْرَ ذَاتِ الشَّوْكَةِ تَكُونُ لَكُمْ وَيُرِيدُ اللَّـهُ أَن يُحِقَّ الْحَقَّ بِكَلِمَاتِهِ وَيَقْطَعَ دَابِرَ الْكَافِرِينَ﴿٧﴾
7. Na (kumbukeni) pale Allaah Alipokuahidini moja kati ya makundi mawili (la msafara au la jeshi) kwamba ni lenu; nanyi mkatamani kwamba lisilo na silaha liwe wenu, na Allaah Anataka Athibitishe haki kwa maneno Yake, na Akate mizizi ya makafiri.


لِيُحِقَّ الْحَقَّ وَيُبْطِلَ الْبَاطِلَ وَلَوْ كَرِهَ الْمُجْرِمُونَ﴿٨﴾
8. Ili Athibitishe haki na Abatilishe ubatilifu japokuwa wahalifu wamekirihika.


إِذْ تَسْتَغِيثُونَ رَبَّكُمْ فَاسْتَجَابَ لَكُمْ أَنِّي مُمِدُّكُم بِأَلْفٍ مِّنَ الْمَلَائِكَةِ مُرْدِفِينَ﴿٩﴾
9. Na (kumbukeni) pale mlipomuomba uokovu Rabb wenu Naye Akakuitikieni kuwa: “Hakika Mimi Nitakusaidieni kwa Malaika elfu wafuatanao mfululizo.”


وَمَا جَعَلَهُ اللَّـهُ إِلَّا بُشْرَىٰ وَلِتَطْمَئِنَّ بِهِ قُلُوبُكُمْ ۚ وَمَا النَّصْرُ إِلَّا مِنْ عِندِ اللَّـهِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ﴿١٠﴾
10. Na Allaah Hakujaalia haya isipokuwa ni bishara na ili zitumainike nyoyo zenu kwayo. Na hakuna nusura isipokuwa kutoka kwa Allaah. Hakika Allaah ni Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika, Mwenye hikmah wa yote.


إِذْ يُغَشِّيكُمُ النُّعَاسَ أَمَنَةً مِّنْهُ وَيُنَزِّلُ عَلَيْكُم مِّنَ السَّمَاءِ مَاءً لِّيُطَهِّرَكُم بِهِ وَيُذْهِبَ عَنكُمْ رِجْزَ الشَّيْطَانِ وَلِيَرْبِطَ عَلَىٰ قُلُوبِكُمْ وَيُثَبِّتَ بِهِ الْأَقْدَامَ﴿١١﴾
11. (Kumbukeni) Pale Alipokufunikeni kwa usingizi (kuwa ni) amani kutoka Kwake, na Akakuteremshieni maji kutoka mbinguni, ili Akutwaharisheni kwayo, na Akuondosheeni wasiwasi na rai ovu za shaytwaan, na ili Atie nguvu nyoyo zenu, na Athibitishe kwayo miguu.


إِذْ يُوحِي رَبُّكَ إِلَى الْمَلَائِكَةِ أَنِّي مَعَكُمْ فَثَبِّتُوا الَّذِينَ آمَنُوا ۚ سَأُلْقِي فِي قُلُوبِ الَّذِينَ كَفَرُوا الرُّعْبَ فَاضْرِبُوا فَوْقَ الْأَعْنَاقِ وَاضْرِبُوا مِنْهُمْ كُلَّ بَنَانٍ﴿١٢﴾
12. (Kumbuka) Pale Rabb wako Alipowatia ilhamu Malaika (kuwaambia): “Hakika Mimi Niko pamoja nanyi; basi wathibitisheni wale walioamini. Nitavurumisha kizaazaa katika nyoyo za waliokufuru. Basi wapigeni juu ya shingo na wapigeni kila kiungo.”


ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ شَاقُّوا اللَّـهَ وَرَسُولَهُ ۚ وَمَن يُشَاقِقِ اللَّـهَ وَرَسُولَهُ فَإِنَّ اللَّـهَ شَدِيدُ الْعِقَابِ﴿١٣﴾
13. Hivyo kwa kuwa wao wamempinga Allaah na Rasuli Wake. Na yeyote ampingae Allaah na Rasuli Wake basi hakika Allaah ni Mkali wa kuakibu.


ذَٰلِكُمْ فَذُوقُوهُ وَأَنَّ لِلْكَافِرِينَ عَذَابَ النَّارِ﴿١٤﴾
14. Ndivyo hivyo kwenu (jazaa yenu), basi ionjeni, na kwamba makafiri wana adhabu ya moto.


يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا لَقِيتُمُ الَّذِينَ كَفَرُوا زَحْفًا فَلَا تُوَلُّوهُمُ الْأَدْبَارَ﴿١٥﴾
15. Enyi walioamini! Mtapokutana na wale waliokufuru vitani, msiwageuzie migongo (kukimbia).



وَمَن يُوَلِّهِمْ يَوْمَئِذٍ دُبُرَهُ إِلَّا مُتَحَرِّفًا لِّقِتَالٍ أَوْ مُتَحَيِّزًا إِلَىٰ فِئَةٍ فَقَدْ بَاءَ بِغَضَبٍ مِّنَ اللَّـهِ وَمَأْوَاهُ جَهَنَّمُۖ وَبِئْسَ الْمَصِيرُ﴿١٦﴾
16. Na yeyote atakayewageuzia mgongo wake siku hiyo - isipokuwa akigeuka kwa kufanya mbinu za kupigana au (amegeuka) kwa kujiunga na kikosi (kingine cha Waislamu) - basi amestahiki ghadhabu ya Allaah, na makazi yake ni Jahannam, na ni pabaya palioje mahali pa kuishia.


فَلَمْ تَقْتُلُوهُمْ وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ قَتَلَهُمْ ۚ وَمَا رَمَيْتَ إِذْ رَمَيْتَ وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ رَمَىٰ ۚ وَلِيُبْلِيَ الْمُؤْمِنِينَ مِنْهُ بَلَاءً حَسَنًا ۚ إِنَّ اللَّـهَ سَمِيعٌ عَلِيمٌ﴿١٧﴾
17. Hamkuwaua (nyinyi), lakini Allaah Ndiye Aliyewaua. Na wala hukurusha (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم mchanga) pale uliporusha lakini Allaah Ndiye Aliyerusha; ili Awajaribu Waumini jaribio zuri kutoka Kwake. Hakika Allaah ni Mwenye kusikia yote, Mjuzi wa yote.


ذَٰلِكُمْ وَأَنَّ اللَّـهَ مُوهِنُ كَيْدِ الْكَافِرِينَ﴿١٨﴾
18. Ndivyo hivyo (Amekufanyieni Allaah), na kwamba Allaah Adhoofishe mbinu za makafiri.


إِن تَسْتَفْتِحُوا فَقَدْ جَاءَكُمُ الْفَتْحُ ۖ وَإِن تَنتَهُوا فَهُوَ خَيْرٌ لَّكُمْ ۖ وَإِن تَعُودُوا نَعُدْ وَلَن تُغْنِيَ عَنكُمْ فِئَتُكُمْ شَيْئًا وَلَوْ كَثُرَتْ وَأَنَّ اللَّـهَ مَعَ الْمُؤْمِنِينَ﴿١٩﴾
19. Mkitafuta hukmu (enyi makafiri), basi imeshakujieni hukmu. Na mkikoma (uhalifu) basi hivyo ni kheri kwenu. Na mkirudia (kuhujumu) Nasi Tutarudia, na wala kikosi chenu hakitokufaeni kitu chochote japo kikikithiri. Na kwamba Allaah Yu Pamoja na Waumini.


يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّـهَ وَرَسُولَهُ وَلَا تَوَلَّوْا عَنْهُ وَأَنتُمْ تَسْمَعُونَ﴿٢٠﴾
20. Enyi walioamini! Mtiini Allaah na Rasuli Wake; na wala msijiepushe nazo (amri za Rasuli) na hali nyinyi mnasikia. 

وَلَا تَكُونُوا كَالَّذِينَ قَالُوا سَمِعْنَا وَهُمْ لَا يَسْمَعُونَ﴿٢١﴾
21. Na wala msiwe kama wale waliosema: “Tumesikia”; na hali wao hawasikii.


إِنَّ شَرَّ الدَّوَابِّ عِندَ اللَّـهِ الصُّمُّ الْبُكْمُ الَّذِينَ لَا يَعْقِلُونَ﴿٢٢﴾
22. Hakika viumbe viovu kabisa mbele ya Allaah ni (wanaojifanya) viziwi, mabubu ambao hawatumii akili.


وَلَوْ عَلِمَ اللَّـهُ فِيهِمْ خَيْرًا لَّأَسْمَعَهُمْ ۖ وَلَوْ أَسْمَعَهُمْ لَتَوَلَّوا وَّهُم مُّعْرِضُونَ﴿٢٣﴾
23. Na kama Allaah Angelijua (kuwa) wana kheri yoyote ile, basi Angeliwasikilizisha; na kama Angeliwasikilizisha, wangeligeuka nao huku wakipuuza.


يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اسْتَجِيبُوا لِلَّـهِ وَلِلرَّسُولِ إِذَا دَعَاكُمْ لِمَا يُحْيِيكُمْ ۖ وَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ يَحُولُ بَيْنَ الْمَرْءِ وَقَلْبِهِ وَأَنَّهُ إِلَيْهِ تُحْشَرُونَ﴿٢٤﴾
24. Enyi walioamini! Muitikieni Allaah na Rasuli Anapokuiteni kwenye yale yenye kukuhuisheni na jueni kwamba Allaah Anaingilia kati baina ya mtu na moyo wake; na kwamba Kwake Pekee mtakusanywa.

وَاتَّقُوا فِتْنَةً لَّا تُصِيبَنَّ الَّذِينَ ظَلَمُوا مِنكُمْ خَاصَّةً ۖ وَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ شَدِيدُ الْعِقَابِ﴿٢٥﴾
25. Na ogopeni fitnah (mitihani na adhabu) ambayo haitowasibu pekee wale waliodhulumu (nafsi zao) miongoni mwenu. Na jueni kwamba Allaah ni Mkali wa kuakibu.


وَاذْكُرُوا إِذْ أَنتُمْ قَلِيلٌ مُّسْتَضْعَفُونَ فِي الْأَرْضِ تَخَافُونَ أَن يَتَخَطَّفَكُمُ النَّاسُ فَآوَاكُمْ وَأَيَّدَكُم بِنَصْرِهِ وَرَزَقَكُم مِّنَ الطَّيِّبَاتِ لَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ﴿٢٦﴾
26. Na kumbukeni (pale) mlipokuwa wachache, mkikandamizwa ardhini, mnakhofu watu wasikunyakueni. (Allaah) Akakupeni makazi na Akakutieni nguvu kwa nusra Yake, na Akakuruzukuni katika vizuri mpate kushukuru.


يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا تَخُونُوا اللَّـهَ وَالرَّسُولَ وَتَخُونُوا أَمَانَاتِكُمْ وَأَنتُمْ تَعْلَمُونَ﴿٢٧﴾
27. Enyi walioamini! Msimfanyie khiyana Allaah na Rasuli na (wala) msikhini amana zenu na hali nyinyi mnajua (matokeo yake mabaya).


وَاعْلَمُوا أَنَّمَا أَمْوَالُكُمْ وَأَوْلَادُكُمْ فِتْنَةٌ وَأَنَّ اللَّـهَ عِندَهُ أَجْرٌ عَظِيمٌ﴿٢٨﴾
28.  Na jueni kwamba mali zenu na watoto wenu ni fitnah (jaribio, mtihani) na kwamba kwa Allaah uko ujira adhimu.  


يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِن تَتَّقُوا اللَّـهَ يَجْعَل لَّكُمْ فُرْقَانًا وَيُكَفِّرْ عَنكُمْ سَيِّئَاتِكُمْ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ۗ وَاللَّـهُ ذُو الْفَضْلِ الْعَظِيمِ﴿٢٩﴾
29. Enyi walioamini! Mkimcha Allaah Atakupeni upambanuo wa haki na batili na Atakufutieni maovu yenu, na Atakughufurieni. Na Allaah ni Mwenye fadhila adhimu.


وَإِذْ يَمْكُرُ بِكَ الَّذِينَ كَفَرُوا لِيُثْبِتُوكَ أَوْ يَقْتُلُوكَ أَوْ يُخْرِجُوكَ ۚ وَيَمْكُرُونَ وَيَمْكُرُ اللَّـهُ ۖ وَاللَّـهُ خَيْرُ الْمَاكِرِينَ﴿٣٠﴾
30. Na (kumbuka ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) walipokufanyia njama wale waliokufuru ili wakufunge, au wakuue, au wakutoe (Makkah). Na wanafanya njama, na Allaah Anapanga mipango (ya kuvurumisha njama zao), na Allaah ni Mbora wa wenye kupindua njama.


وَإِذَا تُتْلَىٰ عَلَيْهِمْ آيَاتُنَا قَالُوا قَدْ سَمِعْنَا لَوْ نَشَاءُ لَقُلْنَا مِثْلَ هَـٰذَا ۙ إِنْ هَـٰذَا إِلَّا أَسَاطِيرُ الْأَوَّلِينَ﴿٣١﴾
31. Na wanaposomewa Aayaat Zetu, husema: “Tumekwishasikia. Lau tungelitaka tungelisema kama haya. Haya si chochote isipokuwa ni hekaya za watu wa kale.”


وَإِذْ قَالُوا اللَّـهُمَّ إِن كَانَ هَـٰذَا هُوَ الْحَقَّ مِنْ عِندِكَ فَأَمْطِرْ عَلَيْنَا حِجَارَةً مِّنَ السَّمَاءِ أَوِ ائْتِنَا بِعَذَابٍ أَلِيمٍ﴿٣٢﴾
32. Na (kumbuka) waliposema: “Ee Allaah!  Kama haya (aliyokuja nayo Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) ni haki kutoka Kwako; basi Tunyeshee mvua ya mawe kutoka mbinguni, au Tuletee adhabu iumizayo”

وَمَا كَانَ اللَّـهُ لِيُعَذِّبَهُمْ وَأَنتَ فِيهِمْ ۚ وَمَا كَانَ اللَّـهُ مُعَذِّبَهُمْ وَهُمْ يَسْتَغْفِرُونَ﴿٣٣﴾
33. Na Allaah Hakuwa wa kuwaadhibu na hali wewe (Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) uko nao. Na Allaah Hakuwa wa kuwaadhibu hali wao wanaomba maghfirah.


وَمَا لَهُمْ أَلَّا يُعَذِّبَهُمُ اللَّـهُ وَهُمْ يَصُدُّونَ عَنِ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِ وَمَا كَانُوا أَوْلِيَاءَهُ ۚ إِنْ أَوْلِيَاؤُهُ إِلَّا الْمُتَّقُونَ وَلَـٰكِنَّ أَكْثَرَهُمْ لَا يَعْلَمُونَ﴿٣٤﴾
34. Na wana nini hata Allaah Asiwaadhibu na hali wao wanazuia (watu) na Al-Masjidil-Haraam, na hawakuwa walinzi wake (Msikiti huo). Hawakuwa walinzi wake isipokuwa wenye taqwa; lakini wengi wao hawajui.


وَمَا كَانَ صَلَاتُهُمْ عِندَ الْبَيْتِ إِلَّا مُكَاءً وَتَصْدِيَةً ۚ فَذُوقُوا الْعَذَابَ بِمَا كُنتُمْ تَكْفُرُونَ﴿٣٥﴾
35. Na haikuwa Swalaah zao (makafiri) kwenye Nyumba (Al-Ka’bah) isipokuwa ni miluzi na kupiga makofi. Basi onjeni adhabu kwa yale mliyokuwa mkikufuru. 


إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا يُنفِقُونَ أَمْوَالَهُمْ لِيَصُدُّوا عَن سَبِيلِ اللَّـهِ ۚ فَسَيُنفِقُونَهَا ثُمَّ تَكُونُ عَلَيْهِمْ حَسْرَةً ثُمَّ يُغْلَبُونَ ۗ وَالَّذِينَ كَفَرُوا إِلَىٰ جَهَنَّمَ يُحْشَرُونَ﴿٣٦﴾
36. Hakika wale waliokufuru wanatoa mali zao ili wazuie njia ya Allaah. Basi watazitoa, kisha itakuwa ni majuto juu yao, kisha watashindwa. Na wale waliokufuru watakusanywa kwenye Jahannam.


لِيَمِيزَ اللَّـهُ الْخَبِيثَ مِنَ الطَّيِّبِ وَيَجْعَلَ الْخَبِيثَ بَعْضَهُ عَلَىٰ بَعْضٍ فَيَرْكُمَهُ جَمِيعًا فَيَجْعَلَهُ فِي جَهَنَّمَۚ أُولَـٰئِكَ هُمُ الْخَاسِرُونَ﴿٣٧﴾
37. Ili Allaah Apambanue waovu na wema, kisha Aweke waovu juu ya waovu wengine, kisha Awarundike pamoja Awatie katika Jahannam. Hao ndio waliokhasirika.


قُل لِّلَّذِينَ كَفَرُوا إِن يَنتَهُوا يُغْفَرْ لَهُم مَّا قَدْ سَلَفَ وَإِن يَعُودُوا فَقَدْ مَضَتْ سُنَّتُ الْأَوَّلِينَ﴿٣٨﴾
38. Waambie waliokufuru kwamba wakikoma wataghufuriwa yaliyopita, lakini wakirudia, basi imekwishapita desturi ya watu wa awali.


وَقَاتِلُوهُمْ حَتَّىٰ لَا تَكُونَ فِتْنَةٌ وَيَكُونَ الدِّينُ كُلُّهُ لِلَّـهِ ۚ فَإِنِ انتَهَوْا فَإِنَّ اللَّـهَ بِمَا يَعْمَلُونَ بَصِيرٌ﴿٣٩﴾
39. Na piganeni nao mpaka kusiweko fitnah (shirki na mateso) na Dini yote iwe kwa ajili ya Allaah, Na wakikoma, basi hakika Allaah kwa wanayoyatenda ni Mwenye kuona.


وَإِن تَوَلَّوْا فَاعْلَمُوا أَنَّ اللَّـهَ مَوْلَاكُمْ ۚ نِعْمَ الْمَوْلَىٰ وَنِعْمَ النَّصِيرُ﴿٤٠﴾
40. Na wakikengeuka, basi jueni kwamba Allaah ni Mola Msaidizi wenu, Mola Mzuri Alioje, na Mnusuraji Mzuri Alioje!


وَاعْلَمُوا أَنَّمَا غَنِمْتُم مِّن شَيْءٍ فَأَنَّ لِلَّـهِ خُمُسَهُ وَلِلرَّسُولِ وَلِذِي الْقُرْبَىٰ وَالْيَتَامَىٰ وَالْمَسَاكِينِ وَابْنِ السَّبِيلِ إِن كُنتُمْ آمَنتُم بِاللَّـهِ وَمَا أَنزَلْنَا عَلَىٰ عَبْدِنَا يَوْمَ الْفُرْقَانِ يَوْمَ الْتَقَى الْجَمْعَانِ ۗ وَاللَّـهُ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ﴿٤١﴾
41. Na jueni ya kwamba ghanima yoyote mnayoipata (vitani), basi humusi yake ni ya Allaah na Rasuli na jamaa wa karibu (wa Rasuli صلى الله عليه وآله وسلم) na (pia) mayatima na maskini na wasafiri (walioharibikiwa); ikiwa nyinyi mumemwamini Allaah na yale Tuliyoyateremsha kwa mja Wetu siku ya upambanuzi (wa haki na batili); siku yaliyokutana makundi mawili (vita vya Badr) na Allaah juu ya kila kitu ni Mweza.


إِذْ أَنتُم بِالْعُدْوَةِ الدُّنْيَا وَهُم بِالْعُدْوَةِ الْقُصْوَىٰ وَالرَّكْبُ أَسْفَلَ مِنكُمْ ۚ وَلَوْ تَوَاعَدتُّمْ لَاخْتَلَفْتُمْ فِي الْمِيعَادِ ۙ وَلَـٰكِن لِّيَقْضِيَ اللَّـهُ أَمْرًا كَانَ مَفْعُولًا لِّيَهْلِكَ مَنْ هَلَكَ عَن بَيِّنَةٍ وَيَحْيَىٰ مَنْ حَيَّ عَن بَيِّنَةٍ ۗوَإِنَّ اللَّـهَ لَسَمِيعٌ عَلِيمٌ﴿٤٢﴾
42. (Kumbukeni) pale nyinyi mlipokuwa kando ya bonde la karibu (na Madiynah), na wao (Makafiri Quraysh) walipokuwa kando ya bonde la mbali, na msafara (uliokuwa wa mali zao) ulikuwa uko chini yenu. Na lau mngeliahidiana (kukutana hapo mlipokutana), basi mngelikhitalifiana katika miadi hiyo, lakini (mlikutana) ili Allaah Akidhie jambo lilokuwa lazima litendwe; ili ahiliki (kwa ukafiri) yule wa kuhiliki kwa hoja bayana na ahuike (kwa iymaan) mwenye kuhuika kwa hoja bayana. Na kwamba Allaah bila shaka ni Mwenye kusikia yote, Mjuzi wa yote.


إِذْ يُرِيكَهُمُ اللَّـهُ فِي مَنَامِكَ قَلِيلًا ۖ وَلَوْ أَرَاكَهُمْ كَثِيرًا لَّفَشِلْتُمْ وَلَتَنَازَعْتُمْ فِي الْأَمْرِ وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ سَلَّمَ ۗإِنَّهُ عَلِيمٌ بِذَاتِ الصُّدُورِ﴿٤٣﴾
43. (Kumbuka ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) pale Allaah Alipokuonyesha wao (makafiri) usingizini mwako kuwa wao ni wachache. Na lau Angelikuonyesha kuwa wao ni wengi, bila shaka (Waumini) mngelivunjikwa moyo, na bila shaka mngelizozana katika jambo hilo (la kupigana), lakini Allaah Amesalimisha (hayo). Hakika Yeye ni Mjuzi kwa yaliyomo vifuani.


وَإِذْ يُرِيكُمُوهُمْ إِذِ الْتَقَيْتُمْ فِي أَعْيُنِكُمْ قَلِيلًا وَيُقَلِّلُكُمْ فِي أَعْيُنِهِمْ لِيَقْضِيَ اللَّـهُ أَمْرًا كَانَ مَفْعُولًا ۗ وَإِلَى اللَّـهِ تُرْجَعُ الْأُمُورُ﴿٤٤﴾
44. Na (kumbukeni) pale Allaah Alipokuonyesheni wao, pale mlipokutana, machoni mwenu (kuwa wao ni) wachache na Akakufanyeni nyinyi kuwa wachache machoni mwao; ili Allaah Akidhie jambo lilokuwa lazima litendwe. Na kwa Allaah Pekee hurejeshwa mambo yote.


يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا لَقِيتُمْ فِئَةً فَاثْبُتُوا وَاذْكُرُوا اللَّـهَ كَثِيرًا لَّعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ﴿٤٥﴾
45. Enyi walioamini! Mtapokutana na kikosi (cha makafiri), basi simameni imara, na mdhukuruni Allaah kwa wingi ili mpate kufaulu.


وَأَطِيعُوا اللَّـهَ وَرَسُولَهُ وَلَا تَنَازَعُوا فَتَفْشَلُوا وَتَذْهَبَ رِيحُكُمْ ۖ وَاصْبِرُوا ۚ إِنَّ اللَّـهَ مَعَ الصَّابِرِينَ﴿٤٦﴾
46. Na mtiini Allaah na Rasuli Wake, na wala msizozane, mtavunjikwa moyo, na zikatoweka nguvu zenu, na subirini. Hakika Allaah Yu Pamoja na wanaosubiri.


وَلَا تَكُونُوا كَالَّذِينَ خَرَجُوا مِن دِيَارِهِم بَطَرًا وَرِئَاءَ النَّاسِ وَيَصُدُّونَ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ ۚ وَاللَّـهُ بِمَا يَعْمَلُونَ مُحِيطٌ﴿٤٧﴾
47. Na wala msiwe kama wale waliotoka majumbani mwao kwa majivuno na riyaa (kujionyesha) kwa watu, na wanazuia njia ya Allaah. Na Allaah kwa yote wanayoyatenda ni Mwenye kuzunguka vyote kwa ujuzi Wake.


وَإِذْ زَيَّنَ لَهُمُ الشَّيْطَانُ أَعْمَالَهُمْ وَقَالَ لَا غَالِبَ لَكُمُ الْيَوْمَ مِنَ النَّاسِ وَإِنِّي جَارٌ لَّكُمْ ۖ فَلَمَّا تَرَاءَتِ الْفِئَتَانِ نَكَصَ عَلَىٰ عَقِبَيْهِ وَقَالَ إِنِّي بَرِيءٌ مِّنكُمْ إِنِّي أَرَىٰ مَا لَا تَرَوْنَ إِنِّي أَخَافُ اللَّـهَ ۚ وَاللَّـهُ شَدِيدُ الْعِقَابِ﴿٤٨﴾
48. Na (kumbukeni) pale shaytwaan alipowapambia ‘amali zao na akasema: “Hakuna watu wa kukushindeni leo, na mimi ni mlinzi  wenu.” Yalipoonana vikosi viwili, (shaytwaan) alirejea nyuma kwa visigino vyake na kusema: “Hakika mimi nimejitoa dhima nanyi (sihusiki), hakika mimi naona msiyoyaona; hakika mimi namukhofu Allaah. Na Allaah ni Mkali wa kuakibu.


إِذْ يَقُولُ الْمُنَافِقُونَ وَالَّذِينَ فِي قُلُوبِهِم مَّرَضٌ غَرَّ هَـٰؤُلَاءِ دِينُهُمْ ۗ وَمَن يَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ فَإِنَّ اللَّـهَ عَزِيزٌ حَكِيمٌ﴿٤٩﴾
49. Na (kumbukeni) pale waliposema wanafiki na wale walio na maradhi katika nyoyo zao: “Dini yao (hawa Waislamu) imewaghuri.” Na anayetawakali kwa Allaah (atashinda tu kwani), hakika Allaah ni Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika, Mwenye hikmah wa yote.


وَلَوْ تَرَىٰ إِذْ يَتَوَفَّى الَّذِينَ كَفَرُوا ۙ الْمَلَائِكَةُ يَضْرِبُونَ وُجُوهَهُمْ وَأَدْبَارَهُمْ وَذُوقُوا عَذَابَ الْحَرِيقِ﴿٥٠﴾
50. Na lau ungeliona pale Malaika wanapowafisha wale waliokufuru, wanawapiga nyuso zao na migongo yao na (wanawaambia): “Onjeni adhabu iunguzayo.”


ذَٰلِكَ بِمَا قَدَّمَتْ أَيْدِيكُمْ وَأَنَّ اللَّـهَ لَيْسَ بِظَلَّامٍ لِّلْعَبِيدِ ﴿٥١﴾
51. “Hayo ni kwa yale (maovu) yaliyotangulizwa na mikono yenu; na kwamba Allaah si Mwenye kudhulumu waja (Wake).


كَدَأْبِ آلِ فِرْعَوْنَ ۙ وَالَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ ۚ كَفَرُوا بِآيَاتِ اللَّـهِ فَأَخَذَهُمُ اللَّـهُ بِذُنُوبِهِمْ ۗ إِنَّ اللَّـهَ قَوِيٌّ شَدِيدُ الْعِقَابِ﴿٥٢﴾
52. (Mwenendo wao ni) Kama mwenendo wa watu wa Fir’awn na wale wa kabla yao. Walizikufuru Aayaat (ishara, hoja) za Allaah; basi Allaah Akawachukuwa kwa (sababu ya) madhambi yao. Hakika Allaah ni Mwenye nguvu zote, Mkali wa kuakibu.


ذَٰلِكَ بِأَنَّ اللَّـهَ لَمْ يَكُ مُغَيِّرًا نِّعْمَةً أَنْعَمَهَا عَلَىٰ قَوْمٍ حَتَّىٰ يُغَيِّرُوا مَا بِأَنفُسِهِمْ ۙ وَأَنَّ اللَّـهَ سَمِيعٌ عَلِيمٌ﴿٥٣﴾
53. Hayo ni kwa kuwa Allaah Hakuwa Mwenye kubadilisha neema yoyote Aliyoineemesha kwa watu mpaka wao wabadilishe yaliyomo ndani ya nafsi zao; na kwamba Allaah ni Mwenye kusikia yote, Mjuzi wa yote.


كَدَأْبِ آلِ فِرْعَوْنَ ۙ وَالَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ ۚ كَذَّبُوا بِآيَاتِ رَبِّهِمْ فَأَهْلَكْنَاهُم بِذُنُوبِهِمْ وَأَغْرَقْنَا آلَ فِرْعَوْنَ ۚوَكُلٌّ كَانُوا ظَالِمِينَ﴿٥٤﴾
54. (Mwenendo wao ni) Kama mwenendo wa watu wa Fir’awn na wale wa kabla yao. Walikadhibisha Aayaat (ishara, hoja) za Rabb wao; Tukawaangamiza kwa (sababu ya) madhambi yao, na Tukawagharikisha watu wa Fir’awn; na wote walikuwa madhalimu.


إِنَّ شَرَّ الدَّوَابِّ عِندَ اللَّـهِ الَّذِينَ كَفَرُوا فَهُمْ لَا يُؤْمِنُونَ﴿٥٥﴾
55. Hakika viumbe viovu kabisa mbele ya Allaah ni wale waliokufuru nao hawaamini.


الَّذِينَ عَاهَدتَّ مِنْهُمْ ثُمَّ يَنقُضُونَ عَهْدَهُمْ فِي كُلِّ مَرَّةٍ وَهُمْ لَا يَتَّقُونَ﴿٥٦﴾
56. Ambao umepeana nao ahadi, kisha wanavunja ahadi yao kila mara, na wala hawana taqwa.


فَإِمَّا تَثْقَفَنَّهُمْ فِي الْحَرْبِ فَشَرِّدْ بِهِم مَّنْ خَلْفَهُمْ لَعَلَّهُمْ يَذَّكَّرُونَ﴿٥٧﴾
57. Basi mkiwashinda vitani (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم), wakimbize (waadhibu vikali ili) walio nyuma yao wapate kukumbuka (na kuwaidhika).


وَإِمَّا تَخَافَنَّ مِن قَوْمٍ خِيَانَةً فَانبِذْ إِلَيْهِمْ عَلَىٰ سَوَاءٍ ۚ إِنَّ اللَّـهَ لَا يُحِبُّ الْخَائِنِينَ﴿٥٨﴾
58. Na kama ukihofu khiyana kwa watu (mliofanya nao ahadi), basi watupie (ahadi yao) kwa usawa (kusiweko tena ahadi baina yenu). Hakika Allaah Hapendi makhaini.


وَلَا يَحْسَبَنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا سَبَقُوا ۚ إِنَّهُمْ لَا يُعْجِزُونَ﴿٥٩﴾
59. Na wala wasidhanie wale waliokufuru kwamba wao wamekwepa.  Hakika wao hawashindi kukwepa (adhabu ya Allaah).


وَأَعِدُّوا لَهُم مَّا اسْتَطَعْتُم مِّن قُوَّةٍ وَمِن رِّبَاطِ الْخَيْلِ تُرْهِبُونَ بِهِ عَدُوَّ اللَّـهِ وَعَدُوَّكُمْ وَآخَرِينَ مِن دُونِهِمْ لَا تَعْلَمُونَهُمُ اللَّـهُ يَعْلَمُهُمْ ۚ وَمَا تُنفِقُوا مِن شَيْءٍ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ يُوَفَّ إِلَيْكُمْ وَأَنتُمْ لَا تُظْلَمُونَ﴿٦٠﴾
60. Na waandalieni nguvu zozote mziwezazo na farasi waliofungwa tayari (kwa vita) muwaogopeshe kwayo maadui wa Allaah na maadui zenu, na wengineo wasiokuwa wao, hamuwajui, (lakini) Allaah Anawajua. Na chochote mkitoacho katika njia ya Allaah mtalipwa kikamilifu, nanyi hamtodhulumiwa.


وَإِن جَنَحُوا لِلسَّلْمِ فَاجْنَحْ لَهَا وَتَوَكَّلْ عَلَى اللَّـهِ ۚ إِنَّهُ هُوَ السَّمِيعُ الْعَلِيمُ﴿٦١﴾
61. Na kama (maadui) wakielemea kwenye amani basi (nawe pia) elemea; na tawakali kwa Allaah. Hakika Yeye ni Mwenye kusikia yote, Mjuzi wa yote.


وَإِن يُرِيدُوا أَن يَخْدَعُوكَ فَإِنَّ حَسْبَكَ اللَّـهُ ۚ هُوَ الَّذِي أَيَّدَكَ بِنَصْرِهِ وَبِالْمُؤْمِنِينَ﴿٦٢﴾
62. Na wakitaka kukuhadaa, basi Allaah Anakutosheleza. Yeye Ndiye Ambaye Amekusaidia kwa nusra Yake, na kwa Waumini.


وَأَلَّفَ بَيْنَ قُلُوبِهِمْ ۚ لَوْ أَنفَقْتَ مَا فِي الْأَرْضِ جَمِيعًا مَّا أَلَّفْتَ بَيْنَ قُلُوبِهِمْ وَلَـٰكِنَّ اللَّـهَ أَلَّفَ بَيْنَهُمْ ۚ إِنَّهُ عَزِيزٌ حَكِيمٌ﴿٦٣﴾
63. Na Akaunganisha nyoyo zao. Lau ungelitoa vyote vilivyomo ardhini, basi usingeliweza kuunganisha nyoyo zao; lakini Allaah Amewaunganisha. Hakika Yeye ni Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika, Mwenye hikmah wa yote.

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ حَسْبُكَ اللَّـهُ وَمَنِ اتَّبَعَكَ مِنَ الْمُؤْمِنِينَ﴿٦٤﴾
64. Ee Nabiy! Anakutosheleza Allaah na anayekufuata miongoni wa Waumini.


يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ حَرِّضِ الْمُؤْمِنِينَ عَلَى الْقِتَالِ ۚ إِن يَكُن مِّنكُمْ عِشْرُونَ صَابِرُونَ يَغْلِبُوا مِائَتَيْنِ ۚ وَإِن يَكُن مِّنكُم مِّائَةٌ يَغْلِبُوا أَلْفًا مِّنَ الَّذِينَ كَفَرُوا بِأَنَّهُمْ قَوْمٌ لَّا يَفْقَهُونَ﴿٦٥﴾
65. Ee Nabiy! Shajiisha Waumini kupigana vita. Wakiweko miongoni mwenu (Waumini) ishirini wanaosubiri, basi watawashinda (makafiri) mia mbili. Na wakiweko miongoni mwenu mia watawashinda elfu katika wale waliokufuru kwa kuwa wao ni watu wasiofahamu. 


الْآنَ خَفَّفَ اللَّـهُ عَنكُمْ وَعَلِمَ أَنَّ فِيكُمْ ضَعْفًا ۚ فَإِن يَكُن مِّنكُم مِّائَةٌ صَابِرَةٌ يَغْلِبُوا مِائَتَيْنِ ۚ وَإِن يَكُن مِّنكُمْ أَلْفٌ يَغْلِبُوا أَلْفَيْنِ بِإِذْنِ اللَّـهِ ۗ وَاللَّـهُ مَعَ الصَّابِرِينَ﴿٦٦﴾
66. Sasa Allaah Amekukhafifishieni na Amejua kwamba kati yenu kuna udhaifu. Hivyo basi wakiweko miongoni mwenu (Waumini) mia wenye kusubiri, watawashinda (makafiri) mia mbili; na wakiweko miongoni mwenu (Waumini) elfu, wawatashinda (makafiri) elfu mbili kwa idhini ya Allaah. Na Allaah Yu pamoja na wenye kusubiri.


مَا كَانَ لِنَبِيٍّ أَن يَكُونَ لَهُ أَسْرَىٰ حَتَّىٰ يُثْخِنَ فِي الْأَرْضِ ۚ تُرِيدُونَ عَرَضَ الدُّنْيَا وَاللَّـهُ يُرِيدُ الْآخِرَةَ ۗ وَاللَّـهُ عَزِيزٌ حَكِيمٌ﴿٦٧﴾
67. Haikumpasa Nabiy awe ana mateka mpaka apigane kuwaua na kuwajeruhi (maadui wa Allaah) nchini. Mnataka vitu vya dunia, na hali Allaah Anataka (mpate vya) Aakhirah. Na Allaah ni Mwenye enzi ya nguvu Asiyeshindika, Mwenye hikmah wa yote.


لَّوْلَا كِتَابٌ مِّنَ اللَّـهِ سَبَقَ لَمَسَّكُمْ فِيمَا أَخَذْتُمْ عَذَابٌ عَظِيمٌ﴿٦٨﴾
68. Lau kama si hukumu iliyotangulia (Majaaliwa na Makadirio) kutoka kwa Allaah; bila shaka ingekupateni kwa yale mliyoyachukua adhabu kuu.


فَكُلُوا مِمَّا غَنِمْتُمْ حَلَالًا طَيِّبًا ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۚ إِنَّ اللَّـهَ غَفُورٌ رَّحِيمٌ﴿٦٩﴾
69. Kuleni katika mlivyopata ghanima (ni) halaal (na ni) vizuri, na mcheni Allaah. Hakika Allaah ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu.


يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ قُل لِّمَن فِي أَيْدِيكُم مِّنَ الْأَسْرَىٰ إِن يَعْلَمِ اللَّـهُ فِي قُلُوبِكُمْ خَيْرًا يُؤْتِكُمْ خَيْرًا مِّمَّا أُخِذَ مِنكُمْ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ۗ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ﴿٧٠﴾
70. Ee Nabiy! Waambie wale waliomo mikononi mwenu katika mateka: “Kama Allaah Akijua kheri (yoyote) katika nyoyo zenu, Atakupeni ya kheri kuliko yale yaliyochukuliwa kutoka kwenu; na Atakughufurieni. Na Allaah ni Mwingi wa kughufuria, Mwenye kurehemu.


وَإِن يُرِيدُوا خِيَانَتَكَ فَقَدْ خَانُوا اللَّـهَ مِن قَبْلُ فَأَمْكَنَ مِنْهُمْ ۗ وَاللَّـهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ﴿٧١﴾
71. Na wakitaka kukufanyia khiyana, basi wao wamekwishamfanyia khiyana Allaah kabla na Akakupa kuwashinda. Na Allaah ni Mjuzi wa yote, Mwenye hikmah wa yote.


إِنَّ الَّذِينَ آمَنُوا وَهَاجَرُوا وَجَاهَدُوا بِأَمْوَالِهِمْ وَأَنفُسِهِمْ فِي سَبِيلِ اللَّـهِ وَالَّذِينَ آوَوا وَّنَصَرُوا أُولَـٰئِكَ بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ ۚ وَالَّذِينَ آمَنُوا وَلَمْ يُهَاجِرُوا مَا لَكُم مِّن وَلَايَتِهِم مِّن شَيْءٍ حَتَّىٰ يُهَاجِرُوا ۚوَإِنِ اسْتَنصَرُوكُمْ فِي الدِّينِ فَعَلَيْكُمُ النَّصْرُ إِلَّا عَلَىٰ قَوْمٍ بَيْنَكُمْ وَبَيْنَهُم مِّيثَاقٌ ۗ وَاللَّـهُ بِمَا تَعْمَلُونَ بَصِيرٌ﴿٧٢﴾
72. Hakika wale walioamini na wakahajiri (Muhaajirina) na wakafanya jihaad kwa mali zao na nafsi zao katika njia ya Allaah, na wale waliowapa makazi (Answaar) na wakanusuru (Dini ya Allaah); hao ni marafiki wandani wao kwa wao. Na wale walioamini lakini hawakuhajiri, hamna nyinyi wajibu wa kuwalinda lolote mpaka wahajiri. Na wakikuombeni msaada kwenu katika Dini, basi ni juu yenu kuwasaidia; isipokuwa juu ya watu mliofungamana mapatano baina yenu na wao. Na Allaah kwa myatendao ni Mwenye kuona.


وَالَّذِينَ كَفَرُوا بَعْضُهُمْ أَوْلِيَاءُ بَعْضٍ ۚ إِلَّا تَفْعَلُوهُ تَكُن فِتْنَةٌ فِي الْأَرْضِ وَفَسَادٌ كَبِيرٌ﴿٧٣﴾
73. Na wale waliokufuru ni marafiki wandani wao kwa wao. (Nanyi Waislamu) Msipofanya hivi itakuweko fitnah katika ardhi na ufisadi mkubwa.


وَالَّذِينَ آمَنُوا وَهَاجَرُوا وَجَاهَدُوا فِي سَبِيلِ اللَّـهِ وَالَّذِينَ آوَوا وَّنَصَرُوا أُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُؤْمِنُونَ حَقًّا ۚلَّهُم مَّغْفِرَةٌ وَرِزْقٌ كَرِيمٌ﴿٧٤﴾
74. Na wale walioamini na wakahajiri na wakafanya jihaad katika njia ya Allaah, na wale waliotoa makazi na wakanusuru, hao ndio Waumini wa kweli. Watapata maghfirah na riziki karimu.



وَالَّذِينَ آمَنُوا مِن بَعْدُ وَهَاجَرُوا وَجَاهَدُوا مَعَكُمْ فَأُولَـٰئِكَ مِنكُمْ ۚ وَأُولُو الْأَرْحَامِ بَعْضُهُمْ أَوْلَىٰ بِبَعْضٍ فِي كِتَابِ اللَّـهِ ۗ إِنَّ اللَّـهَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ﴿٧٥﴾
75. Na wale walioamini baada (ya hijra) na (pia) wakahajiri na wakafanya jihaad pamoja nanyi; basi hao ni miongoni mwenu. Na ndugu wa uhusiano wa damu wanastahikiana wenyewe kwa wenyewe (kwa kurithiana), katika shariy’ah (na hukmu) ya Allaah. Hakika Allaah kwa kila kitu ni Mjuzi.